Waislamu wasiopungua 11 wamefariki dunia baada ya kuripuka bomba la gesi la chini ya ardhi karibu na msikiti mmoja nje ya mji mkuu wa Bangladesh, Dhaka.
Shirika la habari la Associated Press limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, mbali na Waislamu hao 11, makumi ya Waislamu wengine wamepata majeraha makubwa ya moto.
Maafisa wa serikali ya Bangladesh wamethibitisha habari hiyo leo Jumamosi na kuongeza kuwa, mripuko huo ulitokea jana Ijumaa usiku wakati Waislamu wakimalizia kusali Sala ya Isha katika msikiti wa Baitus Salat katika eneo la Narayanganj, nje ya Dhaka, mji mkuu wa Bangladesh.
“Hadi leo asubuhi madaktari walikuwa wanatibu mejeruhi 37 waliopata majeraha ya moto katika tukio hilo,” amesema mkuu wa jeshi la polisi la eneo hilo, Zayedul Alam.
Madaktari wanasema asilimia kubwa ya majeruhi wameunguzwa na moto kwa asilimia 90. Wengi wao wako katika hali mahututi, amesema Daktari Samant Lal Sen, mratibu wa hospitali wanapotibiwa Waislamu hao.
Vituo vya televisheni vya Bangladesh vimeripoti kuwa, kwa uchache AC sita zimeripuka ndani ya msikiti huo. Hadi tunapokea habari hii, maafisa wa Zima Moto walikuwa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kujua chanzo cha kuripuka bomba hilo la gesi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!