Mhadhiri mmoja wa chuo cha lugha na fasihi ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Sidney nchini Australia amesema kuwa, kwa mara ya kwanza Lugha ya Qur’ani wataanza kusomeshwa wanafunzi wa lugha ya Kiarabu nchini humo jambo ambalo litatoa fursa kwa wanachuo hao kujifunza njia za tafsiri na maana za aya za Qur’ani Tukufu.
Kwa mujibu wa mtandao wa “SBS Arabic 24” mhadhiri huyo wa chuo kikuu, Ali Yunus al Dahsh ambaye anasomesha lugha na fani za tarjama katika chuo cha fasihi na sayansi ya jamii cha Chuo Kikuu cha Sidney amesema, somo hilo jipya limebuniwa kutokana na kuhisika haja kubwa ya kielimu ya kusomeshwa somo la Lugha ya Qur’ani au “Kiarabu cha Qur’ani” wanachuo wa lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Sidney.
Kuna tofauti baina ya Kiarabu cha Qur’ani na lugha iliyozoeleka ya Kiarabu
Mhadhiri huyo wa chuo kikuu aidha amesema, hadi hivi sasa somo kama hilo halijawahi kusomeshwa kwenye chuo chochote cha Australia katika historia yote ya nchi hiyo.
Amesema, kuna tofauti baina ya lugha ya Qur’ani na lugha ya Kiarabu inayotumika leo katika magazeti na kwenye vyombo vya habari na inayosomeshwa katika taasisi za kufundishia lugha ya Kiarabu. Sasa hivi Kiarabu cha Qur’ani watasomeshwa wanafunzi wote wa lugha ya Kiarabu, wawe wale ambao Kiarabu ni lugha yao ya asili, au wale wenye shahada za uzamili au wanafunzi wa lugha ya Kiarabu wa daraja nyinginezo huko Australia.
Amesema, kwa mtazamo wake njia bora kabisa ya kufasiri Qur’ani Tukufu ni kutumia njia ya utambuzi wa kina wa lugha ya Kitabu hicho kitakatifu, fasihi na isimu yake.
Mhadhiri huyo wa Chuo Kikuu cha Sidney nchini Australia pia amesema, somo la “Kiarabu cha Qur’ani” ni somo gumu zaidi kwa wanafunzi wa lugha ya Kiarabu kwani wanafunzi wanahitajia kufanya kazi ya ziada kuelewa lugha na misamiati ya Qur’ani Tukufu.
Somo hilo la Lugha ya Qur’ani au Kiarabu cha Qur’ani litaanza kusomeshwa mwezi Agosti 2021 katika Chuo Kikuu cha Sidney huko Australia.