بسم الله الرحمن الرحيم

وَ ما يَسْتَوِي الْأَعْمى‏ وَ الْبَصِيرُ (19) وَ لا الظُّلُماتُ وَ لا النُّورُ (20) وَ لا الظِّلُّ وَ لا الْحَرُورُ (21) وَ ما يَسْتَوِي الْأَحْياءُ وَ لا الْأَمْواتُ إِنَّ اللَّهَ يُسْمِعُ مَنْ يَشاءُ وَ ما أَنْتَ بِمُسْمِعٍ مَنْ فِي الْقُبُورِ (22) إِنْ أَنْتَ إِلاَّ نَذِيرٌ (23)

Tarjuma kutoka al Muntakhab ya Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani

Kwa jina la Allah Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

(19) Na kipofu na mwenye kuona hawalingani. (20) Wala giza na mwangaza. (21) Wala kivuli na joto. (22) Wala hawalingani walio hai na maiti. Hakika Mwenyezi Mungu humsikilizisha amtakaye. Wala wewe si wa kuwasikilizisha walio makaburini. (23) Hukuwa wewe ila ni mwonyaji.

Ndugu yangu, Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tulisema kuwa, aya hizo 5 ni muendelezo wa aya zilizopita za kuwajadili walioamini na waliokufuru katika aya za kabla ya hizi. Nimeamua kuzijadili hapa kutokana na balagha kubwa iliyomo ndani yake, mfananisho wa kipekee na nuru iliyoenea ndani ya aya za Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani. Sehemu ya kwanza ya makala hii inapatikana kwenye link hii: https://ahramed14.com/tafsiri-ya-aya-za-19-hadi-23-za-sura-ya-35-ya-fatir-sehemu-ya-kwanza/

Amma katika sehemu hii ya pili tutajikita zaidi katika kuangalia hikma ya Qur’ani Tukufu ya kutaja mifano hiyo minne kwa mpangilio huo. Yaani haukutangulia mfano wa nuru na kiza mbele ya kipofu na mwenye kuona n.k. Tuanze na kutupia jicho maneno yaliyotumika katika mifano hiyo minne.

Kwa nini yakafananishwa maneno ya asiyeona na anayeona? Sehemu ya kwanza ya makala hii tumenukuu yaliyosemwa na wanavyoni kuhusu kwa nini limetangulia neno A’amaa (kipofu) kabla ya neno Basir (mwenye kuona) au aliyeko kwenye kiza na aliyeko kwenye nuru. Je, wawili hawa wanafanana? Mfananisho mwepesi na wa wazi kabisa, lakini mwanadamu hataki kuelewa. Nuru kwa maana ya Muislamu na giza kwa maana ya kafiri yaani asiye Muislamu. Sehemu ya kwanza tumesema, kwa mantiki ya Uislamu na Qur’ani Tukufu, wanadamu wako wa aina mbili tu, walioamini na wasioamini. Hakuna kundi la tatu.

Naam, kuwa na imani sahihi ya Mwenyezi Mungu ni nuru, ni kuwa na mwangaza.   Nuru hiyo humuongoza vizuri mwanadamu katika kumtambua ipasavyo Muumba wa ulimwengu, katika itikadi zake, matendo na maisha yake yote. Lakini ukafiri ni kiza au giza ndani ya giza hilo, mwanadamu hawezi kupata kabisa mtazamo sahihi kuhusu Muumba wa ulimwengu, hawezi kamwe kuwa na itikadi sahihi; na vitendo vyake pia haviwi sawa. Na anayetafuta dini siyokuwa Uislamu haitakubaliwa kwake. Naye Akhera atakuwa miongoni mwa waliokhasirika. (Aal Imran 3:85). Vile vile aya ya 257 ya Sura ya Pili ya al Baqarah inasema: Mwenyezi Mungu ni Mlinzi wa walioamini. Huwatoa gizani na kuwaingiza mwangazani. Lakini waliokufuru, walinzi wao ni mashet’ani. Huwatoa kwenye mwangaza na kuwaingiza gizani. Hao ndio watu wa Motoni, na humo watadumu.

