Baada ya kuakhirishwa muda mrefu ufunguzi wake, hatimaye Waislamu nchini Ugiriki wameruhusiwa kusali katika Msikiti pekee rasmi nchini humo, lakini kwa idadi chache.

Kwa mujibu wa mtandao wa Greek City Times, Waislamu 18 wanaoishi Athens, mji mkuu wa Ugiriki, Jumatatu, Novemba 6, 2020, waliruhusiwa kutekeleza ibada ya kwanza ya Sala msikitini humo, kwa idadi hiyo ndogo.

Ufunguzi wa Msikiti huo ambao ujenzi wake ulimalizika mwaka jana 2019, umeakirishwa mara nyingi licha ya kwamba msikiti huo umejengwa bila ya mnara kwani serikali ya Ugiriki haiwaruhusu Waislamu kutumia spika za msikiti kufikisha sauti zao nje ya msikiti huo.

Waislamu nchini Ugiriki wameruhusiwa kuwa na msikiti huo pekee rasmi kwa sharti kwamba serikali ya Athens ndiyo isimamie kila kitu ikiwa ni pamoja na kuchagua viongozi wa Msikiti huo. Msikiti huo una uwezo wa kupokea Waislamu 300 wanaume na 50 wanawake kwa wakati mmoja, hata hivyo Waislamu 18 tu ndio walioruhusiwa na serikali kusali Sala ya kwanza kabisa msikitini humo.

Sheikh Zaki Muhammad mwenye asili ya Morocco ndiye aliyesalisha Sala ya kwanza kabisa ya jamaa msikitini hapo. Amehamia nchini Ugiriki zaidi ya miaka 25 iliyopita na anazungumza lugha tatu za Kiarabu, Kigiriki na Kifaransa. Amesomea masomo ya Kiislamu na hisabati.

Msikiti huo uko katika aneo la Votakinos mjini Athens. Serikali ya Ugiriki imetoa amri ya kufunguliwa Msikiti huo nusu saa kabla ya Sala ya Alfajiri na hufungwa nusu saa baada ya Sala ya Isha. Inatarajiwa kuwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani Msikiti huo utakuwa wazi kwa masaa 24.

Athens ndio uliokuwa mji mkuu pekee wa nchi za Ulaya ambao haukuwa na Msikiti.  Mpango wa kujenga Msikiti huo ulipasishwa mwaka 2007 lakini ulipingwa vikali na Kanisa la Orthodox na watu wenye hisia kali za kitaifa wenye chuki na Uturuki.  Ujenzi wa Msikiti huo ulimalizika mwaka jana 2019 kwa gharama ya euro laki nane (800,000) na ujenzi wake umesimamiwa na serikali. Hata hivyo ufunguzi wa msikiti huo ulikuwa ukiakhirishwa mara kwa mara kwa visingizio tofauti kutokana na upinzani wa kanisa na watu wenye misimamo mikali ya kitaifa wasiowapenda Waislamu hasa wenye asili ya Uturuki.

Katika miaka ya huko nyuma, Waislamu nchini Ugiriki walikuwa wakitekeleza ibada zao katika maeneo ya chini ya ardhi hasa Sala na muda wote walikuwa wakiiomba serikali iwajengee Msikiti rasmi. Hatimaye serikali imekubali baada ya Waislamu kukubali masharti yote waliyowekewa na watawala.

Mwaka jana Naim al Ghandour, Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ugiriki alilalamikia ramani na udogo wa Msikiti huo.

Alisema, Ugiriki ina Waislamu wasiopungua laki tano (500,000) na msikiti huo mdogo hauwezi kukidhi haja za Waislamu wote hao. Jengine lililolalamikia na al Ghandour ni kwamba, ramani ya msikiti huo imechorwa kwa namna ambayo haifanani kivyovyote vile na jengo la Msikiti, bila ya shaka lengo la kuchorwa hivyo ramani hiyo ni kukataa kuonesha nembo ya Waislamu japo moja katika nchi hiyo ya Ulaya.

(Visited 270 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!