Bismillahir Rahmanir Rahim.
Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.
Leo wanafunzi wenzangu nataka tuzungumzie kidogo lengo la kutumwa Mtume kwa wanadamu. Nitazungumza kwa mujibu wa aya ya pili ya sura ya 62 ya al Jumua nikitaraji utakuwa waadhi mzuri wa siku ya Ijumaa tukijaaliwa na siku zijazo na kwa watu wote. Nakuomba ukiisoma makala hii na kama utaona ina manufaa, basi usikae nayo, warushie na wengine ili wafaidike, na wewe pia uongeze thawabu katika akiba ya matendo yako mema.
Aya hiyo tukufu ya pili ya sura ya 62 ya al Jumua inasema:
هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الأُمِّيِّينَ رَسُولا مِّنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ وَإِن كَانُوا مِن قَبْلُ لَفِي ضَلالٍ مُّبِينٍ
Tarjuma yake kwa mujibu wa al Muntakhab ni:
Yeye (Allah) Ndiye aliyempeleka Mtume kwenye watu wasiojua kusoma, awasomee Aya Zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapokuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara kwamba, ukamilifu wa tafsiri ya aya ya Qur’ani ni kuangalia aya za kabla yake na baada yake bali baadhi ya wakati hata sura ya kabla yake na baada yake; ni kuangalia maneno ya kabla na baada yake mbali na ilmu nyingine zinazohusiana na tafsiri. Hapa si mahala pake kutaja kila kitu maana bila ya kujua tutashtukia tumetoka kwenye maudhui tuliyokusudia. Hivyo nitosheke na hayo.
Amma unapoangalia aya ya kabla yake utaona ni utangulizi wa mambo muhimu sana yaliyokusudiwa kuzungumziwa hapa na Mwenyezi Mungu. Aya ya kabla yake na ambayo ndiyo iliyofungua sura hii tukufu ya 62 ya alJumua, inasemaje? Inasema:
يُسَبِّحُ لِلَّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ الْمَلِكِ الْقُدُّوسِ الْعَزِيزِ الْحَكِيمِ
Viliomo mbinguni na viliomo katika ardhi vinamtakasa Mwenyezi Mungu, Mfalme, Mtakatifu, Mwenye nguvu, Mwenye hikima.
Sasa huyu Mwenyezi Mungu Mwenye sifa hizi kubwa mno za al Maliki (Mfalme), al Quddus (Mtakatifu), al Aziz (Mwenye nguvu) na al Hakim (Mwenye hikima) na ambaye kila kisichokuwa yeye kinamtakasa kwa utukufu wake kutaka na kukataa; huyu Ndiye aliyemtuma Mtume Muhammad SAW na Manabii wengine na kazi yao pamoja na mambo mengina, ni kuwafunza watu hikima kutoka kwa al Hakim, (Mwenye hikima).
Si mjadala wetu hapa kwamba ni jinsi gani viumbe wote wanamsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu. Huo ni uwanda mpana mwingine. Si mjadala wetu pia hapa kwamba kwa nini sifa hizo takatifu za Allah zimekuja kwa mpangilio huo, bali mjadala wetu ni malengo na kazi za Mtume tena kwa muhstasari maana mjadala wa al Nubuwah nao pia ni mpana. Tujue tu kwamba kuna tofauti baina ya al Nubuwah na al Nabi inatosha kusema hivyo kwa hapa. Tutambue pia kwamba, baina ya kubaathiwa na kupewa Utume Mtume Muhammad SAW kuna uhusiano kamili na madhubuti na sifa hizo takatifu za Allah za al Maliki, al Quddus, al Aziz na al Hakim zilizokuja katika aya ya kabla ya hii tinayoizungumzia hapa.
Tuingie katika tafsiri ya aya tuliyokusudia na tuanze na kutupia jicho yaliyosemwa kuhusu hilo neno “ummiyyin.”
1- Neno “ummiyyin” ni wingi wa neno “ummiyyi.” Maana yake ni mtu ambaye hajui kusoma. Hilo neno limenasibishwa na mama kwa sababu, mtu ummiyyi ni yule ambaye ukitoa elimu aliyoipata kutoka kwa mama yake, hakwenda darasani kusomeshwa na mtu mwingine yoyote.
2- Wengine wamesema hilo neno “ummiyyin” katika aya hiyo lina maana ya watu wa Makkah maana mji huo mtakatifu ni mama ya miji mitukufu. Hata hivyo kauli hiyo ni dhaifu kwa sababu Mtume hakutumwa kwa watu wa Makkah tu. Hata hii sura pia imeteremshwa Madina haikuteremshwa Makkah.
