Bunge la Ufilipino, Jumanne, Januari 26, 2021 lilipasisha Siku ya Taifa ya Hijab ikiwa ni sehemu ya mpango maalumu wa kuheshimu na kuenzi vazi hilo la staha la mwanamke wa Kiislamu.

Mtandao wa habari wa “SunStar Philippines” wa lugha ya Kiingereza umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, bunge la Ufilipino limepasisha muswada huo kwa wingi mutlaki wa kura. Kuanzia sasa tarehe Mosi Februari kila mwaka inahesabiwa kuwa ni Siku ya Taifa ya Hijab nchini Ufilipino.

Bunge la Ufilipino lina wabumbe 203. Muswada nambari 8249 wa Siku ya Taifa ya Hijab umepasishwa kwa kura za ndio za takriban wabunge wote wa nchi hiyo.

Shabaha ya mpango huo ambao ulipendekezwa bungeni na Ansaruddin Abdul Malik Adiong na Amihilda Sangcopan ni kuongeza welewa wa mila na desturi ya Waislamu ya kujisitiri vizuri kwa kuvaa vazi la staha la Hijab kwa amri ya dini yao. Lengo hasa ni kuwahamasisha wanawake wasio Waislamu wa Ufilipino kujua hadhi ya kuvaa nguo za staha na kufuta welewa ghalati na usio sahihi unaoenezwa na maadui wa Uislamu wanaodai kuwa vazi la staha la Hijab ni nembo ya kumdhulumu mwanamke na kumyima uhuru wake. Lengo kuu la mpango huo ni kufuta ubaguzi kwa wanawake Waislamu wanaovaa Hijab.

Hijab ni vazi la staha, linalompa heshima mwanamke wa Kiislamu. Nyuso hizi za furaha kabisa haziwezi kuwa za watu wanaokandamizwa

Lengo jingine la kupasishwa Siku ya Taifa ya Hijab huko Ufilipino ambayo ni tarehe Mosi Februari, ni kulinda haki za wanawake Waislamu kutekeleza kwa uhuru mafundisho ya dini yao na kuthibitisha kivitendo kuwa vazi la staha la Hijab ni nembo ya heshima na kujistahi, si kudhalilishwa wanawake. Shabaha nyingine ni kujenga utamaduni wa kuvumiliana na kuishi kwa kupendana watu wa dini na tamaduni tofauti huko Ufilipino. Baada ya kupasishwa muswada huo, sasa taasisi za serikali, shule na sekta binafsi zitahamasishwa kutoawabagua wanawake Waislamu wanaovaa Hijab na kuwapa haki sawa na wafanyakazi wote wengine.

(Visited 8 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!