Mpya Kabisa

Waislamu Nigeria wataka ubaguzi dhidi ya wanawake ukomeshwe

Wanawake Waislamu nchini Nigeria wamewataka viongozi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika watoe adhabu kali kwa kila anayewanyanyapaa na kuwadhalilisha wanawake wanaovaa nguo za staha ya mwanamke wa Kiislamu, Hijab hasa katika taasisi za idara za serikali, mashuleni, benki n.k.

Mtandao wa habari wa The Nation wa nchini Nigeria umewanukuu wanawake Waislamu wa nchi hiyo wakimtaka Rais Muhammadu Buhari na wakuu wa mikoa kuweka sheria za kumuadhibu kila anayewanyanyasa na kuwanyanyapaa wanawake wanaovaa Hijab.

Taasisi kadhaa za Kiislamu zimeshiriki katika komgamano la mjini Lagos kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Hijab na zimetumia fursa hiyo kulaani ubaguzi wanaofanyiwa wanawake hasa wanaojisitiri kwa vazi la staha la Hijab.

Waislamu wamesema asasi za kiserikali ikiwemo Kamati ya Kusimamia Utambulisho wa Kitaifa (NIMC), mashule na pia baadhi ya mashirika binafsi yanawabagua wanawake Waislamu wanaovaa Hijab.

Hajia (Hajjat) Mutiat Orolu-Balogun aliyeanzisha kampeni na taasisi ya kulinda na kutetea haki za wanawake wanaovaa Hijab (HRAI) amewakilisha taasisi za kulinda haki za Waislamu wanawake katika mazungumzo na waandishi wa habari na amesema, tunaitaka serikali ya Nigeria itoe dhamana ya kupewa adhabu kila mtu ambaye hatochunga haki za wanawake, bila ya kubagua baina ya Waislamu na wasio Waislamu, wanaovaa Hijab na wasiovaa Hijab.

Amesema wana ushahidi wa kutosha unaoonesha jinsi Waislamu wanaovaa Hijab wanavyonyimwa haki zao nchini Nigeria kama vile kujiandikisha katika sehemu mbalimbali na katika utoaji wa ajira kwenye taasisi za serikali, bali hata katika kufaidika na huduma za Benki zinazomilikiwa na makanisa. Amesema kwa masikitiko kwamba, mabinti wa Kiislamu nchini Nigeria wamefikia hata kulazimishwa kuvua Hijab zao kwa ajili ya kupigwa picha za kadi za benki. Amesema, Katiba ya Nigeria imebainisha wazi haki hizo za Waislamu, lakini tatizo ni utekelezaji. Amemtaka Rais Buhari, wakuu wa mikoa, Bunge, mabaraza ya majimbo, Idara ya Mahakama na maafisa wote husika, kuheshimu Katiba na kuhakikisha kuwa wanawake hasa Waislamu hawanyimwi haki zao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!