Katika sehemu ya kwanza ya makala hii tulisema maneno “Wamaa Yastawi” yametumika kwenye mfano wa kwanza na wa nne, hayakutumika kwenye mfano wa pili na wa tatu. Ni kama vile Qur’ani inatutaka tuzingatie kwa kina mjadala ulioanza na maneno hayo. Aidha ni kama vile Qur’ani Tukufu inataka kutueleza hatua anazopitia mwanadamu kufikia kwenye nuru na uongofu kama tulivyonukuu mitazamo ya wanachuoni kenye sehemu ya kwanza ya makala hii.

Naam, mfano wa pili ni “kiza na nuru.” Hapa pia limetangulia neno kiza yaani neno hasi (negative) mbele ya neno chanya (positive) la nuru. Sehemu ya kwanza tumenukuu mtazamo wa hikma ya kuwa hivyo.

Ni ukweli usiopingika kuwa giza na nuru havifanani kabisa. Kiza ni chimbuko la upotofu. Giza hukwamisha na kusimamisha kila kitu. Kiza ni sababu ya aina kwa aina ya hatari. Lakini nuru na mwangaza ni chimbuko la maisha, harakati za viumbe wema, ustawi, ukamilifu na makuzi ya kheri. Ndugu yangu, hebu fikiria iwapo duniani kusingelikuwa na nuru ya aina yoyote, dunia ingelikuwa na hali gani. Maisha ya mwanadamu yangelikuwaje? Ndio maana, kuwa na macho tu hakutoshi, macho yanahitajia nuru. Mfano wa pili wa nuru na kiza umekuja baada ya kutajwa macho katika aya ya 19 ya sura hiyo. Allahu Akbar, ufasaha na balagha kubwa iliyoje ya Qur’ani Tukufu.

Mfano wa tatu ni wa kulinganishwa kivuli na upepo wa joto kali. Je aliyeko kivulini na aliyeko “kibangauwani” chini ya upepo wa joto kali usio na kivuli chochote, wanafanana? Ni wazi kwamba hawafanani kabisa. (Wala dhilli walal harur). Hapa sasa neno “kivuli” – dhil – ambalo ni chanya (posivite) limetangulia neno “upepo wa joto kali” – harur – ambalo ni hasi (negative). Sijui ndugu yangu tuko pamoja? Ni kama vile tunapanda ngazi kuelekea kwenye ukamilifu uliokusudiwa na Mwenyezi Mungu. Tumetoka kenye macho, lakini macho hayafanyi kazi bila ya nuru, lakini kuwepo nuru bila ya utulivu, mambo hayawi. Allahu Akbar! Balagha na ufasaha wa hali ya juu kabisa wa Qur’ani Tukufu. Muislamu huwa yuko chini ya kivuli kinachompa utulivu na usalama wa moyo kutokana na yakini ya imani yake. Lakini kafiri siku zote yuko kwenye hofu na wasiwasi kutokana na kutokuwa na yakini na yatakayomkuta baada ya maisha haya ya hapa duniani. Usione wasio na imani sahihi ya Muumba wa ulimwengu wanacheka na kujionesha wako kwenye furaha kubwa. Nyoyo zao hazina utulivu hata kidogo na ndio maana mara zote wanaficha hofu hizo kenye bilauri za pombe na kuchupa mipaka ya Mwenyezi Mungu na kamwe hawapati utulivu.

Hebu tuangalie kidogo upande wa lugha. Raghib katika kitabu chake cha al Mufradat anasema, kwa upande wa sarfa, neno harur limekuwa kwenye mizani ya qabul na maana yake ni upepo wa moto, mkali na unaochoma. Upepo angamizi na unaokausha kila kitu.

Hata hivyo, wengine wamesema, harur ni upepo kama wa samum na wengine wakasema ni joto la jua kali.

Al Zamakhshari katika kitabu cha al Kashaf anasema, “samum” ni upepo unaoumiza na kuua ambao hupiga nyakati za mchana, lakini “harur” ni upepo huo wa samum lakini unaovuma usiku na mchana.

Alaakullihaal, tusitoke sana kwenye maudhui ya sehemu hii ya pili ya kufasiri aya hizi za 19 hadi 23 za sura ya 35 ya al Fatir. Katika sehemu hii ya pili tumejikita zaidi katika hikma ya kupangiliwa namna hivi mifano hiyo minne pamoja na maelezo yake mengine. Hivyo niseme kwamba, yeyote mwenye akili timamu hawezi kubakia hata sekunde kwenye upepo wenye joto kali linalokausha kila kitu yaani ukafiri, wakati mbele yake anaona pana kivuli ambacho ni rahisi sana kukifikia, ni kipana kupindukia na kinatuliza kabisa nyoyo za waliojikabidhi kwa kivuli hicho yaani Uislamu. Wasio na imani ya kweli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, hawana uvumilivu kabisa katika maisha yao, kitu kidogo tu kwao ni kikubwa, utadhani mbingu zimewaangukia.

