Licha ya kuwa Waislamu nchini Thailand ni jamii ya wachache ikilinganishwa na Mabudha, lakini Waislamu hao wameonesha uwezo mkubwa wa kupata watengenezaji wa vyakula vya halali na vinywaji.

Kwa mujibu wa “ASEAN Briefing,” Waislamu ni jamii ya wachache nchini Thailand ikilinganishwa na Mabudha. Waislamu wanaunda kati ya asilimia 8 hadi 12 ya wakazi milioni 70 wa Thailand.

Waislamu wengi wanaishi katika majimbo ya kusini mwa Thailand, ambayo ni Sutton, Yala, Pattani na Narathiwat. Pia kuna idadi kubwa ya Waislamu eneo la Bangkok. Waislamu wanaishi kwa wingi pia katika miji mikuu ya mikoa ya nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia. Kihistoria, kiutamaduni na kisiasa, Waislamu wamekuwa na mchango muhimu nchini Thailand kwa karne nyingi. Waislamu nchini Thailand ni wa makabila tofauti na kwa upande wa lugha, wanazungumza lugha ya Thai kiasili. Baadhi ya Waislamu wamehamia Thailand kutoka makabila ya China, Indonesia, Pakistan, Kambodia, na Bangladesh. Thuluthi mbili ya Waislamu wa Thailand ni Wamalayu wa Thai, ambao wanashirikiana lugha na utamaduni mmoja na Waislamu wa Malaysia.

Licha ya kuwa na wateja wachache sana wa bidhaa za Kiislamu ndani ya nchi, lakini Thailand imeonyesha uwezo mkubwa wa kupata wazalishaji wa vyakula na vinywaji vya halali (F&B), kiasi kwamba hivi sasa Thailand ni moja ya wauzaji wakubwa wa bidhaa za halali duniani. Kwa kuongezea ni kuwa, nchi hiyo pia inaonyesha uwezo mkubwa wa utalii wa halali.

Jinsi ya kupata kibali cha bidhaa za Halal nchini Thailand

Kama ilivyo kwa Waislamu wengine ulimwenguni, Waislamu wa Thailand pia wanalipa umuhimu mkubwa suala la kula na kunywa vyakula vya halali, na ni kwa sababu hiyo ndiyo maana, inahimizwa bidhaa wanazouziwa Waislamu wa Thai ziwe na cheti cha halali.

Baraza Kuu la Kiislamu la Thailand (CICOT) ni chombo kilichoundwa na serikali chenye jukumu la kuthibitisha na kufuatilia bidhaa za halali nchini Thailand. Pamoja na ufuatiliaji wa bidhaa za halali, taasisi hii ndiyo yenye mamlaka ya kushughulikia masuala ya Kiislamu nchini humo, kama vile ndoa.

Kama ilivyo kwa nchi nyingine za eneo la ASEAN, kupata kibali cha bidhaa za halali nchini Thailand kuna masharti yake kama kufanyiwa majaribio kadhaa kwenye bidhaa zinazozalishwa.

Viwango vya leseni ya bidhaa za Halali nchini Thailand

1. Kuonesha hati na nyaraka zinazohitajiwa na Baraza Kuu la Kiislamu la Thailand

Wamiliki wa biashara zinazotafuta kibali cha Halali wanatakiwa kuwasilisha maombi yao kwa Baraza Kuu la Kiislamu la Thailand (CICOT). Afisa aliyebobea katika masuala ya halali ameteuliwa kuangalia usahihi wa hati na wa biashara ikiwa nyaraka zinazotakiwa zitakuwa zimekamilika. 

2 . Elimu ya bidhaa za Halali

Biashara ambazo zipo tangu zamani lakini hazina kibali cha bidhaa za Halali lazima waendeshaji wa biashara hizo wapitie mafunzo katika Taasisi ya Viwango vya Halali ya Thailand, ambayo ni taasisi kipekee ya kidini chini ya CICOT inayohusika na masuala ya Sharia ya Kiislamu nchini Thailand. Mafunzo yanahusiana na utengenezaji wa bidhaa za halali. Katika ukaguzi wa kampuni, mfanyabiashara lazima aoneshe uthibitisho wa rekodi za elimu kwa wakaguzi wa bidhaa za halali.

3. Kamati ya ukaguzi wa bidhaa za halali

Baada ya kampuni hiyo kumaliza mafunzo yake, CICOT huunda kamati ya ukaguzi wa bidhaa za halali inayojumuisha wasomi, wanasayansi wa chakula, wataalamu wa uzalishaji na wataalamu wa sekta ya wanyama hasa madaktari wa machinjio.