3- Wafasiri wengine wamesema hilo neno “ummiyyin” hapo limekusudia umma wa Waarabu. Ushahidi wao ni aya ya 75 ya sura ya tatu ya Aal Imran. Sehemu moja ya aya hiyo inawanukuu Mayahudi wakisema: Haya ni kwa kuwa (Mayahudi) wakisema: Hatuna lawama kwa ajili ya hawa wasiojua kusoma. Yaani kwa mtazamo wa Mayahudi, watu wote ni wajinga isipokuwa wao tu.
Pamoja na yote, tafsiri ya kwanza ya hilo neno “ummiyyin” inaonekana inafaa zaidi na iko karibu zaidi na uhalisia wa mambo.
Amma moja ya miujiza mikubwa hapa ni kwamba, Bwana Mtume Muhammad SAW ametokana na watu hawa hawa “ummiyyin” wasiojua kusoma lakini angalia dini aliyokuja nayo. Angalia muujiza mkubwa na wa milele yaani Qur’ani aliotumwa nao. Vipi muujiza mkubwa kama huu anaweza kuja nao mtu ambaye si tu hakuna mtu yeyote aliyemsomesha, lakini pia hata hakuishi katika mazingira ya wasomi; sasa kama si muujiza wa Mwenyezi Mungu ni nini? Nani mwengine ghairi ya Mwenyezi Mungu anaweza kuwa mwalimu wa Mtume Muhammad SAW? Nani ghairi ya Allah, mwenye uwezo wa kuteremsha muujiza kama wa Qur’ani? Hayupo. Yako mengi ya kusema kuhusu hii maudhui, lakini tuishie hapo kwa leo.
KAZI ZA MTUME
1- Kazi ya kwanza kabisa ya Mtume kwa mujibu wa aya hiyo ya pili ya Surat al Jumua ni tilawa. Kuna tofauti baina ya tilawa na qiraa. Kwa mujibu wa kitatu cha al Mufradat cha al Raghib al Isfahani, tilawa ina maana mbili ina maana ya kusoma bila ya kuzingatia na kusoma kwa kuzingatia na kutaamali na kutadabari aya za Qur’ani. Amma qiraa ina maana moja, ni kusoma aya za Qur’ani juu juu bila ya kuzingatia undani wa maana za aya za Qur’ani.
Hivyo kazi ya kwanza kabisa ya Bwana Mtume Muhammad SAW ni kuwasomea Waislamu na wanadamu aya za Qur’ani Tukufu kwa sura zote mbili, kuwasomea wasikie maneno ya Allah na kuwasomea kwa namna ambayo alihakikisha wanazingatia maana za aya hizo na ni kwa sababu hiyo ndio maana Bwana Mtume alipata wapinzani wengi sana kwa sababu maadui walielewa taathira kubwa chanya za usomaji wake wa aya za Qur’ani. Kuna matukio mengi yaliyoonesha miujiza ya tilawa ya Bwana Mtume Muhammad SAW kuanzia wale wakuu wa washirikina wa Makkah walivyokuwa wakijibanza penuni ili kusikiliza tilawa ya Mtume, mpaka visa vya wasio Waislamu walivyokuwa wakibubujikwa na machozi hadi viumbe wengine wasio wanadamu walivyotekwa na tilawa ya Bwana Mtume Muhammad SAW ya aya za Qur’ani Tukufu. Kwa hakika Bwana Mtume aliitekeleza kazi hii ya tilawa kwa njia bora na mafanikio makubwa kabisa. Wakati nilipotoa darsa za maqamat, lahani na naghma za tajwidi nililigusia suala hili la tofauti baina ya sauti na naghma. Ukitaka darsa hizo utazipata kwenye tovuti ya https://ahramed14.com.
2- Kazi ya pili ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa mujibu wa aya ya pili ya Surat al Jumua ni tazkia na na kulea nafsi za Waislamu na wanadamu kwa ujumla. Hili suala la tazkia nalo ni pana sana. Kama tunavyojua limo mpaka kwenye mali. Sikutaka kuifanya ndefu hii makala, lakini hata hapa naona imeshakuwa ndefu. Nitosheke na hapo. Niseme tu kwamba kuna hikma kubwa katika huku kutangulia tazkia kabla ya taalim katika aya hii tukufu. Yaani kusafisha kabla ya kutoa elimu. Aya hiyo tukufu imeanza na tazkia baadaye imekuja kwenye taalim. Tab’an katika baadhi ya aya utaona zimetanguliza tazkia mbele ya taalim na nyingine zimetanguliza taalim mbele ya tazkia na kila ilipotokea hivyo imekuja kwa hikma kubwa. Baadhi ya wakati akhlaki na maadili bora ndio huzaa ilmu na baadhi ya wakati ilmu hupelekea watu kuwa na akhlaki na maadili mema. Ni vitu vinavyokamilishana na kila vinapotenganishwa ndio hapo tunapoona maafa haya yaliyoko duniani leo ya kukosekana maadili mema katika elimu.
