Mkurugenzi wa Idara ya Wakfu ya mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri ametangaza kuwa, kumefikiwa uamuzi wa kusaliwa tena Sala za Ijumaa katika misikiti 500 ya mkoa huo wa kaskazini mwa Misri baada ya miezi kadhaa ya kufungwa.

Mtandao wa habari wa al Shurooq umeripoti habari hiyo na kumnukuu Sheikh Muhammad Yunus, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Wakfu ya mkoa wa Sinai Kaskazini nchini Misri akisema, idara hiyo imejiandaa kufungua upya misikiti hiyo 500 kwa ajili ya Sala za Ijumaa baada ya kupita miezi kadhaa ya kufungwa kutokana na janga la corona.

Amesema, misikiti 500 mikubwa ya mkoa huo itaruhusiwa kusali Sala za Ijumaa kwa kufuata protokali zote za kiafya ikiwa ni pamoja na kupiga dawa misikitini na kuweka alama za kuwafanya Waislamu wasali wakiwa mbalimbali.

Wizara ya Wakfu ya Misri imeweka sheria maalumu za kuhakikisha ibada hiyo inafanyika katika mazingira salama.

Sala hizo zitaanza kusaliwa Ijumaa ya wiki hii ya tarehe 28 Agosti 2020 katika misikiti 500 mikubwa kwenye mkoa wa Sinai Kaskazini.

Mingoni mwa sheria hizo ni kuvaa barakoa, kuchunga masafa ya mtu na mtu, kila mmoja kuwa na msala wake mwenyewe na milango ya misikiti kufunguliwa dakika 10 kabla ya Sala na kufungwa mara moja baada ya Sala.

Sheikh Yunus aidha amesema, maeneo ya kutilia udhu, kumbi kubwa za kufanyia shughuli na maeneo ya ziara hayatofunguliwa kama ambavyo hakutoruhusiwa kufanyika sherehe zozote za mikusanyiko ya watu. Hata Sala za maiti pia hazitoruhusiwa kusaliwa misikiti suala ambalo linaonesha kuwa bado janga la corona ni tishio nchini Misri na kwamba majumba hayo ya ibada hayatofunguliwa kikamilifu ila baada ya kuhakikisha ugonjwa huo umeangamizwa kabisa.

(Visited 15 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published.

error: Content is protected !!