Ofisi ya Biashara na Viwanda ya China na Malaysia (ACCCIM) imesema kuwa, watu wanaovutiwa na bidhaa za halali za Waislamu na ambao si Waislamu inazidi kuongezeka duniani.

Hayo yameripotiwa na toleo la mtandaoni la gazeti la “The Malaysia Reserve” ambalo limemnukuu Tan Tian Meng, Mkurugenzi wa Ofisi ya Biashara ya China na Malaysia akisema kuwa, sababu ya kuvutiwa wasio Waislamu ni kwamba Waislamu wanatilia mkazo na umuhimu mkubwa uhalali wa bidhaa zao hasa vyakula. Kuzingatia huko Waislamu kula vyakula halali kumeongeza itibari ya bidhaa halali za Waislamu kwa watu wote na katika mfumo wa vyakula salama kwa binadamu ikilinganshwa na bidhaa zisizojali uhalali wake wa kidini.

Vile vile amesema: Soko la bidhaa halali limestawi na kupanuka sana hivi sasa kutokana na kuwa, hata wasio Waislamu wanapata yakini kwamba chakula wanachokula ni halali na ni salama kwa afya zao.

Mkurugenzi huyo wa Ofisi ya Biashara ya China na Malaysia pia amesema, kitengo cha nchini Malaysia cha ofisi hiyo kimezidi kupokea tenda na maombi ya kuwafikishia bidhaa halali watu wa maeneo tofauti duniani. Huo ni moja ya misukumo mikubwa ya ustawi wa kiuchumi wa nchi hiyo. Sasa hivi kuna Waislamu karibu bilioni mbili duniani ambao wanaunda takriban asilimia 26 ya wanadamu wote ulimwenguni. Idadi hiyo kubwa inatupa ujumbe kwamba, bidhaa halali zina nafasi kubwa sana katika soko la dunia na katika kuimarika uchumi wa kila nchi ulimwenguni.

(Visited 11 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!