Msikiti mkuu wa Colombo, mji mkuu wa Sri Lanka ambao ni maarufu kwa jina la Msikiti Mwekundu, ni kivutio cha kipekee kabisa cha utalii kutokana na muundo na usanifu majengo wa aina yake.
Kwa mjibu wa mtandao wa habari wa “atlasobscura” Msikiti huo unaojulikana kwa jina la Jami Ul-Alfar ni jengo la kale na la kihistoria mjini Colombo, Sri Lanka na uko katika moja ya barabara na mitaa maarufu ya mji mkuu huo. Ni moja ya vivutio vikubwa na vinavyopendwa sana na watalii mjini humo.
Kwa mujibu wa mtandao huo wa habari, ujenzi wa Msikiti huo ulianza mwaka 1908 na kumalizika mwaka mmoja baadaye, yaani 1909. Mhandisi na mchoraji wa Msikiti huo anajulikana kwa jina la Saibu Labbe.
Uhandisi wa Msikiti huo umetegemea vielelezo viwili vikuu, muundo wa majengo ya Kihindi ya nchi hiyo pamoja na muundo wa Kiislamu na umefafanana sana na Msikiti Mkuu wa Kuala Lumpur, mji mkuu wa Malaysia.
Ijapokuwa kuna majengo mengine yaliyojengwa kabla ya Msikiti huo huko Colombo, lakini Msikiti wa Jami Ul-Alfar ndio uliobeba nembo ya mji huo mkuu wa Sri Lanka.
Awali Msikiti huo ulikuwa na uwezo wa kuchukua watu 1500 kwa wakati mmoja. Hata hivyo mwaka 1975 wakuu wa Msikiti huo wakisaidiwa na shirika la eneo hilo la Alhajj Umar, walinunua maeneo ya pembeni mwa Msikiti huo na kuupanua ukawa wa ghorofa 6 na sasa hivi una uwezo wa kuchukua Waislamu elfu 10 kwa wakati mmoja kwa ajili ya Sala.
Sasa hivi Msikiti huo una mnara wa saa ambao umezidi kuufanya kuwa aina ya pekee duniani kiasi kwamba popote ulipo katika mji mkuu Colombo, unaweza kuona minara ya Msikiti huoi iliyonakshiwa rangi nyekundu na nyeupe.
Kivutio hicho kikubwa cha watalii nchini Sri Lanka, ni sehemu muhimu ya ibada ya Waislamu wa nchi hiyo.
Hapa chini tumeweka baadhi ya picha za jengo hilo muhimu sana la ibada kwa Waislamu.
Hapa chini tumeweka kipande kifupi cha video kuhusu msikiti huo:
Na hapa chini tumeweka picha kadhaa za msikiti huo