Labda ndugu yangu utakuwa unajiuliza, ni ipi tofauti baina ya neema, riziki na baraka? Nitakwambia. Neema ni kile kinachoingia mkononi mwako. Mfano fedha, unapopata fedha, hii ni neema. Mtu anaweza kuwa ni bilionea, huyu neema zake ni kubwa. Lakini je, unaweza kutumia fedha zote unazopata? Hapana. Hivyo kile kiwango cha fedha unazotumia kwa manufaa yako, hii ndiyo riziki yako. Sasa neema na riziki ambayo inazaa matunda mazuri, hiyo sasa ndiyo baraka. Kwa mfano umekwenda sokoni kununua mchele kilo mbili ukauleta nyumba. Mchele huo ni neema iliyoingia nyumbani mwako. Kati ya kilo hizo mbili za mchele ile sehemu ndogo ya chakula utakachokula wewe ndiyo riziki yako. Sehemu nyingine yoyote iliyoliwa na wengine si riziki yako wala Mwenyezi Mungu hakupanga iwe riziki yako. Sasa nguvu utakazozipata kwa kula chakula hicho, ukazitumia nguvu hizo kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyekupa riziki hiyo, hapo sasa ndio baraka. Baadhi ya watu wanapata neema, lakini hawapati riziki. Baadhi ya watu wanapata riziki, lakini hawana baraka. Kama ni hivyo, sasa ni nini tofauti baina ya kauthar na takathur?

Naam ndugu yangu, neema inapokuwa nyingi ikakosa baraka inaitwa takathur haiitwi kauthar. Lakini baraka inapokuwa nyingi inaitwa kauthar haiitwi takathur. Utaona inasemwa, nyumba ya fulani ni ndogo lakini imejaa baraka. Neema ya fulani si kubwa lakini imepata bahati ya kuwa na baraka. Lakini wengine majengo yao tu ni makubwa, hayana baraka yoyote. Wana nyumba na majengo makubwa kila sehemu, lakini riziki yake ni kutumia zile sentimita chache tu za chumbani kwake kwa kulalia. Ndio maana Mwenyezi Mungu anatuonya vikali kwa kutwambia: Kumekushughulisheni kutafuta wingi, Mpaka mje makaburini! Sivyo hivyo! Mtakujajua! Sura ya 102 al Takathur aya ya kwanza hadi ya tatu. Hilo ni onyo kwa wanaotumia vibaya neema. Lakini linapokuja suala la neema zenye baraka, Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika tumekupa kheri nyingi.” Aya ya kwanza ya sura ya 108 ya al Kauthar.

Surat al Takathur

Nasaha zangu kwako ndugu yangu, usiangalie unachuma fedha kiasi gani, bali angalia fedha hizo zinatumika katika nini? Usijigambe kuwa leo nimeingiza milioni mbili! Hiyo itabakia kuwa ni takathur tu, maadamu hukuichuma kwa njia halali na hukuitumia vizuri kwa manufaa ya viumbe wa Mwenyezi Mungu. Jiulize hizo milioni mbili zimekwenda kwenye nini? Je, zimefanya mambo yenye manufaa, au zimefujwa katika mambo ya kipuuzi? Hili ndilo la kusema, si kusema umekusanya kiasi gani kwa siku. Usijifakharishe kwa unachoingiza, fakhari yako iwe ni unachoingiza unakitumia katika nini? Kipato chako kinaweza kuwa kidogo, lakini chenye baraka, na hiyo ndiyo kauthar. Lakini kipato chako hata kiwe kikubwa kiasi gani, maadamu hukitumii katika mambo yenye baraka, hiyo ni takathur mbayo Mwenyezi Mungu ameitolea onyo kali. Unaweza kuona jengo dogo tu pembeni mwa barabara lakini lina baraka kutokana na mambo ya kheri yanayofanyika kwenye jengo hilo. Ni jengo la ibada, ni jengo la kusaidia wenye haja, ni jengo la kupanga mikakati ya kuwasaidia mayatima ni jengo la kujenga udugu baina ya wanadamu, hiyo ndiyo kauthar, na hiyo ndiyo baraka. Jengo hili la ibada ingawa ni dogo, ni bora mara mia kuliko lile jengo kubwa mara 10 ya hili lakini ndani yake halina baraka yoyote, ni ukubwa wa bure, yaani takathur. Ndugu yangu kuwa mtu wa kauthar utaokoka, usiwe mtu takathur utaangamia. Naam, ukiangalia kwa undani utaona kuwa vitu vingi katika maisha yetu ni neema tu, lakini si riziki zetu; ni riziki za warithi. Mwengine anapewa neema, lakini si tu anakuwa daraja tu la kuwafikishia wengine riziki za neema hiyo, bali pia atakayeadhibiwa na Mwenyezi Mungu ni wewe kwa kutoifikisha neema hiyo kwenye bustani ya baraka. Hivyo si hoja kuwa na neema nyingi, muhimu ni neema hiyo umeipata vipi na umeitumia katika nini? Utaona tunamuoba Mungu nipe mali nyingi, Mwenyezi Mungu akishakupa huwi mshukurivu na hutumii mali hiyo katika mambo ya kheri na kutoa haki za watu zilizoanishwa kwenye mali hiyo. Sasa nini faida ya mali hiyo? Igeuze neema yako kuwa kauthar upate kuokoka. Mungu apishie mbali, njia yetu yoyote tunayotumia kutuletea neema, isiwe njia ya haramu. Mali ya haramu kamwe haina ustahiki wa kuwa riziki yenye baraka. Mali ya haramu inaweza kuja mkononi mwako, lakini haistahiki kuwa na baraka.

Hii hapa chini sauti ya makala hiyo

(Visited 19 times, 2 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!