Sisi tunakusimulia khabari zao kwa haki. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.

QUR’ANI TUKUFU 

Aya ya Leo…

Al-Kahfi 18:13

(نَّحۡنُ نَقُصُّ عَلَیۡكَ نَبَأَهُم *بِٱلۡحَقِّۚ* إِنَّهُمۡ فِتۡیَةٌ ءَامَنُوا۟ بِرَبِّهِمۡ وَزِدۡنَـٰهُمۡ هُدࣰى)

Sisi tunakusimulia khabari zao kwa haki. Hakika wao walikuwa ni vijana walio muamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uwongofu.

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum. 

Tumo katika siku nyingine tukufu ya Ijumaa ambayo imehimizwa sana kusoma Surat Al Kahf ndani yake. Leo napenda kugusia nukta nyingine katika kisa cha Watu wa Pango kama kilivyosimuliwa na sura hii tukufu.

Inakadiriwa kuwa, tukio la Aswhabul Kahf lilitokea mwaka 250 baada ya kuondoka duniani Nabii Isa AS. Ukilinganisha na mwaka 570 ambao ndio ulioripotiwa kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW utaona kuwa tukio hilo la Watu wa Pango lilitokea miaka 321 kabla ya kuzaliwa Mtume SAW. Surat Al Kahf nayo ambayo aya zake zote ni 110 na iko baina ya juzuu za 15 na 16 za Qur’ani Tukufu, ilikuwa ni sura ya 69 kuteremshiwa Bwana Mtume akiwa mjini Makkah kabla ya kuhamia Madina yaani katika kile kipindi cha miaka 10 ya tangu kupewa Utume Bwana wetu Muhammad SAW.

Surat Al Kahf ilishuka baada ya Surat al Nahl na kabla ya sura ya Al Ghaashiyah.  

Ninayasema haya kwa lengo maalumu. Kuna nukta muhimu za kimiujiza nataka kuzigusia hapa.

Katika aya hiyo ya 13 ya hii sura tukufu, niliyoinukuu hapo juu, Allah anasema: Hakika sisi tunakusimulia habari yao *kwa haki.*

Kwanza huku ni kujiamini kiasi gani ambako hakuna kiumbe yeyote mwenye uthubutu wa kukwambia hiki ninachokueleza hivi sasa ni sawasawa mia kwa mia, nukta kwa nukta ya tukio ninalokusimulia. Mtu hathubutu kusema hivyo kwani akili yake haina uwezo wa kurekodi na kudhibiti kiundani kila kitu kilichotokea, lazima ataongeza lake au atapunguza na wakiwepo wawili na zaidi ndio kabisa. Ndio maana utotoni tulikuwa tunaambiwa kila kisa na hadithi kina ncha saba. Hayo ni kuhusu matukio ya karibuni na mahala pa karibu na pamoja na hayo hakuna mwandishi anayethubutu kusema hiki ninachokiandika hapa, naapa kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vile vile ilivyotokea kwa asilimia mia moja. Ndio maana pia utaona baadhi ya wanachuoni wanasema, Mtume “amenukuliwa” akisema, hawakwambii tu moja kwa moja kwamba Mtume alisema hivi hasa.

