Katika hali inayoonekana ni kuzidi kujaribu kurekebisha makosa yaliyofanywa na rais wa Ufaransa ya kuchukua misimamo ya kiuadui dhidi ya Waislamu, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo ya Ulaya, leo Jumapili, Novemba 8, 2020 anatarajiwa kutembelea Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar nchini Misri na kutoa ujumbe kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Mtandao wa habari wa al Arabi al Jadid umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Jean-Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, leo anatarajiwa kutembelea Chuo Kikuu cha Kiislamu cha al Azhar mjini Cairo Misri ili kuonana na kuzungumza na Sheikh Ahmad al Tayyib, yaani Sheikh al Azhar na huenda akatoa ujumbe maalumu kwa ulimwengu wa Kiislamu.

Itakumbukwa kuwa, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa amewahi kunukuliwa akidai kuwa, kuna ugaidi na ufashisti wa Kiislamu. Ingawa baadaye alidai amenukuliwa vibaya baada ya kuona hasira kubwa za Waislamu. Vile vile Rais huyo wa Ufaransa ameunga mkono kuchorwa vikatuni vinavyomvunjia heshima Nabii wa rehema, Mtume Muhammad SAW akidai eti huo ni uhuru wa kujieleza. Pia alidai Waislamu wa Ufaransa hawanyanyaswi.

Misimamo hiyo ya kiuadui ya viongozi wa Ufaransa imewakasirisha mno Waislamu kote ulimwenguni na sasa hivi kampeni ya kususia bidhaa za Ufaransa inaendelea. Uchunguzi wa kuaminika unaonesha kuwa, Ufaransa itapata hasara kubwa za kiuchumi iwapo ulimwengu wa Kiislamu utasusia bidhaa zake.

Siku chache zilizopita pia, balozi wa Ufaransa mjini Cairo alionana katika kikao cha faragha na Sheikh al Azhar ili kujaribu kupunguza makali ya misimamo ya chuki ya Emmanuel Macron. Taarifa nyingine zinasema kuwa, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amemshinikiza Mkuu wa Chuo Kikuu cha al Azhar, Sheikh Ahmad al Tayyib asichukue misimamo mikali, kwa kuhofia kuharibika uhusiano wa Cairo na Paris.

(Visited 16 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!