Waislamu wa Korea Kusini wamegawanyika mafungu mawili, wenye asili ya Korea na wasio na asili ya Kora. Waislamu hao wana tajiriba, uzoefu na daghadagha ambazo  ni simulizi za kuvutia. Licha ya kuenea wimbi la maambukizi ya kirusi cha corona, Waislamu hao wameendelea vizuri na dasturi na ibada zao kwa kuchunga vilivyo protokali za afya.

Shirika la Habari la Yonhap limeripoti kuwa, Ijumaa ya tarehe 16 Oktoba, 2020; sauti ya adhana katika Msikiti Muu wa Seoul, mji mkuu wa Korea Kusini ilisikika saa sita na dakika 40 mchana kwa majira ya eneo hilo, na Waislamu wengi walishiriki katika ibada ya Sala ya Ijumaa kwa kuchunga kikamilifu miongozo ya watu wa afya kama vile kuchunga masafa na kuvaa barakoa.

Imam Abdul Rahman Lee Ju-Hwa

Wengi wa Waislamu walioshiriki kwenye ibada hiyo walikuwa ni wageni. Walikuwa wa rika na umri tofauti kuanzia watoto wadogo hadi watu wazima wenye umri mkubwa. Waislamu wenye asili ya Korea nao walishiriki ibada hiyo.

Sheikh Lee Ju-Hwa (Abdul Rahman), Imam wa Msikiti huo alisoma khutba za Ijumaa kwa lugha tatu za Kiarabu, Kiingereza na Kikorea na ibada ya Sala hiyo ilidumu kwa muda wa takriban dakika 30.

Kamati ya Msikiti huo imetangaza kuwa, Waislamu 400 walishiriki kwenye Sala ya Ijumaa siku hiyo suala ambalo linaonesha ongezeko kubwa la Waislamu waliojitokeza katika Sala hiyo wakati huu wa kipindi cha maambukizo ya kirusi cha corona. Katika Sala nyinginezo zisizo za Ijumaa, Waislamu wapatao 50 hushiriki kwenye ibada hizo, wakiwemo wenye asili ya Korea na Waislamu kutoka nje ya nchi hiyo.

Muislamu aliyejitambulisha kwa jina la Joong (30) ambaye ni Mkorea aliyesilimu hivi karibuni anasema kuhusu namna alivyovutiwa na Uislamu na kuamua kusilimu akisema, aliutambua Uislamu akiwa Chuo Kikuu wakati alipoonana na Waislamu na kufanya urafiki nao na kuvutia na tabia zao.

Miaka Mitano ya Ongezeko la Waislamu Korea

Sasa hivi idadi ya Waislamu Korea Kusini wanakadiriwa kufikia 60,000. Kwa mujibu wa Umoja wa Waislamu wa nchi hiyo, idadi ya Waislamu katika mji mkuu wa nchi hiyo Seoul ni 5,000 na hivi karibuni Waislamu wengine 5,000 wameongezeka katika idadi ya Waislamu huko Korea Kusini.

Vile vile kuna misikiti 16 katika maeneo mbalimbali ya mji mkuu Seoul. Katika maeneo mengine ya Korea Kusini kuna misikititi 80 mikubwa na midogo. Mwaka 2018 idadi ya Waislamu wenye asili ya Korea Kusini na wasio na asili ya nchi hiyo walikadiriwa kufikia laki mbili na 60 elfu. Wengi wa Waislamu hao ni wale waliofanya kazi katika nchi za Mashariki ya Kati na kuingia katika dini tukufu ya Kiislamu. Wanaporejea Korea wanafanya tablighi, huwa wamebadilika kitabia, wanakuwa na maadili mazuri zaidi na hawanywi tena pombe, masuala ambayo yanawavutia Wakorea wengine kufanya utafiti kuhusu dini hii tukufu ya Mwenyezi Mungu.

