بِسۡمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِیمِ

قُلۡ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلۡكَـٰفِرُونَ ۝  لَاۤ أَعۡبُدُ مَا تَعۡبُدُونَ ۝  وَلَاۤ أَنتُمۡ عَـٰبِدُونَ مَاۤ أَعۡبُدُ ۝  وَلَاۤ أَنَا۠ عَابِدࣱ مَّا عَبَدتُّمۡ ۝  وَلَاۤ أَنتُمۡ عَـٰبِدُونَ مَاۤ أَعۡبُدُ ۝  لَكُمۡ دِینُكُمۡ وَلِیَ دِینِ

Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnachokiabudu; Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu. [Surah Al-Kafirun 1 – 6]

Bismillahir Rahmanir Rahim.

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Nimekusudia kutawakali kwa Mwenyezi Mungu ili anipe taufiki ya kusema ya maana kuhusu sura hii tukufu. Hivyo kabla ya kuendelea nakuomba katika usiku wa Ijumaa, tia nia ya kutoa zawadi thawabu unazopata wakati unasoma haya, zawadi hiyo imfikie kipenzi chetu, ruwaza yetu, kigezo chetu mbora wa viumbe wote, Mtume Muhammad SAW.

Thawabu hizo tutie nia ziende pia kwa mawalii wa Mwenyezi Mungu, masahaba walio wema wa Mtume, wanavyuoni walioupigania Uislamu, walimu wetu na wazazi wetu waliotulea vyema mpaka leo tumepata nguvu za kujumuika kwenye group hili la madrasa. Tia nia pia ya kufika thawabu zake kwa wazazi wako wawili, wawe hai au wawe mbele ya Haki. Kusoma tu Qur’ani ni ibada, hata kama hujui maana yake. Thawabu ziwafikie pia Waislamu na waumini, walio hai na walio mbele ya Haki.

Niingie sasa kwenye tafsiri ya Surat al Kafirun.

Maelezo jumla kuhusu sura hiyo:

Surat al Kafirun ni ya 109 katika mpangilio wa sura za Qur’ani Tukufu. Iliteremshwa Makkah. Iliteremshwa baada ya Surat al Maun. Ina aya sita. Ina maneno 27 ina herufi 99.

Fadhila za Surat al Kafirun:

Katika Tafsiri ya Qur’ani ya Majmaa al Bayan, kumenukuliwa hadithi kutoka kwa Mtume SAW akisema: Anayesoma Surat al Kafirun, mbali na thawabu nyingine, hupata mambo manne. Kwanza huwa ni kama amesoma robo ya Qur’ani. Pili shetani hukimbia akawa mbali naye. Tatu imani yake husafishwa na shirk. Na nne huepushwa na hofu ya Siku ya Kiama

Kutajwa fadhila hizo nne katika hadithi hiyo ya Mtume SAW, huenda ni kwa sababu, karibu robo nzima ya aya za Qur’ani ni kupinga shirk. Sura hii ni tangazo la wazi kabisa la kupinga shirk. Shetani anakimbia ukisoma sura hiyo kwa sababu shetani hakai penye ibada ya kweli ya Mungu Mmoja. Pia kukanusha ibada zote isipokuwa ya Mungu Mmoja ndiyo imani ya kweli na ndiye mwokozi wa adhabu na hofu ya Siku ya Kiyama

Tangu tu wadogo, wazee wetu wakitufundisha mtu usilale bila ya kusoma Sura za al Kafirun, al Ikhlas, al Falaq na an Nas. Pamoja na Bismillahir Rahmanir Rahim mara 21. Nimeona hadithi inayohimiza jambo hilo. Pia huko ni katika kuzilea na kuzilainisha mapema nafsi za watoto na kuzitoa kwenye hatua hatari na kuipandisha juu hatua kwa hatua

Fadhila za sura hii ni nyingi sana. Ninukuu hadithi nyingine kwamba anayesoma Surat al Kafirun, wakati wa kuchomoza na kuzama jua, hutakabaliwa dua yake yoyote iliyotimiza masharti kama yale tuliyoyagusia humu hivi juzi. Ukirudi huko juu utayaona.

