Bismillahir Rahmanir Rahim.

يَا أَيُّهَا النَّاسُ قَدْ جَاءَتْكُم مَّوْعِظَةٌ مِّن رَّبِّكُمْ وَشِفَاء لِّمَا فِي الصُّدُورِ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ  قُلْ بِفَضْلِ اللَّهِ وَبِرَحْمَتِهِ فَبِذَلِكَ فَلْيَفْرَحُواْ هُوَ خَيْرٌ مِّمَّا يَجْمَعُونَ

(57) Enyi watu! Yamekujieni mawaidha kutoka kwa Mola wenu Mlezi, na poza kuponyesha yaliyomo vifuani, na uwongofu, na rehema kwa Waumini. (58) Sema: Kwa fadhila ya Mwenyezi Mungu na rehema yake! Basi nawafurahi kwa hayo. Haya ni bora kuliko hayo wanayoyakusanya.

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Kuna mjadala mpana kuhusu aya za 57 na 58 za Sura ya 10 ya Yunus kuhusiana na swali kwamba, kati ya moyo na roho, hisia zinakuweko wapi?

Ni wazi kwamba moyo ni kiungo kinachosukuma damu mwilini. Hiyo ndiyo kazi yake. Lakini mbona Qur’ani inasema katika nyoyo kuna maradhi ya nafsi? Kwa nini isiseme katika roho ndio kuna maradhi?

Umetolewa ufafanuzi wa kutosha kuhusu hikma ya kutumiwa moyo badala ya roho katika suala hilo na ni hoja zinazokwendana na maumbile ya mwanadamu na uhalisia wake.

Lakini kwa vile tangu mchana nilikuwa nasaka fursa ya kupata kuzungumza machache kuhusu hii aya ya 58 ya sura ya Yunus tena angalau kuhusu tofauti tu baina ya maneno fadhila na rehema yaliyotumika kwenye aya hiyo na sijapata hiyo fursa, ni vyema hapa nidonyoe kiduchu hapa tofauti baina ya maneno hayo mawili na huo mjadala kuhusu moyo na roho tuuache kama ulivyo kwanza.

TOFAUTI BAINA YA FADHILA NA REHEMA

1- Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani wamesema kuwa, fadhila ni neema za dhahiri na rehema ni neema za batini.  Yaani fadhila ni neema za kimaada za kushikika na rehema ni neema za kiroho zisizoshikika. Hoja yao ni kwamba mara nyingi aya za Qur’ani utaona zinasema tafuteni fadhila za Allah yaani riziki za Allah.

2- Wafasiri wengine wa Qur’ani wanasema: Fadhila za Allah katika aya ya 58 ya surat Yunus, maana y ake ni mwanzo wa neema na neno rehema ndani ya aya hiyo ni muendelezo wa neema hizo za Allah. Wenye mtazamo huo wanasema, fadhila za Allah hapa ni Mtume mwenyewe, na rehema ni yale mafundisho yake ambayo yamekuja kuendeleza Utume wake. Hao wamenukuu baadhi ya hadithi kuthibitisha hoja yao hiyo.

3- Wengine wanasema, fadhila na rehema hapo ni Qur’ani yenyewe maana aya ya kabla yake imezungumzia Qur’ani.

4- Mabingwa wengine wa tafsiri wamesema, fadhila hapo maana yake ni neema za Akhera na rehema ni kusamehewa madhambi na neema hizo zinawahusu waumini tu.

5- Wengine wamesema huenda maana ya fadhila hapo ni neema zote tu za Mwenyezi Mungu zinazowafikia viumbe Wake wote hata wasio waumini na hata wasio wanadamu lakini rehema ni neema maalumu za Allah zinazowahusu waumini tu. Hoja yao ni aya ya kabla ya hii tunayoijadili hapa yaani aya ya 57 ya Surat Yunus ambayo kama tulivyosema, rehema zake zinawahusu waumini tu. Hawa wamekwenda kwenye ule mjadala wetu wa leo mchana wa kuifananisha aya ya 57 ya Surat Yunus na Bismillahir Rahmanir Rahim.

6- Wengine wamesema, fadhila za Allah katika aya hii ya 58 ya sura ya 10 ya Yunus ni imani na neno rehema hapo ni Qur’ani.

Kiujumla ukiangalia kwa kina utaona mitazamo yote hiyo mtu unaweza ukaijumuisha pamoja na kusema yote kwa pamoja ndizo maana za maneno mawili ya fadhila na rehema yaliyokuja kwenye aya hii ya 58 ya Surat Yunus. Hakuna mgongano baina yao.

Naam, aya hii inahusiana moja kwa moja pia na uwepo wa Bwana Mtume Muhammad SAW na risala yake. Ni wajibu wetu tumshukuru Allah muda wote kwa kutuletea rehema kubwa ya viumbe wote, yaani Bwana Mtume Muhammad SAW.

Naam aya ya 107 ya Surat al Anbiyaa imebainisha wazi kwamba Mtume Muhammad hakutumwa na Allah ila awe rehema kwa viumbe wote. Hii aya ya 107 ya Surat al Ambiyaa inahitajia muda wake maalumu wa kuichambua. Ona sigha yake iliyokuja sawa kabisa na ya kalimatut tawhid yaani “Laa ilaha illa Llaah.”

Imepokewa hadithi kwamba wakati iliposhuka aya hiyo ya 107 ya Surat al Ambiyaa, Mtume SAW alimuuliza Malaika Jibril AS, je, rehema hizi na wewe umo ndani yake? Jibril alijibu kwa kusema: Mimi nami nilikuwa sijui hatima yangu mbele ya Allah, lakini iliposhuka aya hii, nimepata yakini kwamba nitakuwa miongoni mwa rehema zisizo na ukomo. Jibril akaendelea kusema, anamshukuru Allah kwa kumpa sifa maalumu. Halafu alisoma aya ya 20 ya Surat al Takwir ambayo maana yake kwa Kiswahili inasema: Mwenye nguvu na mwenye cheo kwa huyo Mwenye Kiti cha Enzi. Namuomba Allah atupe taufiki ya kuja kuichambua kwa kituo aya hiyo ya 107 ya Surat al Ambiyaa.

Ukizingatia yote hayo ndugu yangu Muislamu utaona kuwa ni haki ya kila muumini kufurahi kwa neema kubwa ya Qur’ani, kwa kutumwa Mtume Muhammad na kwa kuteuliwa na Uislamu kuwa dini yetu.

Kufurahi kwa kushikamana vilivyo na Uislamu ndiyo njia bora na ya kimsingi, lakini kukaa Waislamu wakafundishana na kukumbusha na kusomeshana na kuzitia furaha nyoyo za Waislamu na kuwalea watoto wao katika malezi ya kufurahia na kuadhimisha neema hizo, ni jambo muhimu pia kwa kila muumini.

Kwa leo tutosheke na hayo.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Mwanafunzi wenu,

Ahmed Rashid.

(Visited 72 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!