Vyombo mbalimbali vya habari likiwemo shirika la habari la Sputnik na mtandao wa habari wa “alkompis” vimeripoti habari ya kupigwa marufuku maandamano ya maadui wa Uislamu ambao walikusudia kuchoma moto Qur’ani Tukufu leo Ijumaa nchini Sweden.

Rasmus Paludan mwanasiasa wa Denmark anayechukia mno wageni hasa Waislamu alikuwa amepanga kukichoma Kitabu kitakatifu cha Qur’ani nje ya msikiti huko Malmö katika wilaya ya Rosengård nchini Sweden lakini polisi wamepiga marufuku jambo hilo na kusema kuwa, kuchoma Kitabu kitakatifu cha Waislamu tena katika siku ya Ijumaa ni uchochezi wa wazi ambao hauwezi kuruhusiwa.

Hatua hiyo ya polisi wa Sweden imechukuliwa baada ya jumuiya 18 za Kiislamu kuandika barua ya kuonya kuhusu uchokozi huo wa wazi wazi dhidi ya Waislamu.

Rasmus Paludan, mwanasiasa wa Denmark mwenye chuki mno na Waislamu

Mwezi Machi mwaka jana pia 2019 na baada ya gaidi mmoja mzungu kufanya mauaji ya kinyama dhidi ya Waislamu katika misikiti miwili nchini New Zealand, adui huyo wa Uislamu ambaye pia ni wakili, alichoma moto msahafu katika uwanja ambao Waislamu walikuwa wamesali Sala ya Jamaa nchini Denmark. Mahakama ya Denmark ilimpa adhabu ya kifungo cha miezi mitatu jela na marufuku ya miaka mitatu ya uwakili kutokana na kitendo chake hicho cha kiuadui.

Ni vyema tukaashiria hapa kwamba, yule mzungu gaidi, Brenton Tarrant, aliyewaua kwa umati Waislamu waliokuwa wanasali katika misikiti mwili ya mji wa Christchurch nchini New Zealand tarehe 15 Machi 2019 amehukumiwa adhabu kubwa zaidi kuwahi kutolewa nchini humo na amepigwa marufuku kuomba radhi au hata kutoka jela kwa sababu yoyote ile.

Jaji Mkuu wa New Zealand, Cameron Mander, amesema, ukatili uliofanywa na Tarrant (raia wa Australia) katika nchi hiyo nyingine dhidi ya Waislamu ni mkubwa mno kiasi kwamba hauwezi kufidia chochote hata kama katili huyo atafungwa jela umri wake wote.

(Visited 41 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!