Sura hiyo na qul audhu mbili na qul huwaLaah ni kinga nzuri sana safarini kama ambavyo Mtume SAW alivyomfundisha Sahaba Khubair. Tuishie hapo kuhusu fadhila za sura hii. Kuna mengi ya kusema.

Natamani elimu jumla kama hizi wasomeshwe vijana wetu kila siku, wakati wakiingia na kutoka chuoni, ili tuzilainishe mapema nafsi zao. Kwa mfano, mwanafunzi ukimuuliza tu Sura ya 114 ya Qur’ani ni ipi, aseme. Imeshuka wapi, aseme, ina aya ngapi, aseme, inahusu nini? Aseme n.k. Wakikulia hivyo watakuwa kamusi za Qur’ani.

Sababu ya kushuka Sura ya 109 ya al Kafirun:

Nitosheke na haya:

جاء في سبب نزول هذه السورة أن كفار قريش عرضوا على النبي، صلى الله عليه وسلم، أن يعبدوا الله سبحانه وتعالى ويقبلوا ما جاء به، بشرط أن يشاركهم في عبادة آلهتهم الباطلة بعض الزمان، فنزلت هذه السورة تقطع كل مفاوضات لا تفضي إلى تحقيق التوحيد الكامل لله رب العالمين

Nitatoa tarjama jumla sana tu. Imepokewa kuhusu sababu ya kushuka sura hii kwamba Muquraish wa Makka walikwenda kwa Mtume wakampendekezea kufanya ibada kwa zamu, baadhi ya wakati waabudu masanamu, baadhi nyingine wamwabudu wa Allah, likaja jibu kali la kupinga kabisa jambo hilo.

Yameelezwa mambo mengi. Mpaka idadi ya mara walizomtaka Mtume kufanya jambo hilo, lakini tusiende huko kwanza. Hilo neno al Kafirun si nakra, ni maarifa, kwa nini? Mjadala huo umeingizwa pia kwenye sababu za kuteremshwa sura hiyo. Hata hivyo tutosheke na hapo.

Uhandisi wa Surat al Kafirun:

Turejee kuisoma hii sura tukufu.

بِسۡمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحۡمَـٰنِ ٱلرَّحِیمِ

 قُلۡ یَـٰۤأَیُّهَا ٱلۡكَـٰفِرُونَ ۝  لَاۤ أَعۡبُدُ مَا تَعۡبُدُونَ ۝  وَلَاۤ أَنتُمۡ عَـٰبِدُونَ مَاۤ أَعۡبُدُ ۝  وَلَاۤ أَنَا۠ عَابِدࣱ مَّا عَبَدتُّمۡ ۝  وَلَاۤ أَنتُمۡ عَـٰبِدُونَ مَاۤ أَعۡبُدُ ۝  لَكُمۡ دِینُكُمۡ وَلِیَ دِینِ

Ukanushaji umekuja mara nne yaani hizo “LA” na “WALA” ndio maana jina jingine la sura hiyo likawa:

سورة الجحد

Neno ibada katika minyambuliko tofauti limekuja mara nane ndio maana ikaitwa pia:

سورة العبادة

UCHAMBUZI ZAIDI

Kuna mjadala mpana sana kuhusu sura hii. Sana tena. Kuanzia hikma ya kuanza neno Qul, mpaka waliyadin. Kwa nini maneno yamerudiwa rudiwa. Wanafiki na wanaopiga vita Qur’ani wanasemaje kuhusu sura hiyo. Kwa nini neno al Kafurun likafuatiwa na Alif na Lam. Kwa nini likatumika neno la al Kafirun wakati waliokwenda kwa Mtume walikuwa Makureishi ambao ni maarufu kwa jina la washirikina wa Makkah. Uhusiano wa yaliyomo humo na tangu kuumbwa Nabii Adam hadi Siku ya Kiama. Hilo neno dini humu limefasiriwa vipi na maswali mengi sana. Hatuwezi kumaliza.

Nitachupia chupia kiduchu kiduchu ili nigusie mambo ya kutosha.

