Vivutio vya watalii nchini Indonesia ni vingi. Usanifu majengo wa Kiislamu, ni sehemu muhimu sana katika ustaarabu na utamaduni wa Indonesia. Miongoni mwa usanifu majengo unaostaajabisha walimwengu ni wa misikiti ya Indonesia.
Hapa tutatoa maelezo mafupi kuhusu msikiti unaojulikana kwa jina la Tiban. Ni msikiti wenye usanifu wa kipekee ambao unawavutia watu wengi ndani na nje ya Indonesia. Msikiti huo uko katika mkoa wa Java Mashariki katika eneo la Malang.
Hata watalii wasio Waislamu wanapenda sana kwenda kwenye Msikiti huo kushuhudia usanifu wake wa kipekee. Pembeni mwa Msikiti huo pana soko kubwa ambalo linapokea watu wengi kila siku.
Msikiti wa Tiban umejengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 6. Ni msikiti wa ghorofa 10. Sehemu kubwa ya kuta na minara yake zimenakshiwa kwa vigae vya rangi ya bluu. Uchoraji wa aya za Qur’ani ndani yake ni wa kipekee ambao hauyachoshi macho wakati yanapoangalia.
Ujenzi wa msikiti huo ulianza mwaka 1967 na ulimalizika baada ya miaka 10 yaani mwaka 1978. Sasa hivi msikiti huo wa Tiban ni moja ya vivutio vikubwa vya utalii katika eneo hilo na nchini Indonesia kiujumla. Maelfu ya watalii hutembelea eneo hilo kila siku kutoka ndani na nje ya Indonesia. Watalii kutoka nje ya Indonesia wengi wao ni wale wa Malaysia, Brunei na nchi nyingine jirani.
Msikiti huo una vyumba 170 na kila chumba kina ukubwa na upana wake. Uhandisi ujenzi wa Msikiti huo pia umechanganywa baina ya ule wa nchi za Kiarabu, Thailand, Java Mashariki na Indonesia kiujumla.
Msikiti huo una chuo cha Kiislamu kinachotoa mafunzo masaa 24. Ndani yake mna pia mkahawa wa kijadi, sehemu ya kufikia wageni, maktaba n.k. Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za msikiti huo tukiwa na matumaini zitakuvutia.