Hii ndiyo dunia. Yule mwenye akili nyingi, hana bidii. Yule mwenye bidii kubwa hana fikra za kutosha. Yule mwenye moyo wa kutoa ni maskini na yule bakhili asiyependa kusaidia, mali yake ni nyingi na fungu huja juu ya fungu. Yule ambaye ukimpa watoto kumi atawalea kwa njia bora kabisa, ana mtihani wa kutozaa na yule mwenye watoto wengi, hashughulishwi na malezi bora. Katika ndoa ukimpata mwenza mwenye sura nzuri, aibu yake anakosa uaminifu, na ukimpata mwaminifu, basi hana sura nzuri.

Mtu anaweza kujiuliza, hii dunia haina mwenyewe? Nani anayeendesha mambo ya hii dunia? Kwa nini mambo yote yamejaa ukinzani, hakuna kimoja kilicho kamili? Huo lakini ni mtazamo potofu wa baadhi ya watu. Kwani unapoiangalia dunia kwa juu, utaona kwamba kila kitu kimewekwa sehemu inayostahiki kuwepo. Mwenyezi Mungu ameiumba hivi dunia tena kwa makusudi.

Dunia ni chombo cha kukusanya mikinzano na mambo yasiyo kamili. Imeumbwa hivyo dunia. Kila sehemu utaona kuna nguvu imewekwa kwa makusudi ili kuparaganya milingano katika maisha. Aliyeiumba dunia ameiumba kwa namna ambayo ndani yake kila kitu chake si kikamilifu kwa maana ya kwamba asiye na hiki ana hiki ambacho hiki hakiko huku. Ameiumba dunia kwa namna ambayo hamna ndani yake starehe kamili. Ni kama vile kila kitu kimefanywa kisipindukie asilimia 40 ya uhalisia wake. Hakuna kizuri kisicho na kasoro. Mwenye furaha katika ndoa utamuona hana pesa. Mwenye pesa utaona ana mtoto mgonjwa na manung’uniko hayeshi nyumbani. Yule mwenye pesa na utulivu katika ndoa yake, utamuona hata mtoto wa dawa hana. Dunia imeumbwa hivyo.

Wala usijitie magharibi ya roho kutafuta falsafa ya kwa nini imekuwa hivyo wakati Mwenyewe Mwenyezi Mungu amesema katika sura ya 90 ya al Balad aya ya nne kwamba Kwa hakika tumemuumba mtu katika taabu. لَقَدْ خَلَقْنَا الإِنسَانَ فِي كَبَدٍ usijitie wahka wa roho, hivi ndivyo ilivyoumbwa dunia. Ukijiuliza swali, kama Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu katika tabu, basi kwa nini amemuumba. Je, amemuumba mwanadamu ili amtese? Majibu ni hapana. Bali hivi ndivyo duniani ilivyoumbwa na huu ndio usahihi wake, kinyume chake ni kwenda kinyume na malengo ya kuumbwa dunia.

Imeumbwa hivi dunia. Hakuna kitu rahisi, utoke jasho ndipo utakipata

Nikupe mfano. Kila mmoja wetu ameshakwenda Benki na kuona wanavyofanya kazi wahudumu wa benki. Hivi imewahi kukupitikia ujiulize, kwa nini muhudumu wa benki hana vifaa vya ujenzi na ufundi, bali amezungukwa na kompyuta, printer, calculator na mashine ya kuhesabu pesa? Swali hili halikupitikii akilini kwa sababu unajua kwamba, hivi ndivyo ilivyopangwa kuwa benki na hivi ndivyo muhudumu wa benki anavyopaswa kuwa. Katika kazi nyingine hali ni hiyo hiyo, kila sehemu ina vifaa vinavyoendana na malengo ya sehemu hiyo. Kwa upande wa dunia ni vivyo hivyo. Mwenyezi Mungu ameiumba dunia kwa malengo aliyoyaumbia maisha ya mwanadamu hapa duniani. Dunia ni konde ya Akhera. Dunia ni kituo cha maandalizi kwa ajili ya maisha ya milele. Dunia ni sehemu ya kupevuka mwanadamu. Naam, kupevuka.