Uzoefu unaonesha kuwa, mara nyingi Wakorea wanasilimu wanapokutana na Waislamu, wanapoamiliana nao au wanapoishi katika nchi za Waislamu. Choi ni Muislamu mwingine mwenye asili ya Korea ambaye kabla ya kuwa Muislamu alikuwa Mkatoliki. Aliutambua Uislamu wakati alipokuwa anafanya kazi katika shirika pamoja akiwa pamoja na Waislamu. Alivutiwa na tabia za Waislamu hao hasa alipowaona vipindi vitano vya Sala haviwapiti. Aliona jinsi wanavyoheshimu wakati, hivyo aliamua kufanya utafiti kuhusu Uislamu na baadaye alisilimu.  Anasema wakati alipokuwa anafanya utafiti aligundua kuwa kuna mambo mengi yanayofanana baina ya Uislamu na Ukristo hasa kwa vile Uislamu na Qur’ani imemtaja kwa njia nzuri sana Yesu (Nabii Isa AS) na mama yake na kutoa hoja zinazoonesha kuwa Yesu si Mungu na wala si mwana wa Mungu. Mwaka 2007 wazazi wawili wa Choi walipinga sana uamuzi wake wa kuwa Muislamu kwani walikuwa wanaamini kuwa Uislamu ni dini ya watu waliopotea. Hata hivyo walipoona kwamba mwana wao amekuwa na tabia nzuri baada ya kuwa Muislamu na anaendelea vizuri tu na maisha yake bila ya matatizo yoyote, upinzani wa wazazi wake uliondoka. Baada ya hapo walianza kumsaidia kupata chakula cha halali na kumrahisishia njia za kutekeleza vizuri ibada zake kama Waislamu wengine.

Daghadagha (wasiwasi) wa kupata chakula cha halali

Katika mahojiano aliyofanyiwa, Choi anasema, tabu pekee anayoipata akiwa Muislamu nchini Korea ni kupata chakula cha halali. Anasema, Waislamu nao ni binadamu na natamani kuona vyombo vya habari vinaeneza taarifa na habari sahihi kuhusu Uislamu.

Moon Sung-joo, ni Muislamu mwingine mwenye asili ya Korea mwenye umri wa miaka 41 ambaye alizaliwa Saudi Arabia na baba yake alikuwa mkuu wa kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha ubalozi wa Korea Kusini. Moon amesoma nchini Korea Kusini bila ya kunyapaliwa na kunyanyaswa au kufanyiwa istihzai na wanafunzi wenzake kwa kuwa kwake Muislamu.

Moon Sung-joo anasema: Nitakuwa nimesema uongo kama nitadai kwamba sikumbani na matatizo yoyote. Wakati watu wanaponiona ni Muislamu wanashangaa. Ninajaribu kuwa na maisha yanayokwendana na hali ilivyo kwani Korea Kusini si nchi ya Kiislamu. Nikiwa kazini pia sipati matatizo yoyote ya kimsingi ninapoamiliana na wafanyakazi wenzangu. Moon alioa nchini Tunisia wakati alipokuwa anafanya kazi katika shirika moja na sasa hivi anaishi nchini Korea Kusini. Mke wake anafanya kazi ya tarjama katika shirika la ustawi wa programu za simu za mkononi. Anasema, baadhi ya wakati mke wangu huwa chini ya mashinikizo anapokumbana na Wakorea ambao hawana mtazamo mzuri kuhusu Uislamu.

Umaarufu wa mtu mashuhuri (Celebrity)

Song Bora ni mtu mashuhuri wa mitandao ya kijamii ambaye naye ni Muislamu mwenye asili ya Korea. Ana wafuasi laki mbili katika mtandao wa kijamii wa Instagram. Ni maarufu sana kati ya wanawake Waislamu wasio Waarabu kwani anatumia mbinu yake ya kipekee ya kufunga hijabu zake. Anaoanisha vizuri uvaaji wake wa vazi la staha la Hijab na nguo za jadi za Korea.

Song Bora anapokea “comments” nyingi kutoka kwa wafuasi wake katika Instagram na wote wameonesha kuvutiwa na uvaaji wake wa Hijab. Pamoja na hayo hasalimiki na mitazamo mibaya waliyo nayo baadhi ya Wakorea kuhusu Uislamu. Anasema: Kila siku napokea “comments” nyingi ambazo zina mitazamo hasi na mibaya kuhusu Uislamu. Ni zile za watu wanaodhani kuwa Waislamu ni magaidi.

