Wakuu wa Misikiti kadhaa nchini Ufaransa wamelalamikia vikali uamuzi wa hivi karibuni wa wizara ya kilimo ya nchi hiyo wa kupiga marufuku uchinjaji wa kuku Kiislamu.

Wakuu wa Misikiti ya miji mikubwa ya Ufaransa kama ya Paris na Lyon wamewasilisha rasmi malalamiko na upinzani wao dhidi ya uamuzi wa Wizara ya Chakula na Kilimo ya nchi hiyo ya Ulaya wa kupiga marufuku uchinjaji wa kuku kwa njia halali na Kiislamu.

Wakuu hao wa Misikiti wamewaambia wakuu wa Ufaransa kwamba ni haramu kwa Waislamu kula vibudu na kwamba marufuku iliyotangazwa na wizara hiyo na ambayo imepangwa kuanza kutekelezwa mwezi Julai mwaka huu wa 2021 inakinzana na msingi wa kufanyika vichinjo kwa mujibu wa mafundisho matukufu ya Kiislamu.

Moja ya maduka ya kuuza nyama ya halali nchini Ufaransa

Sehemu moja ya tamko la wakuu hao wa Misikiti nchini Ufaransa imesema: “Kupiga marufuku kuchinja wanyama kwa njia halali halali kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu tena wakati huu wa kukaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani, kunatoa ujumbe hasi kwa Waislamu. Wakuu wa misikiti mikubwa ya Ufaransa wanatangaza kusikitishwa kwao na kupinga kwao uamuzi huo wa wizara ya ya kilimo na chakula. Wamesema, tulipowasilisha malalamiko yetu, maafisa husika hawakutupa majibu ya kuridhisha.”

Tamko hilo la wakuu wa Misikiti ya Ufaransa limemalizia kwa kusema: “Hatua kama hizi zina mwisho mbaya na hatari. Zinakwamisha uhuru wa kidini na watu kufuata itikadi na imani zao.”

Wakuu hao wa Misikiti walikusanyika wiki hii katika Msikiti Mkuu wa Paris na wamekubaliana kuendelea kupinga jambo hilo kwa nguvu zao zote na kutoa mwamko na elimu kwa umma kuhusu madhara ya uamuzi huo kwa nchi nzima ya Ufaransa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!