Bila ya shaka swali hili limekupitikia mara kadhaa kwamba, kazi ya kuchapisha Misahafu ilianza wapi na mwaka gani? Nyaraka za ulimwengu wa Kiislamu zinatoa uthibitisho gani kuhusu suala hilo na je tangu mwaka gani Waislamu walipata mwamko wa kuchapisha Qur’ani Tukufu? Hapa chini tumeweka kwa muhtasari majibu ya maswali hayo na picha.
Msahafu wa kwanza kabisa kimili na sahihi ulichapishwa nchini Russia mwaka 1803 Milaadia. Msahafu huo ulichapishwa katika mji wa Kazan, makao makuu ya Jamhuri ya Tatarstan huko Russia.
Toleo la mtandaoni la gazeti la An’am limemnukuu Mufti wa Jamhuri ya Tatarstan, Sheikh Kamil hazrat Samigullin (Kamil Samiullah) akisema katika hotuba yake kwenye sherehe za Chuo Kikuu cha Kiislamu mjini Kazan kwamba, Msahafu wa kwanza kabisa sahihi na kamili ulichapishwa mjini humo mwaka 1803 Milaadia.
Ijapokuwa Kazan wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti wa wafalme wa Urusi ambao walipiga marufuku masuala ya kidini lakini Waislamu wa mji huo walifanikiwa kuchapisha Msahafu wa kwanza kabisa ulio sahihi katika historia ya uchapishaji wa Kitabu hicho kitakatifu.
Mufti Kamil hazrat Samiullah amenukuliwa na gazeti hilo akisema: Tunajivunia kuona kwamba Msahafu wa kwanza kabisa sahihi katika Ulimwengu wa Kiislamu, ulichapishwa kwenye mji wetu wa Kazan.
Amesema, Msahafu wa kwanza kabisa kuchapishwa katika moja ya miji mikuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, ni Msahafu huu uliochapishwa mwaka 1803 Milaadia katika enzi hizo ambazo Kazan ilikuwa moja ya miji mikubwa ya Kiislamu. Ijapokuwa Kazan wakati huo ilikuwa chini ya udhibiti wa wafalme wa Urusi ambao walipiga marufuku masuala ya kidini hasa Uislamu na hususan masuala ya kuchapisha vitabu vya lugha ya Kiarabu, lakini pamoja na hayo Waislamu wa mji huo walifanikiwa kuchapisha Msahafu wa kwanza kabisa ulio sahihi katika historia ya uchapishaji wa Kitabu hicho kitakatifu.
Mufti wa Jamhuri ya Tatarstan pia amesema, utafiti uliofanywa na wataalamu wa nchi za Kiarabu unaonesha kuwa, Msahafu wa kwanza kabisa duniani ulichapishwa mwaka 1537 Milaadia katika mji wa Venice huko Italia. Mwaka 1694 kulichapishwa Msahafu mwingine katika mji wa Hamburg, Ujerumani. Mwaka 1787 Miladia kulichapishwa Msahafu mwingine katika mji wa Saint Petersburg nchini Russia chini ya usimamiaji wa Mufti wa wakati huo wa Kazan. Hata hivyo Misahafu yote hiyo ilikuwa na makosa mengi. Imma haikuchapishwa kwa khat za Uthman, au aya zake zilikuwa hazikutenganishwa na zilikuwa na makosa mengi na mabaya sana ya chapa kiasi kwamba Waislamu waliikataa Misahafu hiyo.
Mufti Samilullah amemalizia kwa kusema, hata hivyo Msahafu uliochapishwa baadaye mjini Kazan, ulikuwa kamili na bila ya makosa na kwa mujibu wa maandishi ya juu ya gamba lake, Msahafu huo ulichapishwa mwaka 1803 Milaadia.