بسم الله الرحمن الرحيم

وَ ما يَسْتَوِي الْأَعْمى‏ وَ الْبَصِيرُ (19) وَ لا الظُّلُماتُ وَ لا النُّورُ (20) وَ لا الظِّلُّ وَ لا الْحَرُورُ (21) وَ ما يَسْتَوِي الْأَحْياءُ وَ لا الْأَمْواتُ إِنَّ اللَّهَ يُسْمِعُ مَنْ يَشاءُ وَ ما أَنْتَ بِمُسْمِعٍ مَنْ فِي الْقُبُورِ (22) إِنْ أَنْتَ إِلاَّ نَذِيرٌ (23)

Tarjuma kutoka al Muntakhab ya Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani

19. Na kipofu na mwenye kuona hawalingani. 20. Wala giza na mwangaza. 21. Wala kivuli na joto. 22 Wala hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini. 23. Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.

Ndugu yangu, aya hizo 5 ni muendelezo wa aya zilizopita za kuwajadili walioamini na waliokufuru katika aya za kabla ya hizi. Nimechagua kuzichambua kiujumla hapa aya hizi kwa kunukuu yaliyosemwa na wanavyuoni wa Tafsiri za Qur’ani Tukufu, kutokana na mfananisho wa aina yake kabisa uliomo kwenye aya hizo. Kwanza kabla ya yote tuelewe kwamba, katika mantiki ya itikadi ya dini tukufu ya Uislamu, kuna makundi mawili tu ya wanadamu, kuna Waislamu na wasio Waislamu. Na anayetafuta dini siyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. (Aal Imran 3:85). Hiyo ndiyo mantiki ya dini tukufu ya Kiislamu. Kwa hivyo mipaka ya kijiografia, kikabila, kitaifa, kinchi, kikaumu, kirangi, kilugha, kitajiri, kimaskini, kielimu na wasio na elimu ambayo wanadamu tumejiwekea, haizingatiwi na Mwenyezi Mungu katika malipo ya amali za waja wake. Kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa jitihada zake bila ya kuzingatia mipaka yote hiyo ila miwili, ya mwenye kuamini na asiyeamini yaani Muislamu na kafiri. Hiyo ni nukta moja kati ya nyingi zilizomo kwenye aya hizo, nimeona niitangulize hiyo kutokana na umuhimu wake.

Kabla ya kuelezea nukta nyingine na kabla ya kuangalia uhakika wa yaliyotajwa na Qur’ani Tukufu katika aya hizo, ninapenda hapa ninukuu yaliyoelezwa kiujumla kuhusu uhandisi mkubwa wa kibalagha wa aya hizo. Twende pamoja.

1 – Katika mifano minne iliyopigwa kwenye aya hizo za 19 hadi 22 za Surat Fatir, kumetolewa nadharia nyingi na wanachuoni wa Tafsiri. Nitataja baadhi yake. Kwanza maneno A’amaa na Basir pamoja na Dhil na Harur yamekuja kwa sura ya umoja. Lakini maneno Ahyaa na Amwat yote mawili yamekuja kwa sura ya wingi. Halafu katika mfano mwingine, neno dhulumat limekuja kwa sura ya wingi na neno nur limekuja kwa sura ya umoja.

2 – Jengine lililochambuliwa ni kwamba katika mfano wa kwanza na wa pili, sigha ya hasi imetangulia yaani maneno A’amaa na Dhulumat wakati katika mifano ya tatu na nne sigha ya chanya ndiyo iliyotangulia yaani Dhil (kivuli) na Ahyaa.

3 – Jambo la tatu lililochambuliwa ni kwamba katika mfano wa kwanza herufi ya kukataa Maa haikurudiwa lakini katika mifano mitatu mingine herufi za kukataa za Laa zimerudiwa.

4 – Jambo la nne lililojadiliwa ni kwamba maneno “Maa Yastawi” yametumika tu kwenye mfano wa kwanza na wa mwisho, hayaonekani kwenye mifano miwili ya katikati.

Wafasiri wametoa sababu mbalimbali za kuweko tofauti hizo. Baadhi yake ni za kutiliwa maanani na hapa tutataja baadhi ya hizo.