1 – Tuanze na hikma ya kutumika neno Qul. Wapinzani wa Qur’ani wanasema, kulikuwa na haja gani kuja neno qul, wakati mjadala ulikuwa ni baina ya Mtume mwenyewe na washirikina wa Kikuraishi? Majibu yaliyolewa yamo humo humo. Kwanza hii ni kuthibitisha kwamba kila kilichomo ndani ya Qur’ani ni maneno ya Mwenyezi Mungu hamna hata herufi moja iliyoongezwa. Malaika Jibril AS alimfikishia Mtume kila herufi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mtume naye akatufikishia  kikamilifu, kila herufi aliyoipokea. Kuna ushahidi mwingi wa namna hiyo ndani ya Qur’ani Tukufu. Pili wafasiri wanasema, kama neno qul lisingelikuwepo, huo ukanushaji ungelikuwa ni wa Mwenyezi Mungu Mwenyewe maana Qur’ani nzima ni maneno ya Allah. Sasa kama ukanushaji ungelikuwa ni wa Mwenyezi Mungu Mwenyewe, maneno yaliyofuatia tungeliyafasiri vipi? Kama hayo “Siabudu mnachoabudu?” Mwenyezi Mungu ni Muabudiwa haabudu chochote.

2 – Baada ya kugusia sababu za kutumika neno “qul” katika sura hiyo ya 109 ya al Kafirun, sasa tuingie kwenye swali la pili nalo ni kwa nini ikatumika Alif na Lam katika neno al Kafirun?

Majibu yake yako wazi, ni kwa sababu si Makuraishi wote waliokwenda kujadiliana na Mtume, bali ni baadhi ya wakuu wa makabila ya Kikuraish kama Walid bin Mughera, Aas bin Wail, Harith bin Qeis, Umayyah bin Khalaf n.k. Ni kundi tu la makafiri wa Kikuraish, si wote. Kwa hivyo imekuja kwa Alif na Lam kuwalenga makafiri maalumu, tab’an maudhui yake hiyo inahusu makafiri wote wa zama hizo, za kabla yake na za baada yake mpaka siku ya mwisho.

3 – Kwa nini likatumika neno makafiri na si Makuraish wakati waliomfuata Mtume walikuwa ni Makureish?

Jawabu:

Ingawa waliokwenda kuonana na Mtume ni kundi dogo la wakuu wa Kikuraish, lakini msimamo huu wa Mtume hauwahusu tu Makuraish wa Makka. Ni msimamo wa kiitikadi unaohusu zama zote na wanadamu wote. Vile vile kwa mujibu wa Uislamu, imani ziko aina mbili tu, imma imani ya Mungu Mmoja nayo ni ya Uislamu, au imani ya miungu wengine nayo ni ya kikafiri. “Anayetafuta dini isiyokuwa Uislamu, haitokubaliwa kwake…” Hivyo kilichopo ni dini ya Uislamu mkabala na dini zisizo za Uislamu ambazo ni nyingi na zote ni za kikafiri. Hivyo maneno hapa yanawahusu makafiri wote si Makuraish peke yao. Kama Qur’ani ingelisema Enyi Makuraish! Aya hiyo ingeliishia zama hizo hizo na isingetugusa sana watu wa zama za baadaye wala kabla yake. Inaonekana wazi kuwa, Qur’ani hapo inataka kuonesha kuwa Makuraish waliokwenda kutoa pendekezo hilo kwa Mtume waliwakilisha makafiri wote duniani na Mtume aliwakilisha Waislamu wote yaani kila anayeabudu Mungu Moja, Allah, Muumba wa kila kitu.

Nukta nyingine ya kuzingatia hapa ni kwamba, imani ya Kiislamu baadhi ya wakati inatakiwa kutolewa kwa uwazi bila ya kumuogopa kiumbe yoyote hata kama idadi ya Waislamu ni chache. Katika mazingira kama hayo na licha ya kwamba Waislamu walikuwa ni wachache na dhaifu wakati ilipoteremshwa sura hiyo, lakini Bwana Mtume Muhammad SAW hakutetereka na alitangaza hadharani kuwa Enyi makafiri, msimamo wangu ni huu, mimi kamwe sijawahi kuabudu, siabudu na katika siku za usoni pia sitoabudu ila Mungu Mmoja tu. Hakuna uhusiano wowote baina ya imani yangu ya tawhidi ya Mungu Mmoja na imani yenu ya shirk.