3- Kazi ya tatu ya Bwana Mtume Muhammad SAW ni kusomesha. Naam, Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa mwalimu. Moja ya kazi za Manabii ni ualimu. Wizara ya Elimu ni nguzo muhimu mno katika kila nchi, taifa na jamii, ingawa baadhi ya wakati walimu na wizara hiyo havipewi hadhi na heshima inayotakiwa. Kuwasomesha wanadamu Kitabu na Hikma ni kazi nzito sana, lakini ilfanywa kwa njia bora na kwa ufanisi wa hali ya juu na Bwana Mtume Muhammad SAW.
TOFAUTI BAINA YA KITABU NA HIKMA
Kama tulivyoona, kazi ya tatu ya Bwana Mtume Muhammad SAW kwa mujibu wa aya ya pili ya sura ya 62 ya al Jumua, ni kusomesha Kitabu na Hikma. Sasa kumezungumzwa mambo kadhaa kuhusu tofauti baina ya Kitabu na Hikma. Hapa nitataja baadhi yake:
1- Kwanza imesemwa, huenda maana ya Kitabu hapo ni Qur’ani na Hikma ni hadithi za Bwana Mtume Muhammad SAW yaani vile alivyokuwa akiwafundisha masahaba aya za Qur’ani Tukufu, kivitendo, kimaneno n.k, kama ilivyo maarufu katika “ilmul hadith.”
2- Pili huenda neno Kitabu hapo linaashiria asili ya maamrisho ya Uislamu na neno Hikma linaashiria falsafa na siri za maamrisho na amri hizo za Uislamu.
MAANA YA HIKMA
Hili neno hikma lina visawe (synonyms) vyake vingi. Lakini hapa nitagusia maana ambayo mimi kwa uchache wangu wa ilmu, ndio kwanza nimeiona. Ninanukuu: Neno hikma asili yake lina maana ya kuzuia kitu na kukidhibiti kwa ajili ya kukirekebisha na kukiongoza njia sahihi na ndio maana hata lijamu ya kipando, moja ya majina yake ni “hikmat” kwa sababu ujamu unatumika kumzuia mnyama asifanye ukaidi, kumdhibiti na kumuongoza njia sahihi ili asile vipando na mimea ya watu na aende sehemu anayoelekezwa. Tunapozingatia maana hiyo tutaona kuwa, hikma ni akili inayomdhibiti mwanadamu asitende mambo yasiyofaa mfano wa lijamu. Kwa kweli hikma na akili ni vitu visivyotengana hata sekunde na lahdha moja. Kila penye akili pana hikma na busara na kila penye busara na hikma, pana akili. Aidha tunapofanya tadaburi katika kazi hii ya tatu ya Mtume ya kusomesha Kitabu na Hikma kwa mujibu wa aya ya pili ya sura ya al Jumua tutaona kuwa, moja ya falsafa za kutumika kwa pamoja maneno Kitabu na Hikma huenda ni kwamba Hikma hapa ni akili na Kitabu hapa ni wahyi yaani Qur’ani Tukufu. Qur’ani ni kitabu cha wenye akili, busara na watu wanaoangalia mbali. Anayeidharau Qur’ani, huyo hana akili.
Niseme pia hapa kwamba, hukumu za Mwenyezi Mungu na mafundisho matukufu ya Qur’ani mbali na kwamba utekelezaji wake ni ibada na kumtii Mola Muumba, lakini pia yanakubaliana kikamilifu na akili na maumbile ya mwanadamu.
KWA NINI “DHALAL AL MUBIN?”
Maneno “dhalal al mubin” yaani upotofu ulio wazi na dhahiri kabisa ndiyo yanayohitimisha aya ya pili ya sura ya al Jumua. Naam, hapa inaonekana wazi kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka kutuonesha kuwa, kila jambo lina kipimo cha kufanikiwa na kufeli kwake. Kipimo cha kazi ya Bwana Mtume SAW ni kuwatoa watu kwenye upotofu ulio wazi na kazi hiyo inaendelea hadi leo na itaendelea hadi siku ya Kiyama kwa kutunzwa na kupewa hadhi yake Qur’ani na mafundisho ya Bwana Mtume SAW.
