Mratibu wa misaada ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa huko Palestina ametaka kuongezwa misaada ya kibinadamu kwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza. Licha ya Israel kulazimika kusimamisha vita vya hivi karibuni, lakini hadi hivi sasa inaendelea kukwepa kutekeleza ahadi zake na hairuhusu kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa Wapalestina.

Hayo yameripotiwa na televisheni ya al Jazeera ya Qatar ambayo imemnukuu Bi Lynn Hastings akisema hayo Jumatano na kuitaka jamii ya kimataifa na taasisi za kimataifa kuongeza misaada yao kwa wakazi wa Ukanda wa Ghaza.

Ombi hilo la Umoja wa Mataifa limetolewa katika hali ambayo bado Israel inakaidi kutekeleza ahadi zake za kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia Wapalestina.

Televisheni ya al Jazeera imeripoti pia kuwa, ukaidi unaooneshwa na Israel una uhusiano wa moja kwa moja na mazungumzo baina ya makundi ya Palestina na Israel ambayo si ya moja kwa moja bali yanafanyika kwa upatanishi wa Misri.

Bi Lynn Hastings ameongeza kuwa, hali katika Ukanda wa Ghaza haijarejea kama ilivyokuwa kabla ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel. Sababu yake amesema ni kwamba kivuko cha Karam Abu Salem cha kusini mwa Ghaza hakina uwezo wa kupitisha zaidi ya asilimia 50 ya mahitaji ya ukanda huo.

Amesema pia kuwa, kivuko cha Beit Hanoun nacho kinafanya kazi kwa nadra na kwa kiwango cha chini sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!