Waziri wa Afya ya Uingereza amewapongeza Waislamu wa nchi hiyo kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha upigaji wa chanjo ya corona au COVID-19.

Kwa mujibu wa The National News, Matt Hancock ametoa pongezi hizo katika kikao kilichozungumzia chanjo ya COVID-19 cha kundi la G7 la nchi zilizoendelea kiviwanda duniani. Ametumia kikao hicho kuwapongeza Waislamu wa Uingereza kwa kufungua milango ya misikiti kuhamasisha watu kupiga chanjo ya COVID-19. Amesema, Waislamu ni jamii ya watu waaminifu nchini humo hususan wakati wa mwezi wa Ramadhani na wako mstari wa mbele kuhamasisha watu kupiga chanjo ya corona.

Wakati huo huo ripoti ya London News Online inaonesha kuwa, jana Jumatano, karibu watu 1,000 walijitokeza katika Msikiti wa  Wimbledon kupiga chanjo ya corona nchini Uingereza. Misikiti huo uliendelea kutoa huduma hiyo hadi katikati ya usiku.

Msikiti wa  Wimbledon wa nchini Uingereza

Chanjo hiyo ilianza kutolewa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 35 na kuendelea, lakini baadaye ilibadilishwa na kutolewa kwa vijana wa kuanzia umri wa miaka 25 na kuendelea.

Mwezi uliopita, uchunguzi wa taasisi ya kukusanya maoni ya YouGov ulionesha kuwa, wananchi wa Uingereza wanaongoza duniani kwa kuwa na hamu ya kupiga chanjo ya corona. Asilimia 90 ya walioshiriki kwenye uchunguzi huo wa maoni walisema watapiga chanjo hiyo.

Katika kikao cha G7 kilichofanyika jana Jumatano Uingereza ikiwa mwenyekiti wa hivi sasa, serikali ya London ilisema kuwa, kumeanzishwa kampeni maalumu ya kuhamasisha watu kupiga chanjo ya corona duniani. Kampeni hiyo inasimamishwa na nchi wanachama wa G7.

Waziri wa Afya wa Uingereza amesema kuwa, kuvutia imani ya walimwengu na kuwafanya wakubali kupiga chanjo za COVID-19 ni changamoto ya kimataifa.

(Visited 8 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!