Ni vyema hapa nitoe mifano ya kufanikiwa Bwana Mtume Muhammad SAW kuwatoa watu katika upotofu ulio wazi hata kabla ya kuondoka kwake duniani na kurejea kwa Mola wake kwa fakhari kubwa. Tuiangalie jamii ya Waarabu kabla ya kuanza kazi ya Bwana Mtume na baada yake. Wakati wa ujahilia yaani kabla ya kuanza kazi ya Bwana Mtume Muhammad SAW, upotofu ulio wazi na mkubwa sana ulikuwa umeifunika jamii ya Waarabu.
1- Hivi kuna upotofu gani mkubwa na wa wazi zaidi ya ule wa watu kuchonga kwa mikono yao, mawe na miti halafu kudai ni miungu na kuanza kuieleza shida zao na kutaraji itawatatulia na kufikia hata kuitolea kafara wakati wenyewe wanajua kuwa midude hiyo haina hisia zozote. Ni nani bora, fundi mwenye akili, au dude alilotengeneza kwa mikono yake, lisiloweza kumdhuru wala kumnufaisha? Waarabu wakitengeneza pia miungu kwa tende, njaa ilipokuwa inawashika walikuwa wakienda kuinyofoa kidogo kidogo miungu hiyo na ilikuwa haionesha reaction yoyote ya angalau kupiga kelele jamani mnaninyofoa! Mnaniumiza! Kuna upotofu mkubwa zaidi ya huo? Lakini Mtume alifanikiwa kuisafisha al Kaaba na hakukubakia hata sanamu moja.
2- Hivi kuna upotofu gani mkubwa na wa wazi zaidi ya ule wa mtu kuchukua damu yake, kitoto chake kichanga, malaika wa Mungu na kwenda kumzika hai. Zile hisia za baba zilikuwa wapi wakati walipokuwa wanaona vitoto vyao vidogo na vichanga vya kike vinawaangalia kwa macho ya huruma na wao kwa ukatili wao mkubwa wanawafukia ardhini wakiwa hai na wakikata roho mbele yao? Kwa kweli naona uzito sana hata kuelezea visa vya kutia huruma mno vya ukatili huo wa zama za ujahilia, bora niishie hapo… Bwana Mtume SAW alifanikiwa kusafisha kabisa ukatili huo.
3- Hivi kuna upotofu gani mkubwa na wa wazi zaidi ya ule mtu kumchukua mama yake na kumfanya bidhaa na urithi wake? Tutambue kuwa, mke wa baba ni mama ingawa hakukuzaa na mume wa mama ni baba angawa wa kufikia. Sasa vipi mama yake mtu atamfanya bidhaa sawa na mali nyingine kama wanyama, mashamba na nyumba? Huo ni katika upotofu mkubwa ambao Bwana Mtume Muhammad SAW alipambana nao na akahakikisha ameuondoa kabisa hata kabla hajaondoka duniani. Inasikitisha lakini kuona kuwa, leo hii yale ya kufanywa wanawake ni bidhaa ndiyo yaliyojaa duniani kwa madai ya eti kumpa uhuru wake mwanamke.
4- Hivi kuna upotofu gani mkubwa na wa wazi zaidi ya vile vituko walivyokuwa wakifanya Waarabu wa Makka, vya wanawake kuzunguka al Kaaba wakiwa uchi wa kuzaliwa huku wakipiga mbinja na makofu wakijidanganya kwamba walikuwa wakifanya ibada? Waarabu wa enzi za ujahilia walijaa mambo ya upotofu, mauaji, wizi, uporaji na maasi ya kila namna, lakini Mtume kwa taufiki ya Allah alifanikiwa kusafisha sehemu kubwa ya upotofu uliokuwa umeenea enzi hizo. Siwezi kusema kwamba kabla ya kuondoka duniani Bwana Mtume alifanikiwa kuondoa upotofu wote lakini mtukufu huyo wa daraja aliweka misingi ya kuhakikisha upotofu wote unatokomezwa. Iwapo wanadamu watayafuata ipasavyo mafundisho ya Uislamu, hakuwezi kubakia upotofu wowote. Nimalizie tafsiri ya aya hii ya pili ya sura ya 62 ya al Jumua kwa kunukuu sehemu moja ya aya ya 103 ya sura ya pili ya Aal Imran inayosema: …kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyokuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu, kwa neema Yake mkawa ndugu. Na mlikuwa ukingoni mwa shimo la moto, Naye akakuokoeni nalo…
Naam, mtu anapouliza kazi za Manabii ni zipi, Qur’ani ina majibu mapana, ya wazi na ya kukinaisha kabisa kama hayo.
Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Mwanafunzi mwenzenu, Ahmed Rashid.