Kutoka kitabu cha Raudhat al Safa

Bimsillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatu. Luqman ambaye sura ya 31 ya Qur’ani Tukufu imetajwa kwa jina lake, alikuwa Mwafrika wa Habasha sehemu ya Nubia ya Sudan ya leo na aliishi zama za Nabii Daud AS. Alisifika mno kwa hikma zake. Kuna visa vyake vingi vimenukuliwa katika vitabu vya historia, kama kisa chake alipomtembelea Nabii Daud wakati Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu alipokuwa anatengeneza kimiujiza nguo za vita. Jinsi Luqman alivyomuokoa bwana wake kutokana na sharti zito la kunywa maji ya mto na visa vingine vingi. Hata hivyo kwa hivi sasa sisi tutasitia hapa kuhusu mfululizo wa makala fupi fupi za Luqman al Hakim.

Hikma ilivyopelekea Luqman aachiliwe huru

Sababu ya kuachiliwa huru Luqman ilikuwa ni kisa kifuatacho. Siku moja bwana wa Luqman alimtuma aende akapande ufuta shabani. Baada ya muda kupita yule bwana alikwenda shambani kuangalia maendeleo ya kilimo chake. Alishangaa, badala ya ufuta, Luqman alikuwa amepanda uwele. Alimuuliza kwa nini ukafanya hivi Luqman? Luqan alijibu kwa kusema: Nilidhani nikipanda uwele nitavuna ufuta. Bwana wake akamuuliza, imekuwakuwaje ukafikiria kitu kama hicho? Luqman alijibu kwa kusema ni kutokana na vitendo vyako Seyyid yangu. Maana nakuona umeghiriki katika vitendo viovu, lakini bado unataraji kupata pepo. Yule bwana akatulia na kufikiri kwa kina aliyoambiwa. Akasema, hivi vitendo vyangu vyote hivi visivyofaa na viovu, vitaniingiza peponi kweli? Kama nitaingia peponi kwa vitendo hivi, basi itawezekana pia anayepanda uwele, avune ufuta.

Zinduo hilo lilimfanya yule bwana aache kabisa vitendo vyake viovu kwani alipata yakini kwa hikma hizo za Luqman kwamba mtu huchuma anachokipanda. Si hayo tu, lakini pia alimwachilia huru Luqman kama sehemu ya kumshukuru kwa kumzindua na kwa kuhisi kwamba mtu mwenye hikma kama Luqman, hafai kuendelea kuwa mtumwa.

Naam ndugu yangu, wakati tunapoangalia matendo ya watu tutaona kuwa, watu wengi hawajishughulishi na maandalizi ya kweli ya huko twendako, lakini wakati huo huo wanataraji Mwenyezi Mungu atawasamehe na kuwaingiza peponi. Wengi wako katika usingizi mzito na wanadhani kwamba pepo inapatikana bila ya kuitafuta na kujipinda kikwelikweli. Unachokipanda hapa duniani ndicho utakachokivuna kesho Akhera. Dunia ni konde ya Akhera.

Wengi wetu tunakiri kwamba bila ya kufanya ibada hatutoingia peponi, lakini bado tuna tamaa ya kupata pepo. Hatutekelezi vizuri majukumu na ibada zetu, lakini bado tunataraji kupata matokeo mazuri kutokana na matendo yetu maovu au yasiyofanywa kwa uangalifu.

Kama kweli tunataka pepo, basi tusijipumbaze kudhani kwamba tukipanda uwele tutavuna ufuta. Tufanye juhudi za kutekeleza kwa uangalifu na kikamilifu kazi zetu zote kwa ajili ya kutafuta radhi za Muumba wetu katika kila neema ya pumzi tunayovuta.

(Visited 13 times, 1 visits today)
One thought on “Hikma za Luqman (Sehemu ya Nne) Sababu ya kuachiliwa huru Luqman”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!