Tumo kwenye siku nyingine ya Ijumaa. Nina hamu kila wiki niseme japo machache kuhusu Sura ya 18 ya al Kahf kutokana na umuhimu wake mkubwa, lakini mazonge ya maisha si haba nami. Nukta zinanipitikia nyingi akilini za kuzungumzia lakini huo muda tu ndio mtu unakuwa huna.

Bismillahir Rahmanir Rahim

Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tumo kwenye siku nyingine ya Ijumaa. Nina hamu kila wiki niseme japo machache kuhusu Sura ya 18 ya al Kahf kutokana na umuhimu wake mkubwa, lakini mazonge ya maisha si haba nami. Nukta zinanipitikia nyingi akilini za kuzungumzia lakini huo muda tu ndio mtu unakuwa huna.

Kwa mfano waandishi wa vitabu na riwaya, watu wa maktaba, Wizara za Elimu n.k, wanafundishwa nini na Surat al Kahf katika sehemu zake mbalimbali? Hayo unayapata kwa upana ndani ya sura hii. Watu wa kilimo na mabwanashamba wanaelimishwa nini na aya za Surat al Kahf, hayo pia utayapata kwa upana humo.

Wazazi na walezi wanafundishwa mikakati gani na Surat al Kahf, hayo utayapata kwa wingi pia humo. Watawala na mbinu bora za utawala, aya za Surat al Kahf zinakufundisha yote hayo. Heshima baina ya mwalimu na mwanafunzi zinapaswa kuwaje? Haki ya mwanafunzi ni ipi na haki ya mwalimu ni ipi? Aya zinakufundisha za Surat al Kahf.

Mijadala baina ya Waislamu na wasio Waislamu iweje? Surat al Kahf inatufundisha cha kufanya. Je, mtu anayejihusisha na mambo ya dini ndio aishie tu kwenye dini asijishughulishe na elimu zinazoitwa za dunia? Surat al Kahf inatwambia hapana. Surat al Kahf inatufundisha kivitendo faida za Tenda Wema Wende Zako, Usingoje Shukrani na methali nyingine ya Wema Hauozi.

Sehemu walipoonana Nabii Musa na Nabii Khidhr (Alayhimas Salaam) ni wapi? Nini tofauti ya ilmu ya Nabii Musa na ya Nabii Khidhr? Nini tofauti baina ya majukumu ya Nabii Musa na Nabii Khidhr? Nini maana ya Hamkupewa ilmu ili kihiiibi sana? Kwa nini baina ya visa vyote vilivyomo kwenye surat al Kahf kila baada ya kisa, Mwenyezi Mungu ameweka aya kadhaa kabla ya kusimulia kisa kingine, ila baina ya visa viwili, hicho cha Nabii Musa na Nabii Khidhr na kile cha Dhulk Qarnain? Hakuweka aya zozote baina ya visa hivyo viwili, bali ameviunganisha moja kwa moja?

Huyu Dhul Qarnain ni nani na kwa nini akaitwa Dhul Qar’nain na safari yake hiyo inayosimuliwa na Qur’ani Tukufu hapa, ilifanyika wapi? Hao Juju na Majuju ni viumbe gani? Haya na mengineyo mengi, mna ndani yake nukta nyingi za kuzizungumzia kila siku au kwa uchache kila wiki kuhusu sura hii tukufu ya Qur’ani Tukufu, lakini ndio hivyo, mazonge si haba nasi.

Leo hebu tuangalie busara anazopaswa kuwa nazo mwalimu kwa mwanafunzi wake, mzazi kwa mwanawe, mlezi kwa anayemlea, mtawala kwa anayemtawala, mwenye satua mbele ya mtu dhaifu n.k.

Kwanza Surat al Kahf inatufundisha kwamba, unapomkatalia kitu mtu, ni busara kumueleza sababu za kumkatalia, usifanye udikteta. Kwa kuwa mimi ni baba, nasema tu hapana! Nasema; Usifanye hivi! Mimi kwa kuwa ni mtawala nimeamua iwe hivi, wala usiulize sababu! Mimi nina nguvu, wewe ni nani utake kujua sababu? Aya za Surat al Kahf, za 67 na 68 zinatuonesha kuwa, busara ni mtu kueleza sababu, hasa unapozungumza na mtu mzima bila ya hata kusubiri kuulizwa kwa nini?

Aya za Sura hii ya 18 ya al Kahf zinatufundisha kumpa mtu fursa ya kuona kivitendo sababu za kuzuiwa asifanye jambo fulani na hii inawahusu watu wote. Maana yake ni kwamba, tunatakiwa kufanya urafiki na walioko chini yetu, tusiwaendeshe kipunda na kiimla. Hata kama si kila sehemu lazima tutoe sababu, lakini miamala yetu na walioko chini yetu isiwe ya kidikteta. Wajibu ni kuziteka nyoyo si kuteka hofu kidhabi ambayo haidumu mbali na macho ya anayeogopewa. Kisa cha Nabii Khidhr na Nabii Musa na ushirikiano wao mpaka katika kujenga ukuta wa mja mwema, kinatufundisha mambo mengi.

Nina hamu ya kuzungumzia kwa nini sehemu moja Nabii Musa AS alitumia neno “Imra” na sehemu nyingine akatumia neno “Nukra” lakini naona maelezo yameshakuwa marefu, yasije yakamtia mtu uvivu wa kuyasoma na kuyazingatia.

Mwanafunzi wenu,

Ahmed Rashid.

(Visited 19 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!