Sasa tukio la Watu wa Pango lilitokea zaidi ya miaka 361 kabla ya kupewa Utume kipenzi chetu na ruwaza yetu njema, Muhammad al Mustafa SAW, lakini aya inasema kwa kujiamini kabisa kwamba hiki kinachoelezwa hapa ndicho chenyewe hasa kilichotokea, mia kwa mia.  Ni challenge kwa kila mtu ajitokeze aseme hapana haikuwa hivyo, ilikuwa hivi. Ni kujiamini kiasi gani huku tunakofundishwa na Kitabu chetu kitakatifu! Kuweza Bwana Mtume kuhadithia namna hii, baada ya karne zote hizo za tukio, wenyewe ni muujiza. Ndio maana Mfalme Najashi wa Habasha aliposomewa aya za Surat Maryam na swahaba Jaafar Tayyar, hakusita kuamini maana mwenye akili lazima atajiuliza, kijana aliyekulia jangwani, katika jamii ya watu wasiojua kusoma na kuandika, anaweza vipi kusimulia kwa umahiri wa hali ya juu kama vile matukio yaliyotokea miaka mingi kabla ya kuzaliwa kwake tena katika maeneo ya mbali. Lazima kuna nguvu ya Allah, Mjuzi wa kila kitu. Niseme pia kuwa, mapokezi ya historia yanataja maeneo matatu makuu lilipotokea tukio hilo la Aswhabul Kahf, yaani katika mji wa Ephesus ambao leo unajulikana kwa jina la Selçuk nchini Uturuki. Pili katika eneo lililoko karibu na Amman, mji mkuu wa Jordan na tatu Damascus, mji mkuu wa Syria. Maeneo yote hayo yako mbali na Makkah. Kila mmoja anatoa ushahidi na nadharia yake kujaribu kuthibitisha eneo lake ndipo lilipotokea tukio hilo. Hii ni kuzidi kuthibitisha kuwa ni muujiza mkubwa kuweza Qur’ani kusimulia kwa haki kisa hicho vile vile ilivyojiri mia kwa mia.

Nukta nyingine ya kimiujiza kuhusu hicho kipande cha aya ya 13 ya Surat Al Kahf, ni kwamba Allah ametumia maneno ya tunakusimulia kwa haki. Hakusema tunakusimulia kwa yakini au kwa usahihi au au au, bali ameteua neno haki.

 Uteuzi huu wa maneno sahihi na mahala pake, ni muujiza mwingine katika visa vya Qur’ani Tukufu kikiwemo hiki cha Aswhabul Kahf. Hiki ni kisa cha haki, hamna khurafa, hamna upuuzi, hamna upotoshaji, hamna laghw, bali ni uongofu tu ndio uliojaa kwenye kisa hiki na vinginevyo vya Qur’ani Tukufu na kila harf unayosoma ya Kitabu hiki kitakaifu unaandikiwa thawabu na inakuongoza kwenye njia sahihi. Kuweza kuteua neno sahihi kabisa na mahala panapofaa zaidi kuliko neno jingine lolote, si kazi ya mwanadamu, bali ni kazi ya Mjuzi Alimu Ambaye ilmu Yake imekienea kila kitu hata kabla ya kutukia kwake.

Nukta nyingine ya kimiujiza kuhusu hilo neno Haki ni kwamba, Qur’ani ni Kitabu cha uongofu, si kitabu cha riwaya wala si kitabu cha ngano na hadithi simulizi wala si Kitabu cha utabiri wa nyota. Lakini pia tunaona ndani yake mumejaa visa na simulizi za matukio ya kila namna. Sasa muujiza uko wapi hapo? Muujiza umo katika huku kusimulia kwa haki. Muujiza uko katika umahiri wa hali ya juu wa Qur’ani Tukufu wa kuchunga sifa yake ya kuwa Kitabu cha uongofu. Inakuhadithia kisa, inakusimulia matukio ya kale, inakutabiria yatakayotokea baadaye, lakini imechunga kikamilifu sifa yake ya kuwa kitabu cha uongofu na kisicho na chembe ya upuuzi ndani yake. Huu ni muujiza, hasa kwa kuzingatia kuwa Qur’ani imeshushwa katika kipindi cha miaka 23 lakini kila aya imekamilika kikamilifu na huoni udhaifu wala unyong’onyevu wala migongano katika simulizi zake, katika maelezo yake, katika maamrisho na makatazo yake na katika chochote kile. Huu kwa kweli ni muujiza mwingine ambao licha ya Qur’ani na Uislamu kuwa na maadui wakubwa kupindukia kwa karne nyingi, lakini wameshindwa na watashindwa kuzima nuru yake.

Nimeandika hayo kwa kunukuu hapa na pale. Mapungufu yote yaliyomo yanatokana na udhaifu na uchache wangu wa maarifa.

Mwanafunzi wenu, Ahmed Rashid.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

(Visited 19 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!