Nakala ya kale zaidi ya tafsiri ya Qur’ani Tukufu iliyoandikwa kwa hati za mkono inahifadhiwa hivi sasa katika maktaba ya makumbusho ya Alexandria nchini Misri na inavutia watu wengi wakiwemo hata viongozi wa mataifa tofauti duniani.

Mtandao wa habari wa al Yaum al Sab’i umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Tafsiri ya al Busti ya Qur’ani Tukufu ndiyo nakala ya kale zaidi ya tafsiri ya Qur’ani iliyoandikwa kwa hati za mkono. Tafsiri hiyo inahesabiwa kuwa ni nakala ya kale zaidi ya uandishi wa lugha ya Kiarabu kwa mkono.

Nakala hiyo imefasiri baadhi ya aya na sura za Qur’ani Tukufu si Qur’ani nzima. Sheikh Abu Is’haq bin Ibrahim, maarufu kwa jina la al Busti aliyefariki dunia mwaka 307 Hijria ndiye aliyeandika tafsiri hiyo.

Tafsiri hiyo ni ya tangu mwaka 978 sawa na mwaka 368 Hijria. Karatasi zake zimechakaa hivyo hivi sasa zinafanyiwa marekebisho sambamba na kulindwa asili yake.

Nakala hiyo ya tafsiri ya Qur’ani Tukufu imeandikwa kwa kalamu ya Maghribi (Morocco) ambayo ni kalamu ya kale sana. Baadhi ya maandishi yake yanasomeka vizuri lakini baadhi ya sehemu mwandishi hakujisumbua kuandika maneno kiukamilifu pamoja na nukta zake.

Mfumo aliotumia mfasiri wa nakala hiyo ya Qur’ani ni wa kunukuu aya, baadaye kutaja hadithi iliyotafsiri aya hiyo, na baadaye maelezo na mitazamo muhimu iliyotolewa ikiwa ni pamoja na maana za maneno na misamiati kwa ajili ya kutoa ufafanuzi mzuri zaidi wa aya hizo.

Nakala hiyo ni muhimu sana kwani pamoja na mambo mengine, ni uthibitisho kuwa ustaarabu wa kuandika ulianza tangu kale katika ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu.

Tafsiri hiyo iliandikwa mwaka 368 Hijria kwa khati za Khalaf ibn Hakim katika kurasa 333 huku kila ukurasa ukiwa na mistari 31.

Viongozi wengi wa nchi za dunia wanatembelea sana Maktaba na Makumbusho ya Alexandria kutokana na umuhimu wake mkubwa wa kihistoria na turathi za kale.

(Visited 135 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!