Mahakama moja ya mji wa Münster wa magharibi mwa Ujerumani jana Jumatano ilitoa hukumu iliyoruhusu kusomwa adhana katika msikiti mmoja wa mjini humo kwa ajili ya Sala ya Ijumaa.

Tovuti ya Kiingereza ya shirika la utangazaji la Ujerumani DW imeripoti habari hiyo na kusema kuwa, usomaji wa adhana katika msikiti huo ulikuwa umepigwa marufuku baada ya Wakristo wawili, mtu na mkewe kufungua mashtaka na kudai adhana inawavunjia uhuru wao wa kidini. Hata hivyo mahakama hiyo imesema adhana haivunji haki za watu wanaoisikia.

Waislamu wakiwa msikitini nchini Ujerumani

Hukumu hiyo imetolewa baada ya rufaa iliyofunguliwa na mji wa Oer-Erkenschwick wa wilaya ya Recklinghausen wa Rhine-Westphalia Kaskazini huko Ujerumani, ikilalamikia hukumu ya kwanza iliyokuwa imetolewa kupiga marufuku kusoma adhana msikitini hapo.

Akitoa hukumu hiyo, jaji Annette Kleinschnittger amesema: “Kila jamii inapaswa kukubali kwamba baadhi ya wakati mtu ataelewa kuwa watu wengine katika jamii yake wanatekeleza mafundisho ya imani yao.”

Hukumu ya mahakama iliyokatiwa rufaa ilitolewa mwaka 2018 na iliuzuia msikiti huo kusoma adhana siku za Ijumaa baada ya Wakristo hao wawili mtu na mkewe ambao wanaishi umbali wa kilomita nzima kutoka msikitini hapo kulalamika mahakamani kwamba eti adhana inawavunjia uhuru wao wa kidini na kutaka watu walindwe na wasilazimishwe kushiriki katika ibada za kidini kinyume na ridhaa yao. Mahakama hiyo ya Münster imesema, sheria za uhuru wa dini zinazojulikana katika eneo hilo kwa jina la “uhuru hasi wa kidini” hazimpi mtu yeyote haki ya kupinga makundi mengine kutangaza imani yao, bali zenyewe sheria hizo zimewekwa ili kuwalinda watu wasilamizishwe kutekeleza mafundisho ya kidini bila ya ridhaa yao.

(Visited 28 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!