‘بِسْمِ ٱللَّٰهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ

أَمۡ يَقُولُونَ شَاعِرٞ نَّتَرَبَّصُ بِهِۦ رَيۡبَ ٱلۡمَنُونِ

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Leo nilikuwa nasoma sura ya 52 ya Tur nikaguswa zaidi na hiyo aya ya 30 hasa ilipotumika hiyo istilahi ya “Raybal Manun.” Nikasema, kila siku naipita nikiipituka hii aya lakini haijawahi kunipitikia kujiuliza hii istilahi maana yake ni nini. Yaani Raybal Manun na hapa imetumika vipi na ina uhusiano gani na hiyo natarabbas,

Maana ya hiyo aya kwa Kiswahili kwa mujibu wa tarjuma ya al Muntakhab ni “Au wanasema: Huyu ni mtunga mashairi, tunamtarajia kupatilizwa na dahari.

Mara zote huwa nasema, mtu akitaka kujua maana sahihi na kwa upana ya aya au neno la Qur’ani tukufu, basi anapaswa kuzingatia pia mtungo wa aya za kabla na baada yake na mtungo wa aya wenyewe. Hivyo nimerudi juu kidogo kumbe huu ni muendelezo wa shutuma na tuhuma tu za makafiri kwa Mtume. Kabla ya aya hiyo walimwita ni kuhani ni majinuni. Hilo neno majinuni nalitumia hivyo hivyo kutokana na maana zilizotolewa na wafasiri wa Qur’ani Tukufu.

Hilo neno rayb katika istilahi ya raybal manun, asili yake ni shaka. Laa rayba fiih, sasa hapa mbona limetumika kwa maana ya kupatilizwa? Manun asili yake ni upungufu, kukatika kitu, kupungua n.k, lakini hapa Sheikh Ali Muhsin amelifasiri kwa maana ya dahari. Bila ya shaka yoyote ana mashiko yake madhubuti. Na ndivyo ilivyo, mashiko yake ni madhubuti.

Hilo neno manun limefasiriwa pia katika lugha kwa maana ya dahari na mauti. Ndio maana baadhi ya wafasiri wameifasiri “natarabassu bihi raybal manun” kwa maana ya tunasubiri kifo chake. Lakini wengine kama hii tarajama ya Kiingereza wamefasiri kwa maana tunasubiri Muhammad yamfike ya kumfika. “Do they say, ‘[He is] a poet, for whom we await a fatal accident’?”

Dua ya kuku haimpati mwewe. Makafiri baada ya kuona hawawezi kukabiliana na Mtume SAW kwa hoja walianza kumporomoshea matusi na shutuma na tuhuma zisizoingia akilini. Mara walimwita kuhani, mara walimwita mshairi mara walimwita punguwani, mara walimwita mwenyedawazimu, mara amepagawa. Alimradi hawakumbakisha, na kama wangeliweza wangelimla nyama, lakini wapi!

Nukta (point) ninayotaka kuanza nayo hapa ni kwamba, hizo sifa mbaya walizokuwa wanampa Mtume zenyewe zilikuwa zinagongana. Kwa mfano wakimwita mtunga mashairi, kawaida mtunga mashairi ni mtu mwenye hikma na busara na akili za kuteua vizuri maneno na ni mtu fasaha wa lugha. Ushairi unaochunga misingi ya Uislamu ni jambo zuri sana. Lakini hapo hapo huyo huyo waliyemwita mshairi wakimwita pia punguwani na mpumbavu na mtu aliyepagawa. Alah! Nyie vipi? Mtu huyu huyu ana akili na hapo hapo hana akili? Msio na akili ni nyiye makafiri.

Swahib Tafsir al Nnur amegusia points na nukta kadhaa kuhusu aya hizo zinazofanana hapo na hapa nanukuu kama alivyoandika: Nimefasiri neno kwa neno na nimepunguza baadhi ya nukta ambazo nimehisi zimejirudia. Ameandika hivi:

“Kuhani ni mtu ambaye anajifanya kujua siri na mambo ya ghaibu na ana mawasiliano na majini na wanamwambia kila anachotaka. Yaani kwa lugha ya moja kwa moja, ni mpiga ramli. “Raibal Manun” ni istilahi inayotumika kwa maana ya matukio machungu katika maisha hasa kifo na mauti.

Lengo la washirikina hapa kumwita Mtume majinuni, hawakukusudia mwendawazimu, maana mwendawazimu haiendani na kuhani na mshairi ambao ni watu wenye akili. Hivyo maana hapa itakuwa ni mtu aliyekumbwa na majini na sasa anatoa bishara za mambo yajayo kama wafanyavyo makuhani na wapiga ramli na maneno anayapanga kama washairi.

Maana nyingine ni kwamba washirikina walikuwa wamachanganyikiwa, hivyo walikuwa wanavurumisha tu tuhuma zisizo na msingi kwa Mtume Muhammad SAW bila ya kujali migongano iliyopo kwenye tuhuma zao. Mara watamwita punguwani, mara kuhani, mara mshairi alimradi akutukanaye hakuchagulii tusi.

