Msahafu wa kwanza kabisa kuchapishwa katika ukanda wa Asia Mashariki unajulikana kwa jina la Mas-haf Tokyo. Msahafu huo ulichapishwa mwaka 1934 baada ya kuasisiwa kiwanda cha Kiislamu cha kupiga chapa katika mji mkuu wa Japan, Tokyo. Kazi ya uchapishaji huo ilidhaminiwa kifedha na Waislamu kutoka nchi za Japan, Korea na kisiwa cha Taiki. Nakala 500 za Mas-haf Tokyo zilichapishwa wakati huo.

Mtandao wa habari wa “UKR Press” umeripoti habari hiyo na kusema kwamba Waislamu wa Tatarstan waliwasili nchini Japan katika karne ya 19 Milaadia.

Baada ya kuanza vita baina ya Warusi na Wajapani mwanzoni mwa karne hiyo, uhusiano wa Japan na ulimwengu wa Kiislamu uliongezeka sana. Idadi kubwa ya Waislamu akiwemo Sheikh Abdul Rashid Ibrahim ambaye alifukuzwa nchini Urusi kutokana na kufanya tablighi ya Kiislamu, walielekea nchini Japan. Sheikh Abdul Rashid alifika Japan na rafiki yake Akashi ambaye alikuwa ni jenerali wa jeshi la Japan. Sheikh Abdul Rashid Ibrahim alikuwa mubalighi wa Kiislamu, hivyo mara baada ya kuwasili Japan alianza kazi yake ya tablighi na kufanikiwa kuwasilimisha Wajapani wengi.

Mabadiliko makubwa na muhimu ya Kiislamu nchini Japan yalitokea baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia. Mabadiliko hayo makubwa yalichangiwa na kuwasili nchini Japan, mkimbizi aliyejulikana kwa jina la Muhammad Abdul Hayy Qurban ambaye alifukuzwa Turkmenistan na wafuasi wa fikra ya Kimaksi waliokuwa wakipinga mafundisho ya dini na kuweko Mwenyezi Mungu. Kama ilivyo ada, mwanachuoni anapokwenda sehemu huenda na wafuasi wake. Sheikh Muhammad Qurban alihamia Japan na wakimbizi 600 Waislamu kutoka Turkmenistan. Hilo lilikuwa kundi la kwanza kubwa la Waislamu kuhamia nchini Japan, baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia.

MSAHAFU WA TOKYO

Mas-haf Tokyo (Msahafu wa Tokyo)  ulichapishwa kwa lugha ya asili ya Kiarabu tarehe 12 Januari 1934. Nakala 500 kamili za Qur’ani Tukufu zilichapishwa mwaka huo. Msahafu huo ulichapishwa kwa Khat za Qazani (Kazan) kwa herufi zinazosomeka vizuri na juu ya karasi nzuri sana. Ukubwa wa Msahafu huo ulitegemea nakala ya Qur’ani Tukufu iliyochapishwa katika mji wa Kazan mwaka 1913. Mas’haf Tokyo ni Msahafu wa kwanza kabisa kuchapishwa katika ukanda mzima wa Asia Mashariki.

Vifaa na zana za kuchapishia pamoja na herufi za Kiarabu zilizohitajika kwa ajili ya chapa, vilipelekwa nchini Japan mwaka 1928 kutoka Uturuki. Ikumbukwe kuwa wakati huo Uturuki ilikuwa inatawaliwa na Ataturk ambaye kutokana na kuathiriwa vibaya na fikra za Kimagharibi, alikuwa amepiga mafuruku matumizi la lugha ya Kiarabu nchini Uturuki ikiwa ni pamoja na kuandikwa lugha ya Kituruki kwa hati za Kiarabu yaani lugha ya Kitabu hicho cha Allah.

Waislamu wa maeneo mbalimbali ya Asia Mashariki kama vile wa miji ya Tokyo, Seoul, (mji mkuu wa Korea Kusini ya sasa hivi) na kisiwa cha Taiki cha kaskazini mwa Japan walisimamia na kugharamia kikamilifu uchapishaji wa Mas-haf Tokyo. Fedha zilizotumika katika kazi hiyo muhimu ya kheri zilikuwa nyingi yaani zilikuwa takriban Yen elfu mbili (2,000) za Japan. Wakati huo kila dola moja ya Kimarekani ilikuwa ni Yen 4 za Japan). Hivyo fedha zilizotumika kuchapisha Msahafu wa kwanza kabisa katika eneo la Asia Mashariki zilikuwa nyingi sana kulingana na zama hizo yaani mwaka 1934 Milaadia. Kila nakala moja ya Msahafu huo iligharimu takriban Yen 10 za Japan. Baada ya kukamilika zoezi la uchapishaji, Misahafu hiyo, mbali na kugaiwa Waislamu wa Japan, walifikishiwa pia Waislamu wa Tatarstan waliokuwa wanaishi China, Korea, Finland na Poland. Sherehe za uzinduzi wa Mas-haf Tokyo zilifanyika mjini Seoul, Korea. Waislamu wa Tokyo walimpa zawadi ya Msahafu huo, Mfalme wa 124 wa Japan aliyejulikana kwa jina la Hirohito aliyekuwa mfalme wa jadi wa Japan katika miaka ya 1924 hadi 1989. Sasa hivi nakala moja ya Msahafu huo inahifadhiwa katika Makumbusho ya Utamaduni wa Kiislamu katika Msikiti wa Kul Sharif huko Ulitsa Sheynkmana mjini  Kazan katika Jamhuri ya Tatarstan, nchini Russia. Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za Msahafu wa kwanza kabisa kuchapishwa katika ukanda wa Asia Mashariki unaojulikana kwa jina maarufu la Mas-haf Tokyo.

(Visited 119 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!