Miongoni mwa uchambuzi huo ni ule unaosema sababu ya neno dhulumat kuja kwa sigha ya wingi yaani plural, na sababu na neno nur kuja kwa sura ya umoja yaani singular, ni kama tulivyosema mwanzoni mwa kuandika makala hii kwamba, nuru hapa maana yake ni Uislamu, Uislamu nao ni mmoja tu. Mungu wake ni Mmoja, Mtume wake ni mmoja, Kitabu chake ni kimoja, Kibla chake ni kimoja na Waislamu wote ni sawa na mwili mmoja. Lakini ukafiri una matawi na chanjaa nyingi zisizo na idadi na miungu yao pia si mmoja, zina miungu zaidi ya mmoja. Uislamu ni njia moja tu iliyonyooka ya uongofu lakini ukafiri umejaa njia zinazogongana na zilizogawika kwenye maelfu ya matawi ya upotofu.

Uchambuzi mwingine ni ule unaosema, sababu ya mfano wa kwanza na wa pili  kuanza kwa maneno ya hasi (negative) ni ishara ya kipindi cha mwanzoni mwa kudhihiri dini tukufu ya Uislamu ambapo washirikina wa Makkah walikuwa wameghariki kwenye upofu wa ujahilia na kiza cha shirki, na baadaye wakaongoka kwa kumwilikiwa na nuru ya Uislamu. Lakini mifano mingine miwili inahusiana na hatua ya baada ya hapo. Yaani baada ya Uislamu kuimarika na kuzitawala nyoyo za watu wengi na kueneza baraka na neema zake katika jamii. Hivyo maneno yaliyotangulia ni chanya yaani positive katika mifano miwili ya mwisho ya aya hizo.

Tukiachana na yote hayo, lililo muhimu zaidi kuliko kila kitu ni umbuji na umahiri mkubwa sana wa Qur’ani Tukufu wa kubainisha mambo na kubakisha utamu na mvuto wake mkubwa wa kila namna kuanzia matumizi yake ya maneno bora kabisa, vibwahizo vyake, utangulizi wa maneno na balagha kubwa mno ambayo kadiri tutakavyosema, hatuwezi kufikia mwisho bali akili zetu pia haziwezi kudiriki ipasavyo ukubwa wa balagha na ufasaha huo. Majimbi wa lugha huwaoni wakirudia neno hilo kwa hilo isipokuwa penye udharura wa kufanya hivyo. Qur’ani Tukufu ina viwango vya juu mno vya balagha na ufasaha wa maneno.

Kila mtu na zama zake anaweza kuibua lulu za thamani kubwa sana kwenye maneno na aya za Qur’ani Tukufu kadiri zama na muda unavyopita. Naam, kadiri muda unavyopita, ndivyo Qur’ani Tukufu inavyozidi kuwa mpya na yenye manufaa makubwa zaidi, haizeeshwi na kupita kwa wakati.

Namna hivi ndugu yangu ndivyo tunavyopaswa kuzisoma aya za Qur’ani Tukufu na kuwafundisha wengine. Tuisoma kwa namna ya kutuathiri katika matendo yetu tusiwe miongoni mwa ambao Mtume atakwenda kuwashitaki mbele ya Allah kwa kuifanya Qur’ani ni mahame.

Kuna mijadala mingine kadhaa imebakia kuhusu aya hizo na mifano yake. Hikma ya vilivyofananishwa. Je, maiti hasikii? Tukifanye nini kisa cha maiti wa vita vya Badr? Kwa nini yatumike maneno hayo yasitumike ujinga na werevu katika aya hizo kwa mfano? Hikma yake ni nini? Yote hayo tukipata nafasi tutayachambua katika sehemu zitakazofuata za makala hii InshaAllah.

Ndugu yako, Ahmed Rashid.

(Visited 17 times, 1 visits today)
One thought on “Tafsiri ya kina ya Aya za 19 hadi 23 za Sura ya 35 ya Fatir (Sehemu ya Kwanza)”
  1. […] Ndugu yangu, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tulisema kuwa, aya hizo 5 ni muendelezo wa aya zilizopita za kuwajadili walioamini na waliokufuru katika aya za kabla ya hizi. Nimeamua kuzijadili hapa kutokana na balagha kubwa iliyomo ndani yake, mfananisho wa kipekee na nuru iliyoenea ndani ya aya za Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani. Sehemu ya kwanza ya makala hii inapatikana kwenye link hii: https://ahramed14.com/tafsiri-ya-aya-za-19-hadi-23-za-sura-ya-35-ya-fatir-sehemu-ya-kwanza/ […]

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!