Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary, qarii maarufu wa Misri ambaye wakati alipokuwa safarini nchini Kuwait, alipata misahafu ambayo Wazayuni  walikuwa wameitia mkono na kubadilisha baadhi ya aya zake, akapambana na upotoshaji huo na akawafedhehesha maadui hao wa Uislamu mbele ya walimwengu. Ndiye qarii wa kwanza duniani kurekodi sauti ya Qur’ani nzima.

Mahmoud Khalil al Hussary ni nani?

Sheikh Mahmoud Khalil al Hussary ni qarii maarufu katika ulimwengu wa Kiislamu. Alizaliwa tarehe 17 Septemba 1917 katika kijiji cha Shubra an Namlah cha mji wa Tanta wa mkoa wa Gharbia huko Misri.

Tangu akiwa mdogo kabisa, baba yake alianza kumpeleka mtawalia katika madrasa na vyuo vya Qur’ani vilivyokuwa vikijulikana kwa jina maarufu la Maktaba za Qur’ani. Wakati huo alikuwa akienda mfululizo katika msikiti wa kijijini kwao. Kwa maneno ya wazi zaidi ni kwamba al Hussary alilelewa msikitini.

Baada ya kujifunza usomaji wa aina 10 za Qur’ani Tukufu, al Hussary alijiunga na Chuo Kikuu cha al Azhar kwa ajili ya masomo ya juu zaidi ya Qur’ani Tukufu.

Aliporekodi Qur’ani

Mwaka 1961, Ustadh al Hussary alikuwa mtu wa kwanza kabisa duniani aliyepata taufiki ya kurekodi sauti ya Qur’ani nzima kwa kisomo cha Hafs. Baada ya kushinda mashindano ya yaliyoendeshwa na Radio Qur’an ya Misir, Sheikh al Hussary alifunga mkataba na redio hiyo kwamba iwe ndiyo redio pekee inayorusha usomaji wake wa Qur’ani kwa muda wa miaka 10.

Sauti yenye umaanawi ya Sheikh al Hussary ilikuwa inasikika katika kila kona za Misri, kwenye maeneo ya umma, masokoni, mikahawani, katika shughuli mbalimbali za harusi na za huzuni, alimradi usomaji wake uliojaa umaanawi wa Qur’ani Tukufu ulipamba anga zote za Misri. Kwa vile alikuwa na sura yenye mvuto wa kiucha Mungu, Ustadh al Hussary alipewa lakabu ya Shaikhul Qurra yaani Sheikh wa maqarii na wasomaji wa Qur’ani. Baadhi ya wapenzi wa qiraa yake walipokuwa wanaandika chochote kuhusu Sheikh al Hussary, walikuwa wanamwita kwa jina la Sauti ya Anayemaanisha Anachokisoma.

Jumuiya ya Maqarii

Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary alikuwa mtu wa kwanza aliyeasisi Jumuiya ya Maqarii wa Qur’ani Tukufu ili kulinda na kuhifadhi haki zao.

Mwaka 1960, Ustadh al Hussary alitambuliwa kwa jina la Sheikh wa Masheikh wa Qiraa nchini Misri. Kabla ya hapo alitambuliwa kwa jina la Mtaalamu wa Baraza la Utafiti wa Kiislamu na Mkuu wa Jumuiya ya Kusahihisha Makosa ya Chapa ya Qur’ani Tukufu. Vile vile alikuwa ni mshauri wa mausala ya Qur’ani katika Wizara ya Wakfu ya Misri.

Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary, alitembea mabara matano ya dunia kwa ajili ya kueneza usomaji sahihi wa Qur’ani Tukufu na katika safari zake hizo, alipata taufiki ya kuwasilimisha watu wengi kutokana na qiraa yake ya kipekee.

Wakati akiwa safarini mjini London, kisomo cha Qur’ani cha Sheikh al Hussary kiliwavutia mno viongozi wa ngazi za juu wa Uingerea.

Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary alikuwa na mapenzi makubwa sana ya Qur’ani Tukufu kiasi kwamba kila pale wanawe walipokuwa wakimuomba pesa, alikuwa akiwapa kwa kiwango cha kuhifadhi kwao Qur’ani Tukufu.

Vitabu vyake

Mtumishi huyo wa Qur’ani Tukufu ametunga vitabu vingi. Miongoni mwa vitabu vyake muhimu ni “Ahkam Qiraatul Qur’anil Karim,” “Al Qiraatul ‘Ashr,” “Al Nahjul Jadid fii Ilmit Tajwid” na “Rihilat fil Islam.”

Wakati akiwa safarini nchini Kuwait, Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary aligundua misahafu iliyotiwa mkono na Wazayuni kwa nia ya kuipotosha. Alisimama imara kupambana na upotoshaji huo na alifichua haraka njama hizo za Wazayuni.

Mwaka 1967 Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary aliteuliwa kuwa mkuu wa Jumuiya ya Maqarii Duniani.

Kufariki dunia

Sheikh Mahmoud Khalil al Hussary alifariki dunia tarehe 24 Novemba 1980 baada ya kumaliza kusali Sala ya Isha na baada ya kuitumikia Qur’ani Tukufu kwa muda wa miaka 55.

Kabla ya kufariki dunia, Ustadh Mahmoud Khalil al Hussary alikuwa ameusia kwamba thuluthi moja ya mali zake itumike katika mambo ya kheri na nyumba yake igeuzwe kuwa msikiti.

(Visited 1 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!