Kupevuka nako hakuwezi kupatikana bila ya tabu. Umepata kumuona mtu aliyepevuka ambaye hakupitia shida na tabu? Hakuna mtu yeyote maarufu duniani ila atakuwa amepitia kwenye tabu mashaka na kuhangaika. John C. Maxwell ndiye aliyekuwa mtu maarufu zaidi katika masuala ya uongozi na kusimamia mambo duniani mwaka 2014. Inadaiwa kuwa Maxwell amelea na kufundisha viongozi milioni sita wakubwa duniani. Katika moja ya nadharia zake ambazo huenda kwa baadhi ya watu zikaonekana ni kitu cha ajabu anasema: Ukitaka kujua mchakato wa kupevuka kwako umesimama na sasa hupevuki tena, basi jipime kwa kutokuwa na matatizo, tabu na mashaka tena katika maisha yako. Ukiona maisha yake yanakwenda kirahisirahisi, basi tambua kuwa mchakato wako wa kupevuka umekwama. Ni kwa sababu hiyo ndio maana muda wote dunia tunaiona inakwenda upande wa kuvuruga mazoea ya watu.

Mazoea maana yake ni kuishi kiurahisirahisi katika mambo yasiyo na tabu na yaliyo rahisi kuyafikia, na hilo haliendani kabisa na mchakato wa kuendelea kupevuka. Ndio maana hakuan wakati wowote ambapo mambo ya mtu ni rahisi. Mwenye fedha hana maisha rahisi, maskini pia maisha yake si rahisi. Maisha ya maskini si rahisi kwa kukosa fedha, maisha ya tajiri si rahisi kwa kudhibiti na kusimamia fedha. Kama huamini, hebu angalia saa wanayoamka mabilionea duniani. Tafuta katika Intaneti, utaona muda wa kuamka mabilionea duniani ni baina ya saa 11 na 12 asubuhi. Swali langu kwako ni kwamba, ni kwa nini mtu ambaye tunamuona hana shinda na fedha hata asipofanya kazi umri wake wote, hana usingizi wa kituo? Ana wasiwasi muda wote? Ili aweze kusimamia na kudhibiti fedha zake, tajiri analazimika kukaa macho hadi usiku mkubwa akijumla fedha na kuangalia madeni na kupiga mahesabu na kupanga ratiba za vikao na semina hizi na zile. Hivi ndivyo dunia ilivyoumbwa.

Niseme pia kwamba, usije kamwe ukafikiria kwamba maisha ya rahisi ni sawa na maisha ya furaha? Hivyo ni vitu viwili tofauti. Duniani unaweza kuishi kwa furaha, lakini huwezi kuishi kiurahisirahisi. Maisha ya kiurahisirahisi ni kitu cha nje kinachoonekana mbele ya macho ya watu, lakini furaha sehemu yake ni moyoni na wewe ndiye unayeiratibu na kupanga kiwango cha furaha yako kulingana na mtazamo wako kuhusu maisha ya duniani. Kimsingi, utulivu na furaha ni nyenzo za kupevuka mwanadamu lakini maisha ya kiurahisirahisi ndiye adui mkuu wa kupevuka mwanadamu.

Kipaji kikubwa cha mtu katika maisha kinaonekana pale anapolinda utulivu na furaha yake katika hali na mazingira yote anayokumbana nayo katika maisha. Huwezi kufikia daraja hiyo bila ya kukubaliana na hali halisi ya duniani na mambo yake yote na kukubali kwa dhati kwamba, duniani ni chombo kilichokusanya ndani yake mikinzano na mambo yanayogongana na yasiyopatana. Ukijua hivyo, muda wote utaishi maisha ya utulivu na furaha, kwani hutotarajia kabisa kwamba kuna siku itapita bila ya tabu, mashaka na mahangaiko. Utaishi vizuri duniani pale utakapokiri kwamba, kupevuka kwako kunapatikana kwa kutatua matatizo yako, si kuyakimbia kwani popote ulipo, matatizo huwezi kuyaepuka.

Hii hapa chini sauti ya makala hiyo

(Visited 50 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!