4 – Je, wanaoabudu masanamu wanakanusha kuwepo Mwenyezi Mungu?

Jawabu:

Tunajua wazi kuwa, wanaoabudu masanamu hawakanushi kuwepo Mwenyezi Mungu. Aya ya 25 ya Surat Luqman inasema wazi kwamba: “Na ukiwauliza: Nani aliyeziumba mbingu na ardhi? Bila ya shaka watasema: Ni Mwenyezi Mungu. Wewe sema: Alhamdulillahi! Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu. Lakini wengi wao hawajui.”

Swali:

Kama ni hivyo, kwa nini Surat al Kafirun inasema: Mimi siabudu mnachokiabudu na wala nyinyi hamumwabudu ninayemwabudu?

Jawabu:

Kuna tofauti baina ya aya hizi za Surat al Kafirun ya 109 na ile aya ya 25 ya sura ya 31 ya Luqman. Kule katika Surat Luqman kinachozungumziwa ni Muumba lakini hapa kinachozungumziwa ni ibada. Ni wazi kwamba wanaoabudu masanamu wanakiri kuweko Mungu aliyeumba dunia na vilivyomo. Tatizo lao ni nani anayepasa kuabudiwa. Itikadi yao ni kwamba inabidi waabudu masanamu ili ibada yao hiyo iwaweke karibu na Mwenyezi Mungu. Hapa ndipo penye tofauti kubwa na ya kimsingi baina ya Waislamu na makafiri. Waislamu wanaamini kuwa anayepaswa kuabudiwa ni Mungu Mmoja tu Muumba wa kila kitu na hakuna kiumbe chochote kinachopasa kuabudiwa. Yeyote anayeabudu chochote na kumwacha Mwenyezi Mungu au kumshirikisha Mwenyezi Mungu, huyo ni kafiri na yuko upande mwingine tofauti kabisa na Uislamu haijalishi aina ya miungu inayoabudiwa na makafiri hao. Iwe ni mwanadamu, iwe mizimu, iwe masanamu, iwe jua, iwe mwezi, iwe chochote kile, zote ibada hizo ni haramu, ni za kikafiri na hazikubaliwi kabisa na Uislamu.


5 – Kwa nini sura hii imerudiarudia maneno?

Jawabu:

Wapinzani wa Qur’ani Tukufu wanaposhindwa kupata kosa ndani ya Kitabu hicho Kitakatifu hukimbilia kwenye vitu kama hivi. Wanaojaribu kuikosoa Qur’ani wanadai kuwa, kurudiarudia maneno si katika ufasaha wala balagha ya lugha. Hata hivyo wanakosoa tu ili na wao waambiwe kuwa wamekosoa hata kama ukosoaji wao hauna maana. Kila mtu anajua kwamba si mara zote kurudia kitu ni kinyume cha ufasaha na balagha ya lugha. Mara nyingine kurudia kitu ni jambo la dharura na la lazima kabisa. Ndio maana utaona hata katika maisha yetu ya kawaida, chombo fulani cha habari kinarudia kutangaza habari moja kwa lugha tofauti kutwa nzima au siku kadhaa na kwa tofauti ndogo tu, ili kufanya habari hiyo ijikite vizuri kwenye akili za walengwa. Tunaona pia jinsi matangazo ya biashara yanavyorudiwarudiwa kila mara na kila siku na wala wakosoaji hao hawasemi, jambo hilo halifai. Hivyo kurudia kitu ni jambo la dharura baadhi ya wakati.

Sasa tuangalie wanachuoni wa Tafsiri za Qur’ani wanasemaje kuhusu hikma ya kurudiwa maneno katika Surat al Kafirun.

