Mgombea wa urais kwa tiketi ya chama cha Democrats nchini Marekani ametuma ujumbe kwenye Kongamano Kubwa la Kila Mwaka la Waislamu wa Amerika Kaskazini (ISNA) na kusema kuwa, siku ya kwanza kabisa ya kuingia kwake madarakani atafuta marufuku inayowazuia Waislamu kuingia nchini humo ambayo imewekwa na rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump.
Biden ni mshindani mkubwa wa Donald Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu. Amesema ni fakhari kwangu kupata fursa hii ya kuzungumza moja kwa moja na jamii ya Waislamu wa Amerika Kaskazini.
Ameongeza kuwa, suala la kusikika sauti ya Waislamu nchini Marekani ni muhimu lakini mara nyingi sauti hiyo haisikiki wakati ni haki ya kiraia na kikatiba ya Waislamu wa Marekani kusikika sauti yao.
Mpinzani huyo mkubwa wa Donald Trump katika uchaguzi ujao wa nchini Marekani pia amesema: Tunajua kwamba Waislamu (Marekani) muda wote wamekuwa wakinyanyaswa na Trump na serikali yake. Jamii ya Waislamu ilikuwa ya kwanza kuathirika na sheria iliyowekwa na Trump ya kupiga marufuku Waislamu kuingia Marekani. Wamehisi athari za chuki dhidi ya Waislamu na watu wasio Wazungu. Matokeo ya kueneza chuki (nchini Marekani) tumeyaona nayo ni kuenea chuki dhidi ya Waislamu na mtukio mengine mbalimbai mabaya yaliyowafika Waislamu. Watoto mashuleni wananyanyaswa na uhalifu unatokana na chuki umeongezeka Marekani.
Ameongeza kuwa: “Migogoro imeongezeka sana (nchini Marekani) katika kipindi cha utawala wa Trump. Ameshindwa kuliongoza vizuri taifa kukabiliana na janga la corona, ameharibu uchumi (wa Mrekani) na ukandamizaji wa polisi na propaganda za kwamba Wazungu ni bora kuliko watu wengine ni sehemu nyingine ya migogoro hiyo iliyoletwa na Donald Trump. Tab’an Waislamu wenye asili ya Afrika ndio walioathiriwa zaidi na siasa hizo za Trump. Tunahitaji kuwa na rais ambaye ataruhusu sauti za watu wote zisikike; ambaye atajali vizazi na dini zote na kuwaunganisha wananchi (wa Marekani).” Vile vile amesisitiza kuwa: Iwapo nitachaguliwa kuwa Rais, nitahakikisha makamu wangu anasikiliza mitazamo yenu (Waislamu) katika maamuzi yote. Siku ya kwanza kabisa ya kuingia madarakani nitaondoa marufuku ya Waislamu kuingia Marekani. Nitakuwa Rais niliye pamoja nanyi wala sitakuwa Rais ambaye anaiona jamii yenu Waislamu kuwa ni ya kulaumiwa.