Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuhu. Ndugu yangu, Je unajua tasbihi ni nini?

Tasbihi ni dhikri ambayo wawalikuwa wakiisoma mtawalia ndege na majabali pamoja na Nabii Daud AS. Qur’ani Tukufu inasema:

وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ وَكُنَّا فَاعِلِينَ

Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tuliofanya hayo. al Anbiyaa 21: 79.

Tasbihi ni dhikri ya viumbe wote. Qur’ani Tukufu inasema:

أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ وَاللَّهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ

Je! Huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtakasa vilivyomo katika mbingu na ardhi, na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Sala yake na namna ya kumtakasa kwake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuyajua wayatendayo. Sura ya 24 ya Annur aya ya 41.

Wakati Nabii Zakaria AS alipotoka katika mihrabu yake aliwaamrisha qaumu yake kusoma tasbihi. Aya ya 11 ya Sura ya 19 ya Maryam inasema:

فَخَرَجَ عَلَى قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَى إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا

Basi akawatokea watu wake kutoka mihirabuni. Akawaashiria: Msabihini Mwenyezi Mungu asubuhi na jioni.

Nabii Musa AS alimuomba Mola wake amjaalie kaka yake Haruna kuwa waziri wake ili amsaidie katika tasbihi na dhikri. Aya za 29 hadi 34 za sura ya 20 ya Taha zinasema:

وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي. هَارُونَ أَخِي. اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي. وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي. كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا. وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا

 Na nipe waziri katika watu wangu, Harun, ndugu yangu. Kwake yeye niongeze nguvu zangu. Na umshirikishe katika kazi yangu. Ili tukutakase sana. Na tukukumbuke sana.

Tasbihi ni dhikri ya watu wa peponi. Mwenyezi Mungu amesema:

دَعْوَاهُمْ فِيهَا سُبْحَانَكَ اللَّهُمَّ

Mwito wao humo utakuwa: Subhanaka Llahumma “Umetakasika Ee Mola wetu! Sura ya 10 ya Yunus, aya ya 10.

Tasbihi ni dhikri ya malaika. Katika sehemu moja ya aya ya 5 ya Sura ya 42 ya al Shuura, Qur’ani Tukufu inasema:

وَالْمَلائِكَةُ يُسَبِّحُونَ بِحَمْدِ رَبِّهِمْ

Na Malaika wanamtakasa Mola wao Mlezi na kumhimidi.

Kwa hakika tunaishi katika ulimwengu uliosheheni tasbihi kila upande. Lakini huwa hatusikii, au hatuhisi au hatujui au hatujali. Aya za Qur’ani zinasema:

وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ

Na radi inamtaka Mwenyezi Mungu kwa kumhimidi, na Malaika pia kwa kumkhofu.

وَسَخَّرْنَا مَعَ دَاوُودَ الْجِبَالَ يُسَبِّحْنَ وَالطَّيْرَ

Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu

يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ

Vinamtakasa Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini.

وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلاَّ يُسَبِّحُ بِحَمْدِهِ

Na hapana kitu chochote ila kinamsabihi na kumtakasa Allah kwa sifa Zake.

Labda ndugu yangu utajiuliza, tasbihi inafaidisha nini? Tasbihi inaishibisha, inaituliza na kuifanya nafsi kuridhika. Naam, lengo na shabaha bora kabisa kwa kila mtu. Sehemu moja ya aya ya 39 ya Surat Qaf inasema: Na mtakasema Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa. Angalia, angalia jinsi tasbihi ilivyoenea kila lahdha na kila sekunde katika masaa 24 ya siku. Kabla ya kuchomoza na kabla ya kuzama jua, mwanzo wa usiku na mwanzo wa mchana na pembe za usiku na pembe za mchana. Je, umebakia wakati wowote ambao haikuhimizwa tasbihi? Faida za tasbihi ni za duniani na Akhera.

Tasbihi ndiyo njia ya kufikia ridhan nafs. Aya tatu za mwisho za Surat Hijr zinasema:

وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ. فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ. وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّى يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ

Na Sisi tunajua kwa hakika kuwa wewe kifua chako kinaona dhiki kwa hayo wayasemayo. Basi mtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi, na uwe miongoni wanaomsujudia. Na muabudu Mola wako Mlezi mpaka ikufikie Yakini.

Naam, tasbihi ni dawa ya kupoza moyo na ni ponyo bora kabisa la mashaka ya nafsi. Amma swali moja limebakia kwamba je, kuna faida yoyote ya tasbihi katika mambo mengine yasiyo ya thawabu na kuzipa tulizo na tuo nafsi? Naam, sikiliza ndugu yangu. Tasbihi hufuta qadar kwa idhini ya Mwenyezi Mungu. Tasbihi hufuta qadar kwa uwezo wa Allah. Kama alivyosema Muumba wa ulimwengu na mbingu na ardhi saba katika kisa cha Nabii Yunus AS kwamba, Na lau asingelikuwa katika wanaomsabihi na kumtakasa Mwenyezi Mungu, Bila ya shaka angelikaa ndani ya tumbo la samaki mpaka siku ya kufufuliwa.

Sasa utajiuliza, ni tasbihi gani alikuwa akiitaja Nabii Yunus AS ndani ya tumbo la samaki? Alikuwa akisema, Laailaha Illah Anta Subhanaka. Hakuna mungu ila Wewe, Umetakasika.

Naam, tasbihi hufuta qadar kwa idhini Yake Allah. Allahumma ja’alna mimman yusabihuka kathira wayadhkuruka kathira. Fasubhanallah wabihamdihi ‘adada khalqih wa ridha nafsih wazinata ‘arshih wamidada kalimaatih.

Tunakuomba Allah utujaalie kuwa miongoni mwa wanaokusabih, kukutasa na kukumbuka mno. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

(Visited 152 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!