Amma mfano wa nne na wa mwisho katika aya hizi tukkufu ni kupigwa mfano wa mtu aliye hai na mtu aliyekufa, je, wanafanana? (وَ ما يَسْتَوِي الْأَحْياءُ وَ لَا الْأَمْواتُ) Tab’an hawafanani kabisa. Sasa sifa za mtu hai ni zipi na sifa za mfu ni zipi? Kwa mantiki ya Qur’ani, si kila anayetembea yu hai na si kila aliyeondoka duniani ni maiti na mfu. Wala kabisa usiwadhanie waliouliwa katika Njia ya Mwenyezi Mungu kuwa ni maiti. Bali hao wako hai, wanaruzukiwa kwa Mola wao Mlezi.  (Aal Imra 3:169).

Sasa kutokana na utaratibu huu wa kutajwa kwa mpangilio namna hii mifano minne ya Qur’ani Tukufu tunasomeshwa na Qur’ani Tukufu maana halisi ya mtu aliye hai na mtu aliyekufa. Mtu aliye hai ni mwenye macho, macho yenye nuru, nuru iliyoko chini ya kivuli cha utulivu bila ya wahka. Amma mtu aliyekufa hata kama tunamuona anatembea ni yule ambaye macho yake hayaoni nuru, bali yanaona kiza, yuko chini ya joto kali, linalochoma vibaya, lakini kwa ujinga na upofu wake, akili yake haimtumi kwenda kujificha kwenye kivuli chepesi kukifikia yaani Uislamu na chenye neema zisizo na kikomo. Huyo ndiye mfu, na huyo ndiye maiti kwa mantiki ya Qur’ani Tukufu.

Hapa nigusie pia kwamba hili neno dhil yaani kivuli ni katika neema kubwa za peponi. Aya za 55 na 56 za sura ya 36 ya Yaasin zinasema: 55. Hakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi. 56. Wao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.

Lakini kingine tunachofundishwa na Qur’ani Tukufu kwenye mfano huu wa nne hapa ni kwamba, Waislamu hawatakiwi wawe wavivu na magoigoi. Uislamu maana yake ni maisha. Uislamu maana yake ni harakati. Uislamu maana yake ni kuwa amilifu (active) muda wote. Uislamu maana yake ni ustawi. Uislamu ni mti ambao matunda yake mazuri hayamaliziki katika misimu yote. Macho ya Muislamu yanaona, yana nuru, yana utulivu, yako chini ya kivuli cha kheri, hakuna sababu ya kwa nini Waislamu waweko nyuma kimaendeleo.

Lakini kafiri yeye ni kama gogo kavu lisilo na uhai wowote, lisiloota majani, wala maua, wala kuzaa matunda, wala kutoa kivuli. Halina faida nyingine ila kugeuzwa kuni na kupigwa moto katika upepo mkali wa harur unaochoma na kuunguza kila kitu. Aya ya 122 ya Sura ya 6 ya al An’am, Qur’ani Tukufu inasema: Je, aliyekuwa maiti kisha tukamhuisha, na tukamjaalia nuru inakwenda naye mbele za watu, mfano wake ni kama aliyeko gizani akawa hata hawezi kutoka humo? Kama hivyo makafiri wamepambiwa waliyokuwa wakiyafanya.

Naam katika sehemu ya tatu ya tafsiri hii ya kina ya aya za 19 hadi 23 za Sura ya 35 ya Fatir na ambayo tunataraji itakuwa ya mwisho, tutaangalia masuala mengine ikiwa ni pamoja na lile tuliloligusia kwenye sehemu ya kwanza ya makala hii yaani kusemezwa watu waliokufa.

Namuomba Allah atupe taufiki ya kuisoma kwa kina Qur’ani Tukufu, tuielewe na kuifanyia kazi.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Ndugu yako, Ahmed Rashid.

(Visited 61 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!