Makumi ya maelfu ya Wapalestina wameshiriki katika ibada ya Sala ya Ijumaa iliyosaliwa leo katika Kabla cha Kwanza cha Waislamu, Msikiti wa al Aqsa kwenye mji mtakatifu wa Baytul Muqaddas licha ya hatua kali za kiusalama zilizochukuliwa na na Israel ili kuwazuia Waislamu wasifike kwenye Msikiti huo.

Shirika la habari la Palestina WAFA limeripoti kuwa, maelfu ya Waislamu wa Palestina wameshiriki katika ibada ya leo ya Sala ya Ijumaa licha ya wanajeshi wa Israel kuweka vizuizi vingi vizito katika njia za kuelekea kwenye Msikiti wa al Aqsa.

Izam al Khatib, Mkurugenzi wa Idara ya Qakfu wa Kiislamu katika mji wa Quds amesema kuwa, Waislamu 40,000 wameanza kumiminika kwenye Msikiti wa al Aqsa kwa ajili ya kushiriki katika ibada ya leo ya Sala ya Ijumaa tangu mepema sana asubuhi.

Wanajeshi wa Israel wameweka vizuizi na vituo vingi vya upekuzi katika njia zote za kuingilia eneo la kale la mji wa Quds. Wanajeshi hao walikuwa wakichunguza kila kitu na kuwazuia Waislamu wengi wasielekee Msikitini hapo.

Hii ni katika hali ambayo, jana Alkhamisi Msikiti wa al Aqsa ulitoa tangazo ukisema kuwa, karibu walowezi 120 wenye misimamo mikali wa Kizayuni wameuvamia Msikiti wa al Aqsa kwa kutumia mlango wa kusini magharibi mwa Msikiti huo mtakatifu wakisaidiwa kikamilifu na wanajeshi wa Israel. Baada ya kukaa kwenye eneo la Msikiti huo muda waliopenda, kundi hilo la walowezi wa Kizayuni liliondoka likilindwa na jeshi la polisi la Israel.

Siku ya Jumapili pia, walowezi 250 wa Kizayuni waliuvamia Msikiti wa al Aqsa kwa ulinzi kamili wa jeshi la Israel. Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imesema kuwa, uvamizi huo unadhoofisha makubaliano ya kusimamisha vita yaliyofikiwa baina ya Israel na Wapalestina, takriban wiki moja iliyopita, baada ya kumalizika vita vya Ghaza ambavyo Wapalestina wamevipa jina la Upanga wa Quds.

(Visited 119 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!