Kutokana na kuenea vibaya ugonjwa wa corona na kuongezeka umaskini na ukosefu wa ajira, Waislamu wengi nchini India wameamua fedha zao za kwendea Hija wazitumie katika masuala ya kutoa misaada kwa wenye haja na hasa wagonjwa na waathiriwa wa COVID-19.

Kwa mujibu wa gazeti la The Times of India, ugonjwa wa corona umepelekea Waislamu wengi nchini India wapoteze ajira na kazi zao kama ilivyo kwa wananchi wengine wa nchi hiyo. Ni kwa sababu hiyo ndio maana bibi mmoja na mumewe wakazi wa jimbo la Maharashtra wameamua fedha walizokuwa wamezitenga kwa ajili ya safari ya HIja wazitumie kuwasaidia wenye haja na watu waliopoteza kazi na ajira zao kutokana na janga la COVID-19.

Shaikh Anjum Pervez na mkewe Bi Samina wamekuwa wakitumia fedha wanazokusanya kwa ajili ya Hija, kutoa msaada kwa wenye haja na huo ni mfano mmoja tu wa maadili mema ya Waislamu wa India katika kipindi hiki kigumu cha ugonjwa wa corona.

Shaikh Anjum Pervez ameliambia gazeti la Thie Times of India kwamba, katika wimbi la kwanza la corona, walitumia fedha zao zote za Hija kusaidia wenye haja. Katika wimbi la pili la ugonjwa huo, Waislamu hao walitumia fedha zao za Hija kulipia wagonjwa mahospitalini, kununua vifaa vya matibabu pamoja na mitungi ya oksijeni kwa anili ya watu maskini. 

Waislamu hao walikuwa wanakwenda kuhiji Makka katika kila msimu wa Hija tangu mwaka 2008. Hata hivyo kutokana na zuio la kusafiri na kutekeleza ibada ya Hija kutokana na janga la corona, kwa miaka miwili sasa Waislamu hao wanatumia fedha zao za Hija kusaidia wenye mahitaji katika mambo ya kheri na ya kibinadamu.

Waislamu wengi wa India wamekuwa wakifanya hivyo kwa miaka miwili sasa. Wamekuwa wakitumia fedha zao za Hija na Umra kwa ajili ya kusaidia wagonjwa na watu maskini. 

Gazeti la The Times of India limemnukuu Muislamu mwingine anayeitwa Iqbal ambaye kila mwaka katika mwezi wa Ramadhani yeye na mkewe walikuwa wanakwenda kufanya ibada ya Umra akisema kukwa, hivi sasa nao wameamua kutumia fedha zao kuwasaidia maskini na walioathiriwa na janga la corona. 

Bw. Iqbal ambaye ni mfanyabiashara anasema, hata hali itakaporejea kuwa ya kawaida baada ya janga la corona, yeye na mkewe wametia nia ya kutumia fadha zao za Umra kwa ajili ya watu maskini na wenye mahitaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!