Jumuiya ya Kuhuisha Mirathi za Kiislamu nchini Kuwait imefanya sherehe za kuwaenzi na kuwapa zawadi washindi wa mashindano ya 21 ya hifdh na qiraa (tajwidi) ya Qur’ani Tukufu.
Mtandao wa habari wa “Emeknes” umetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, sherehe hizo zimehudhuriwa na Tariq Issa, Mudiri wa Jumuiya ya Kuhuisha Mirathi ya Kiislamu nchini Kuwait.
Sherehe hizo zimefunguliwa kwa tilawa (tajwidi) ya aya za Qur’ani Tukufu zilizosomwa na Ustadh Sultan al Swarim ambaye ni miongoni mwa washindi wa qiraa wa mashindano hayo. Baada ya hapo Sheikh Jasim al Misbah, mudiri wa vituo vya kuhifadhi Qur’ani Tukufu vya Jumuiya ya Kuhuisha Mirathi ya Kiislamu ya Kuwait amehutubia sherehe hizo.
Katika hotuba yake hiyo, Sheikh al Misbah amezungumzia umuhimu wa kuhifadhi na kujifunza Qur’ani Tukufu na kusisitiza kwamba, Qur’ani ni mwanga unaoyatia nuru macho na nyoyo za wanadamu na kuwapa nguvu za kukabiliana na njia potofu na ujinga.
Pia amesema, mashindano ya 23 ya Qur’ani Tukufu ya huko Kuwait yaliwashirikisha watoto wadogo na mabarobaro wa daraja mbalimbali za elimu kuanzia elimu za awali hadi vyuo vikuu. Kategoria za mashindano hayo zilikuwa ni pamoja na hifdh juzuu moja, mbili, tatu na nne. Mashindano ya wazi yalihusu kategoria za hifdh juzuu 5, 10, 15, 20, 25 na 30 (msahafu mzima). Watu wanane wamekuwa washindi wa mashindano hayo ambao ni wanaume watano na wanawake watatu.