Baadhi ya tunayojifundisha katika aya hizi:

1- Haipasi kuogopa matusi na tuhuma zisizo na msingi za makafiri kama kuitwa mchawi, au kuhani, au mshairi au mjinga au mtu aliyepagawa. Lililo wajibu ni mtu kuendelea kufikisha ujumbe wa Uislamu bila ya kushughulishwa na maneno ya watu waliochanganyikiwa kama hao washirikina wa Makkah. Mwenyewe Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Wake, kumbusha na wewe aslan si kuhani kama wanavyodai hao makafiri.

2- Mwenyezi Mungu ameapa kuwahami na kuwalinda mawalii wake kama aya inavyosema: فَذَكِّرْ فَمٰا أَنْتَ بِنِعْمَةِ رَبِّكَ بِكٰاهِنٍ وَ لاٰ مَجْنُونٍ   Basi kumbusha! Kwani wewe, kwa neema ya Mola wako Mlezi, si kuhani wala mwendawazimu.

3- Anayefanya tablighi ajikubalishe na atambue kuwa muda wote atakumbwa na mishare ya tuhuma na maneno yasiyo sahihi. Hilo si jambo jipya.

4- Kadiri mtu anapojiweka mbali na madhambi na nuksani za kibinadamu ndivyo anavyozidi kuwa chini ya kivuli na rehema na neema zenye baraka za Mwenyezi Mungu. Aya imesema wazi kumtuliza Bwana Mtume na kumwambia wewe uko ndani na rehema na neema za Mola wako Mlezi na kamwe wewe si punguani, wala si kuhani wa kutabiri mambo ya uongo. (Tuzilee nafsi zetu kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara na tuzipandishe daraja nafsi zetu kila sekunde kwa mbinu mbali ambazo baadhi yake tuliwahi kuzisema humu wakati tulipokuwa tunatoa majibu ya babu wa Mtondoo Butu kuhusu watu wanaofanya ibada na kujivuna).

5- Tunajifunza katika aya ya 29 ya Sura hiyo hiyo ya Tur kwamba makuhani na wapiga ramli wako mbali na rehema za Mwenyezi Mungu. Neema ni za Mtume na wafuasi wake wanaojiweka karibu na Allah kwa kuwa wao si makuhani wala si punguwani na wala si wendawazimu.

6- Adui hana sababu kama tulivyosema, mtu asitarajie kuna siku matusi na tuhuma zao zitaisha na hata kama zitakuwa shutuma zao haziingii akilini, lakini daima wataendelea kuzitoa.” (Tunaona jinsi makafiri leo duniani wanavyowasakama Waislamu, kuwatukana, kumtukana Mtume, kumchora vibonzo n.k. Tusitaraji kuwa haya yatakwisha, labda siku Waislamu watakapoachana na dini yao).

Baada ya kunukuu nukta na nasaha hizo tuendelee kwa kusema, je, wakati Waislamu wawanapotukanwa wakae kimya? Hapana! Hatuna sisi akupigaye kibao chavu hili mgeuzie la pili. “Laa tadhlimu wala tudhlamun.” Msidhulumu lakini pia msikubali kudhulumiwa. Sawa kuna aya inayosema wanaposemezwa na wajinga husema salama, lakini linapofika suala la kulinda mtu heshima yake na dini yake na dhati yake, anapaswa asimame kujihami. Mfano ni hapa. Je, Mwenyezi Mungu hapa alimruhusu Mtume akaye kimya mbele ya shutuma hizo za makafiri? Hapana! Alimpa majibu ya kuwaambia. قُلۡ تَرَبَّصُواْ فَإِنِّي مَعَكُم مِّنَ ٱلۡمُتَرَبِّصِينَ “Sema: Tarajieni, na mimi pia ni pamoja nanyi katika kutarajia.

Kama nyinyi mnatarajia yanifike ya kunifika, mimi natarajia ulinzi wa Allah na adhabu kali itakayokufikeni.

Kama nyinyi mnataraji kwa kuondoka kwangu duniani ndio Uislamu utaisha, mimi nataraji ulinzi kutoka kwa Allah na ataibakisha milele dini yake hii hata kama mtachukia.

Kama mnataraji dahari inimalize, mimi sitaraji chochote ila alichonipangia Mola wangu. Lakini tu je, yuko kati yetu atakayebakia milele hapa duniani? Lakini mimi natarajia mamilioni ya watu watanitaja kwa kheri na watapata nuru niliyokuja nayo, huku nyinyi mkilaaniwa milele na milele na wala njama zenu hazitofua dafu.

Naam, haya ndiyo matarajio ambayo tunatakiwa sote tuwe nayo. Matarajio ya kutawakali kivitendo kwa Mwenyezi Mungu, si kujipweteka.

Naona yanatosha ingawa si yote niliyoyaona kwenye hizi tafsiri nilizochungulia na kuelewa kwa kiwango hicho hicho kidogo cha welewa wangu uliojaa nuksani…

Tab’an kuna mambo mengi hatujayasema. Kuna vitu kama sababu ya kushuka hiyo aya ya 30 ya sura ya 52, hiyo raybal manun kwa nini likatumika hilo neno rayb, kuna mjadala wa nahw kama hilo neno Shaair kuwa ni khabar ya mubtada mahdhuf na taqdiri yake ni “huwa shaa’ir” mengi yamezungumzwa kuhusu hiyo aya. Lakini muda hauruhusu tena. Na nimemnukuu yale muhimu zaidi kuliko yote. Kila tukipata fursa tutakuwa tukikumbushana hivyo hivyo kiduchu kiduchu.

(Visited 67 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!