Taasisi za Kiislamu nchini Nigeria zimeitaka serikali ya shirikisho ya nchi hiyo kukomesha ubaguzi inaowafanyia wanawake na wasichana wanaovaa vazi la staha la Hijab.

Tovuti ya habari ya Vanguard imeripoti kuwa, taasisi 13 za Kiislamu za Nigeria zimemtaka Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo pamoja na wakuu wake wa mikoa wakomeshe ubaguzi wanaofanyiwa wanawake na wasichana wa Kiislamu wanaovaa Hijab. Ubaguzi huo umekithiri sana kwenye sekta za elimu na ajira.

Katika mazungumzo yao na waandishi wa habari kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Hijab kwa mwaka huu wa 2022, taasisi hizo zimesema mjini Abuja kwamba, Hijab ni taji la vichwa vyetu, na si uhalifu kuvaa vazi hilo la staha. 

Akizungumza kwa niaba ya muungano wa taasisi hizo 13 za wanawake Waislamu nchini Nigeria, Hajiya Maryam Ahman amesema, kuna kesi nyingi za kubaguliwa na kunyapaliwa wasichana na wanawake Waislamu wanaojistahi na kuchunga vazi la Hijab. Nyingi ya kesi hizo zimeripotiwa katika majibo ya Kwara na Ogun, pamoja na katika kambi ya askari cha NYSC huko Akwa Ibom. 

Amesema, udhalilishaji wa kidini umeshika kasi na kuongezeka sana nchini Nigeria hivi sasa na kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua za haraka za kukabiliana nao.

Katika sehemu moja ya matamshi yake, Hajiya Maryam amesema: Tunaliomba Bunge la Taifa kuwasilisha na kupasisha sheria itakayochunga haki za wananchi wote na kulinda haki na uhuru wao bila ya kubaguliwa hasa katika sekta za elimu, afya, ajira, fedha, umiliki wa mali, n.k, na bila ya kujali mavazi yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!