Wakuu wa kundi la Taliban nchini Afghanistan wametangaza kuwa, kwa mara ya kwanza tangu walipochukua madaraka ya nchi hiyo, wameruhusu wanafunzi wa kike washiriki katika masomo ya vyuo vikuu vya serikali.

Shirika la habari la “Rusia al Yaum” limeripoti habari hiyo na kuwanukuu viongozi wa Taliban wakisema kuwa, kuanzia Jumatano, Februari 2, 2022, majimbo sita ya nchi hiyo yameruhusu wanafunzi wa kike warejee masomoni katika vyuo vikuu vya serikali. Majimbo hayo ni Laghman, Nangarhar, Kandahar, Nimruz, Helmand na Farah. 

Viongozi wa serikali ya Taliban huko Afghanistan wametoa ufafanuzi zaidi kwa kusema, idadi ndogo ya wanafunzi wa kike wataruhusiwa kushiriki katika masomo bila ya kuchanganyika na wanaume. 

Ikumbukwe kuwa, suala la haki za wanawake hususan katika masuala ya elimu ni miongoni mwa maudhui kuu zenye mvutano baina ya serikali ya Taliban na jamii ya kimataifa.

Licha ya shule nyingi za msingi kufunguliwa, lakini idadi kubwa ya skuli za Elimu ya Kati na vyuo vikuu vya serikali bado haviruhusu wanawake kushiriki katika masomo nchini humo.

Taliban walirejea madarakani mwezi Agosti 2021 baada ya wanajeshi wa Marekani kuondoka ghafla nchini Afghanistan.

Inatabiriwa kuwa, vyuo vikuu vya mikoa mingine ya Afghanistan navyo vitakuwa vimeruhusu wanafunzi wa kike kuendelea na masomo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Februari.

(Visited 13 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!