(i) Kundi moja linasema, sababu ya kurudiwa huko ni kuwakatisha tamaa kikamilifu makafiri na kuwasisitizia kuwa, msimamo huo wa Mtume na Waislamu hautetereki kabisa. Ni kutangaza hadharani kwamba njia ya Mtume na Waislamu ni tofauti kabisa na ya washirikina na hakuna sehemu yoyote wanapoweza kukutana Waislamu na washirikina katika itikadi ya Mwenyezi Mungu na anayestahiki kuabudiwa kwa haki.

Wakati wa ukhalifa wa Harun al Rashid, kulikuwa na mijadala mingi kuhusu itikadi za Mwenyezi Mungu Mmoja na kuhusu Uislamu kiujumla. Kipindi hicho kilikuwa na wanafiki wengi pia ambao wakijidhihirisha kwa sura ya Waislamu kwa lengo la kuupiga jambia kwa nyuma Uislamu. Mmoja wao aliitwa Abu Shakir Deisani (?). Siku moja alitoa hoja kwamba mbona katika Surat al Kafirun kumerudiwarudiwa maneno. Alidai hiyo inathibitisha kuwa Qur’ani si fasaha na wala haina balagha. Majibu aliyopewa na mwanachuoni mmoja mkubwa aliyeitwa Abu Jaafar al Ahwal (?) ni kwamba, Makuraish wa Makka walipojadiliana na Mtume, walimwambia mwaka wa kwanza Mtume aabudu miungu yao, mwaka wa pili wao waabudu Mungu Mmoja, mwaka wa tatu Mtume aabudu tena miungu yao na mwaka wa nne wao waabudu Mungu Mmoja ndio maana majibu yamekuja na kurudiwa mara nne ili kukanusha pendekezo moja baada ya jingine.

(ii) Wafasiri wengine wanasema, aya hizo zimerudiwa kwa kuzingatia nyakati zake. Ukanushaji wa kwanza ulihusu wakati uliopo yaani wakati ule Mtume alipokuwa anasoma aya hizo na ukanushaji wa pili unahusu siku za usoni. Kwa maana ya kwamba, hivi sasa siabudu na katika siku za usoni pia kamwe sitoabudu.

(iii) Tafsiri nyingine iliyotolewa kuhusu sababu za kurudiwa maneno katika Surat al Kafirun ni kwamba ukanushaji wa kwanza unataja tofauti baina ya waabudiwa, ukanushaji wa pili unahusu tofauti ya ibada yaani siabudu mnavyoviabudu na wala nyinyi hamumwabudu ninayemuabudu mimi. Ibada yangu ni ya ikhlasi na haina chembe ya shirki lakini ibada yenu ya masanamu haina ikhlasi yoyote, mnafuata kibubusa mliyowakuta nayo mababu zenu na hamuwezi kusema kuwa mnayaabudu masanamu hayo ili kuyashukuru kwani hayajakufanyieni jema lolote wakati ibada yangu mimi ya Mungu Mmoja ni ya kumshukuru kwa dhati Muumba wangu aliyenipa neema nisizoweza kuzihesabu.

6 – Tuje kwenye aya ya mwisho ya “Nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu.”

Baadhi ya wakati mtu anaweza kudhani kuwa, aya hiyo inaruhusu na inaridhia watu wawe na dini nyinginezo si Uislamu. Imenukuliwa maadui wa Uislamu walikuwa wanasema, Mtume wenu Waislamu amesema wazi kuwa, nyinyi mna dini yenu na mimi nina dini yangu, ya nini ugomvi na ya nini kutushikilia lazima tuwe Waislamu? Wakisema, Qur’ani yenu yenyewe inasema kuwa sisi tuna dini yetu na nyinyi mna dini yenu?

