Mpya Kabisa

Video: Historia fupi ya Sheikh Muhammad Siddiq al Minshawi

Sheikh Muhammad Siddiq al Minshawi mmoja wa maqarii bingwa wa Qur’ani Tukufu alizaliwa tarehe 20 Januari, 1920 katika mji wa al Minshah katika mkoa wa Sohag wa kusini mwa Misri. Baba yake Sayyid Siddiq al Minshawi na kaka yake Mahmoud Siddiq al Minshawi walikuwa wasomaji wakubwa wa tajwidi kama yeye Ustadh Muhammad.

Kutokana na mdundo wa aina yake ndani ya sauti ya Sheikh Muhammad Siddiq al Minshawi, alipata umaarufu wa qarii mwenye koo la sauti ya huzuni au sauti ya kuliza.

Ustadh Muhammad Siddiq al Minshawi alipata taufiki ya kuhifadhi Qur’ani nzima akiwa bado na miaka minane. Alipotimia miaka 9 alikuwa tayari anaandamana na baba yake kusoma tajwidi katika vikao mbalimbali mkoani Sohag. Usomaji wake ulimpa umashuhuri mkubwa akiwa bado mtoto mdogo. Umashuhuri wake uliwafikia viongozi wa Radio Cairo ambao walimtaka aende kwenye kituo cha redio hiyo akasome mbele ya majaji wa qiraa ili wakimpasisha, basi apewe fursa ya kurushiwa redioni qiraa zake.

Ustadh Muhammad Siddiq al Minshawi alipata taufiki ya kuhifadhi Qur’ani nzima akiwa bado na miaka minane.

Hata hivyo alihisi hiyo ilikuwa ni kumpunguzia heshima hivyo alikataa ombi hilo. Chema chajiuza, hivyo na kwa mara ya kwanza katika historia ya Radio Cairo, timu ya waandishi na wataalamu wa kurekodi enzi hizo, ililazimika kufungasha na vifaa vyao hadi nyumbani kwa Sheikh al Minshawi na kurekodi qiraa zake.

Hayo yalikuwa ni mabadiliko makubwa, kwani baada ya kurushwa hewani qiraa zake redioni, umashuhuri wa Sheikh Muhammad Siddiq al Minshawi uliongezeka si katika kona zote za Misri tu, bali pia katika ulimwengu mzima wa Kiarabu na nje ya nchi za Kiarabu.

Sheikh Minshawi alipata umashuhuri wa kusoma tajwidi kwa sauti ya kuvutia akiwa bado mtoto mdogo. Akiwa na miaka 9.

Alisafiri hadi nchi mbalimbali kusoma Qur’ani kama vile Indonesia, Jordan, Libya, Kuwait, Palestina ambapo alisoma katika Msikiti wa al Aqsa, Hijaz yaani Saudia, Syria, Iraq, Pakistan, Morocco na Sudan. Nchini Indonesia alikwenda mwaka 1955 akiwa pamoja na Sheikh Abdul Basit Abdul Samad akiwa na umri wa miaka 35. Mwaka 1966 alielekea Baghdad, mji mkuu wa Iraq, ambapo safari yake nchini Libya ilikuwa mwaka 1969 akiwa pamoja na Sheikh Mahmoud Khalil al Hussary.

Mwaka 1966, Sheikh Muhammad Siddiq al Minshawi alikumbwa na ugonjwa ambao madaktari walimkataza kuendelea kusoma tajwidi. Hata hivyo alikataa pendekezo hilo na aliendelea na qiraa hadi mwisho wa umri wake. Qarii huyo bingwa wa Misri aliendelea kusoma tajwidi hadi alipofariki dunia. Sheikh Minshawi alifariki dunia mjini Cairo tarehe 20 Juni, 1969 akiwa na umri wa miaka 49.

Hapa chini tumeweka kipande cha video cha historia fupi ya qarii huyo bingwa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!