4. Uchunguzi wa maabara

Timu ya ukaguzi wa bidhaa za halali ina jukumu la kukusanya sampuli za kiwandani kama malighafi za kampuni, na kujikinaisha kuwa zinakidhi masharti ya Taasisi ya Viwango vya Halal ya Thailand. Inachukua sampuli hizo kwa ajili ya kuzifanyia uchambuzi wa kimaabara. Matokeo ya uchunguzi huo wa kimaabara hurejeshwa kwa kamati ya bidhaa za halali.

5. Ukaguzi katika eneo husika 

Timu ya ukaguzi wa Halal ina jukumu la kufanya ukaguzi wa mchakato mzima wa utengenezaji na uzalishaji bidhaa. Hii inajumuisha ukaguzi wa maghala na malighafi.

6. Upasishaji

Hatimaye, Baraza Kuu la Kiislamu la Thailand CICOT na baada ya kukamilika mchakato huo, hutoa idhini ya mwisho na kibali cha bidhaa halali na mkataba kwa biashara.

Uwezo wa juu wa Thailand wa kuzalisha bidhaa za halali

Ingawa Thailand ni nchi yenye Waislamu wachache, ni nchi ya 12 duniani kwa kuuza kwa wingi bidhaa za halali kiujumla na ni ya tano duniani kwa kuuza kwa wingi vyakula vya halal. Chakula cha Halali kinachangia 20% ya jumla ya chakula chote kinachouzwa nje ya Thailand, na 60% ya mauzo yake ya chakula halali huenda kwa nchi zenye Waislamu wengi za Indonesia, Malaysia, na Brunei. Inakadiriwa kuwa, thamani ya soko la kimataifa la chakula halali mwaka 2027 itakuwa ni zaidi ya dola trilioni 2 za Kimarekani kama ambavyo inakadiriwa pia kuwa idadi ya Waislamu itakuwa ni asilimia 25 ya watu wote duniani ifikapo mwaka 2030.

Kutokanana na msaada mkubwa na wa kuendelea wa serikali, Thailand iko katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha uzalishaji bidhaa za halali (F&B) katika eneo la ASEAN. Wizara ya Biashara ya Thailand mara kwa mara huanzisha kampeni za kutangaza bidhaa na huduma zake ili viwanda vya bidhaa za halal nchini humo viweze kunufaika kutokana na ongezeko la uwezo wa ununuzi wa wateja Waislamu duniani kote. Bidhaa muhimu zaidi za Thailand zinazouzwa nje ya nchi ni pamoja na mchele, bidhaa zinazotengenezwa kutoka tapioca yaani wanga unaotolewa kutoka kwenye muhogo, muhogo wenyewe, samaki wa vibati pamoja na matunda na mboga zilizochakatwa. Nchi hiyo imepanua orodha yake ya bidhaa za halali hadi katika bidhaa za vipodozi, kuku, nyama nyekundu na bidhaa za mimea zenye vibali vya vyakula vya halali. Inakadiriwa kuwa, usafirishaji wa vyakula vya Thailand utaongezeka kwa 8.4% mwaka huu wa 2022, na kuifanya nchi hiyo kuwa ya 13 duniani kwa uzalishaji wa bidhaa hizo. Thailand imefanikisha mikakati kadhaa muhimu katika tasnia ya chakula halali, kama vile kuongeza uwezo katika uthibitishaji na uandaaji wa wa bidhaa za halali na kuboresha utafiti na maendeleo yake.

Utalii wa Halali nchini Thailand

Uwezo mwingine muhimu wa uchumi wa halali nchini Thailand ni sekta yake ya utalii halali, ambayo ni moja ya sekta inayokua kwa kasi katika tasnia ya halal. Soko hilo linaweza kufikia watalii milioni 230 ifikapo 2026 na kuiingizia Thailand pato la dola bilioni 300 za Kimarekani.

Kwa mujibu wa takwimu za Global Muslim Travel Index 2022, Thailand iliorodheshwa kuwa nchi ya nne kati ya maeneo 10 ya juu yanayopendelewa na Waislamu nje ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Utalii ni sehemu muhimu ya uchumi wa Thailand, na sekta hiyo inachangia takriban asilimia 20 ya Pato Jumla la Taifa. Pato la Taifa kabla ya janga la corona lilichangia takriban dola bilioni 64 katika uchumi wa ndani ya Thailand.

(Visited 21 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!