Hata hivyo hoja yao hiyo ni dhaifu sana. Wakati Qur’ani imeshasema kuwa “Anayetafuta dini isiyo Uislamu haitokubaliwa kwake,” haiwezi tena kusema kuwa kila mtu yuko huru kufuata dini anayotaka au madai ya baadhi ya makafiri kwamba dini yoyote ni sawa tu alimradi uwe mwanadamu mwema. Yote hayo si sawa. Bali maana ya aya hii ya 6 ya sura ya 109 ya al Kafirun inafanana na ile aya ya 55 ya Sura ya 28 ya al Qasas ambayo inasema: “Na (waumini) wanaposikia upuuzi hujitenga nao na husema: Sisi tuna vitendo vyetu, na nyinyi mna vitendo vyenu. Amani juu yenu! Sisi hatutaki kujibizana na wajinga.”

Hapa katika aya hii ya sita ya Surat al Kafirun ni vivyo hivyo. Mwenyezi Mungu amemuamrisha Mtume Wake awaambie makafiri wote kwamba, hiyo dini mnayoifuata haina thamani yoyote kwangu na kwetu Waislamu, ni yenu wenyewe na adhabu ya matendo yenu maovu mtaipata wenyewe haituhusu sisi, kwani dini yetu sisi ya kumwabudu Mungu Mmoja, Muumba wa kila kitu, ni tofauti kikamilifu na dini yenu ya miungu mingine isiyokuwa Allah.


Kumetolewa pia majibu mengine kuhusu aya hiyo. Miongoni mwake ni lile linalosema: Katika tafsiri kuna maneno yamefichwa hapo yaani tafsiri ya aya hiyo iwe hivi: Nyinyi mna malipo ya dini yenu na mimi nina malipo ya dini yangu. Au: Malipo ya dini yenu yatakurejeeni wenyewe na malipo ya dini yangu yatanijia mwenyewe.

Majibu mengine ni kulifasiri hilo neno dini lenyewe kwa maana ya malipo. Yaani maana ya aya hiyo iwe hivi: Nyinyi mna malipo yenu na mimi nina malipo yangu.

7 – Tumalizie kwa kuangalia uhusiano wa sura hii na maisha ya tangu Nabii Adam hadi siku ya Kiama.

Kiufupi ni kwamba sura hii inadhihirisha uhakika kuwa hakuna mapatano ya aina yoyote ile hata ya sekunde moja baina ya shirk na ibada ya Mungu Mmoja. Hilo limekuwepo kwa Mitume wote tangu Nabii Adam AS hadi Mtume wa Mwisho, Muhammad al Mustafa SAW na mpaka Siku ya Kiama. Hivi ni vita vya haki na batili na siku zote haki haijawahi kushindwa na batili kwa maana halisi. Haki ni kama maji ya mvua, yanaweza baadhi ya wakati yakafunikwa na povu la maji hayo wakati yanatiririka, lakini haina maana maji hayapo. Haki ni vivyo hivyo inaweza baadhi ya wakati ikafunikwa na povu la batili, lakini haina maana haki imeondoka na hakuna mapatano wala suluhu baina ya haki na batili na baina ya kheri na shari kwa maana ya wema na uovu. Qur’ani Tukufu inasema: “Basi anayetenda chembe ya wema, atauona! Na anaye tenda chembe ya uovu atauona!” Hapo hapana kitu cha tatu yaani mchanganyiko wa wema na uovu kwani wema na uovu ni vitu viwili visivyokutana wala kupatana kabisa. Na hii ndiyo maana halisi ya “Siabudu mnachoabudu na wala nyinyi hamumwabudu ninayemwabudu.”

Suala hilo linahusu zama zote na mahala popote. Hivi ndivyo walivyoishi mawalii wa Mwenyezi Mungu tangu kuumbwa Nabii Adam AS na baada yake na ndivyo tunavyopaswa kuishi Waislamu leo hii, kutochanganya tauhidi na shirk, kutochanganya wema na uovu, kutochanganya kheri na shari.

Tunamuomba Allah atuepushe na aina zote za shirk. Azifanye imara imani zetu tusitetereke ndani ya tauhidi na ibada ya Mungu Mmoja. Atuweke mbali na wanaochanganya wema na uovu kwa kutarajia kupata radhi za Mola Muumba. Tunamuomba Allah atupe mwisho mwema anaouridhia. Aamin.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Ndugu yenu, Ahmed Rashid.

(Visited 91 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!