Serikali ya Uingereza imefikia uamuzi wa kupiga marufuku zaidi ya watu kukusanyika pamoja kuanzia Jumatatu ya Septemba 14, 2020 kutokana na kuanza wimbi jipya la maambukizo ya ugonjwa wa COVID-19.

Vyombo vya habari vimeripoti habari hiyo na kuinukuu serikali ya London ikisema kuwa, mabadiliko hayo ya sheria yatazuia mikutano ya watu wengi popote pale katika maeneo ya ndani na ya wazi.

Pamoja na hayo, sheria hiyo haitohusu skuli, maeneo ya kazi au shughuli mbalimbali kama za harusi, maziko na michuano ya michezo ambayo inachunga protokali za afya za kujikinga na corona.

Serikali ya Uingereza imeweka faini ya Pound 100 kwa watu watakaokaidi marufuku hayo na kila kosa litakuwa linaongezeka faini yake hadi kufikia Pound 3,200.

Kabla ya hapo mamlaka ya England ilikuwa imeruhusu mikusanyiko ya zaidi ya watu 6 kutoka familia tofauti katika maeneo ya nje na ya wazi, au au familia mbili za idadi yoyote ya watu ile katika maeneo ya ndani na ya nje. Hata hivyo hadi hivi sasa polisi hawakuwa na nguvu za kisheria za kuzuia mikusanyiko ya watu wasiopindukia 30. Ikumbukwe kuwa Uingereza ndiyo inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vya corona barani Ulaya. Wagonjwa 41,586 wa COVID-19 wameripotiwa kufariki dunia nchini humo hadi hivi sasa. Aidha Uingereza ni ya pili kwa idadi kubwa zaidi ya wagonjwa wa corona barani Ulaya baada ya Uhispania.

(Visited 17 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!