Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC Jumatano, Januari 27, 2021 imekuwa mwenyeji wa kikao cha kuzungumzia mateso ya Waislamu wa jamii ya Rohingya. Kikao hicho kilichofanyika kwa njia ya Intaneti kimehudhuriwa pia na Kamishna Mkuu wa Wakimbizi wa Umoja wa Mataifa na timu ya watu wanaofuatilia masuala ya Waislamu wa jamii ya Rohingya ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuangalia hali ya kibinadamu ya Waislamu hao waliofukuzwa nchini kwao na mabudha wa Myanmar.
Mtandao wa lugha ya Kiarabu wa shirika la habari la BNA umeripoti habari hiyo na kumnukuu mkuu wa sekretarieti ya OIC ambaye pia ni Mshauri wa Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo katika masuala ya Palestina akisema kuwa, OIC inazishukuru nchi na taasisi zote kwa misaada na uungaji mkono wao kwa Waislamu wa jamii ya Rohingya. Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Waislamu wa Rohingya ni miongoni mwa jamii zilizopata mateso makubwa sana katika miaka ya hivi karibuni.
Kiongozi huyo mwandamizi wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC pia amegusia ahadi thabiti za jumuiya hiyo za kuwasaidia Waislamu wa jamii ya Rohingya na kutaka ushirikiano wa kimataifa na kugawama majukumu kwa ajili ya kutatua mgogoro huo wa kibinadamu hasa wakati huu wa maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19. Kwa upande wake, Ibrahim Khayrat, mwakilishi wa OIC katika masuala ya Myanmar amesema, jumuiya hiyo inaendeleza juhudi zake zisizosita kwa ajili ya kutatua hali ya kibinadamu na kisiasa pamoja na kulinda haki za Waislamu hao waliouliwa kinyama, kuchomewa nyumba na mashamba yao na kuteswa kupindukia na wanajeshi na mabudha wa Myanmar.