Usomaji wa Qur’ani Tukufu

Park Dong Shin Imam wa msikiti raia wa Korea Kusini ambaye ana wafuasi wengi pia katika mitandao ya kijamii ya YouTube na Facebook alisilimu mwaka 2009 na sasa ni mwakilishi wa Jumuiya ya Waislamu ya Amani nchini Korea Kusini. Anaendesha harakati zake katika nyuga tofauti hasa za kupiga vita ugaidi na kueneza mafundisho ya Uislamu.

Anasema: Usomaji wa Qur’ani wa Wakorea umewavutia watu wengi nje ya nchi hiiyo. Ijapokuwa baadhi ya wakati anakumbana na “comments” mbaya za chuki na za kiafiriti, lakini anaendelea bila ya kusita na harakati zake na anaamini kwamba Korea Kusini itakuwa ni kigezo bora cha nchi ambayo Waislamu wanaishi kwa amani na utulivu.

Picha Irfin Maaz (24) ni Muislamu anayeishi Korea Kusini kutoka nchini Indonesia. Hivi sasa anaendelea na masomo katika Chuo Kikuu kimoja mjini Seoul. Anasema, utamaduni wa Korea una wapenzi wengi Mashariki ya Kati na Kusini Mashariki mwa Asia. Wakati Muislamu Mkorea anapokwenda kwenye maeneo hayo anapokewa vizuri hata kama atakuwa ni mtu wa kawaida tu.

Kuanzisha jumuiya za Wanachuo Waislamu

Kutokana na kuongezeka idadi ya Waislamu nchini Korea Kusini, wanafunzi wa vyuo vikuu nchini humo wamelazimika kuanzisha jumuiya zao. Moja ya jumuiya hizo ni ile inayoitwa “Jumuiya ya Wanachuo Waislamu” ya Chuo Kikuu cha Seoul. Kila wiki jumuiya hiyo inasimamia Sala ya Ijumaa. Mkuu wa jumuiya hiyo anasema: Jumuiya yetu ina wanachama 170 na baadhi yao ni Waislamu wenye asili ya Korea. Mikahawa ya Chuo Kikuu inatoa pia chakula halali ingawa hivi sasa huduma hiyo imesitishwa kutokana na kuenea ugonjwa wa COVID-19. Nimeonana na Waislamu wengi na sioni tofauti yoyote baina ya Waislamu wenye asili ya Korea na wale wasio na asili ya Korea.

Muhammad Usama ambaye naye ni kiongozi wa Jumuiya ya Wanachuo Waislamu nchini Korea Kusini anasema: Wakati watu wasio Waislamu wanapoonesha hamu ya kuwa Waislamu, wanaruhusiwa kushiriki katika ratiba za jumuiya yetu. Tuna ratiba mbalimbali za Qur’ani na shughuli nyingine za Kiislamu ili kuitangaza dini hii tukufu kwa njia nzuri kati ya Wakorea.

Tarjama ya Qur’ani Tukufu

Tarjama ya Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Korea nayo ina wafuasi wengi sana na kila siku idadi ya wanaonunua Misahafu yenye tarjama ya lugha ya Korea, wanaongezeka.

Moon Song-Joo anasema: Waislamu wenye umri wa miaka 60 na zaidi nchini Korea Kusini wana mitazamo tofauti na Waislamu vijana wa miaka 20 na 30. Waislamu wenye umri mkubwa wanaamini kwamba Uislamu na sheria zake inabidi zibakie kama zilivyo. Hata hivyo Waislamu vijana wanapenda Uislamu wenye mwamko wa kisasa bila ya kutoka kwenye misingi ya dini hii tukufu. Wanataka kuweko uhuru wa kutoa watu mitazamo yao, uhuru wa mijadala kuhusu Uislamu na kuwaachia watu wawe huru kuuliza na kudadisi kila wanaloona hawalielewi.

(Visited 139 times, 1 visits today)
One thought on “Waislamu wa Korea Kusini + Picha”

Leave a Reply to Muislamu mpya wa Korea alivyoathiriwa na tartili ya Qur’ani Tukufu Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!