Kituo cha Kiislamu cha Bolivia katika mji wa Santa Cruz de la Sierra kimeanzisha harakati mpya za kuwasaidia wenye haja katika miji tofauti ya nchi hiyo ikiwa ni kuendeleza moyo wa mapenzi na kutoa waliojifunza kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mtandao wa habari za Kiislamu wa “Alukah” umenukuu taarifa ya Kituo cha Kiislamu cha Bolivia (Centro Islamico Boliviano) ikisema kuwa kituo hicho kimeanza kugawa mahitaji mbalimbali ya lazima kama ya afya na chakula katika eneo la Lindo huko Bolivia.

Aidha kituo hicho cha Kiislamu kwa kushirikiana na timu ya kujitolea ya madaktari na wahudumu wa afya, kimekuwa kikitoa matibabu bure kwa watu maskini na wasiojiweza kwenye eneo hilo.

Kituo hicho kinashirikiana pia na makundi ya watu wanaojitolea kugawa chakula kwa maskini katika baadhi ya vituo vya elimu za wazazi nchini Bolivia. Kampeni hiyo imefikisha misaada ya chakula pia katika mji wa San Lorenzo huko huko Bolivia ikiwa ni njia nzuri ya kuwaonesha wananchi wa nchi hiyo, utukufu na ubora wa dini ya Kiislamu.

Hata baada ya kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani, Kituo cha Kiislamu cha Bolivia kinaendelea kugawa chakula kwa wahitaji wa maeneo tofauti ya nchi hiiyo ya Amerika ya Latini pamoja na huduma nyingine kwa wahitaji kama ilivyokuwa wakati wa Ramadhani.

Bolivia ni nchi ndogo ya kusini mwa Bara la Amerika. Idadi ya watu wake ni karibu milioni 12. Dini kuu ya nchi hiyo ni Ukristo. Idadi ya Waislamu nchini humo ni ndogo sana ni takriban watu 2000 tu, lakini pamoja na hayo wamejipanga vizuri kiasi kwamba wanaweza kutoa misaada ya kila namna kwa wahitaji hata baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!