Nakala tatu za zamani na za kihistoria hivi sasa zinahifadhiwa katika maktaba moja ya mjini New York, Marekani zikiwa na umri wa zaidi ya miaka 500.
Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi’i umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, iwapo utatembelea maktaba kubwa duniani utagundua kuna nakala nyingi za kihistoria na za zamani sana za Qur’ani Tukufu na sababu yake ni kwamba tangu kale Waislamu wamekuwa wakikipa umuhimu mkubwa sana kitabu hicho kitakatifu. Wamishionari waliokuja katika nchi za Waislamu kwa malengo ya kiistikbari na kikoloni, nao walikuwa wakifanya kazi ya kusoma Qur’ani na kuzifasiri kwa lugha mbalimbali ili kutafuta mbinu na udhaifu wa Waislamu kwa ajili ya kuwakoloni. Hivyo nakala za zamani na za kihistoria zinapatikana kwa wingi katika maktaba za nchi za Magharibi.
Picha za nakala hizo tatu za kihistoria zinazohifadhiwa katika maktaba moja mjini New York, Marekani zimeenea kwenye mitandao ya kijamii na katika maelezo imeandikwa, nakala tatu za kihistoria za Qur’ani Tukufu zinahifadhiwa katika Maktaba ya Morgan mjini New York.
Mtandao wa habari wa al Yaum al Sabi’i umeandika kuwa moja ya nakala hizo za Qur’ani Tukufu ina umri wa miaka 504.
Aliyerusha mtandaoni kwa mara ya kwanza picha za nakala hizo amesema: Msahafu ambao una sura tukufu ya Alfaatiha ni wa mwaka 1580 Milaadia na unatoka katika mji wa Shiraz wa ardhi ya Fars (Iran ya leo).
Msahafu wenye sura tukufu ya al Israa pia ni wa enzi wa utawala wa Othman (Ottoman Empire) mwaka 1832 Milaadia.
Amma msahafu wenye rangi kijani unatoka katika eneo la Kashmir la upande wa India na ni wa mwaka 1800 Milaadia.
Hapa chini tunaweka picha za misahafu hiyo.
Maktaba ya Morgan (The Morgan Library) ya huko New York Marekani imekusanya hazina kubwa za masuala ya fasihi, sanaa na historia. Vitabu vingi vilivyo nadra kupatikana, vimehifadhiwa katika maktaba hiyo. Vingi vya vitabu hivyo ni vya kuanzia karne za kati hadi karne ya 20.
Maktaba hiyo iliasisiwa mwaka 1907 ikiwa ni maktaba mahsusi ya J. P. Morgan na iligharimu dola milioni 1.2 za wakati huo. Mwaka 1924 iligeuzwa kuwa taasisi ya umma na mwaka 1966 iliorodheshwa kuwa moja ya athari za kihistoria za New York.