Kama tulivyoona katika sehemu ya kwanza ya mfululizo wa makala fupi fupi za Hikma za Luqman, mja huyo wa mwema wa Mwenyezi Mungu, alitekwa nyara na kuuzwa kama mtumwa katika nchi ya Palestina enzi za Nabii Daud AS. Bwana aliyemnunua alikuwa mwenye moyo wa huruma, mwenye akili na busara ingawa si katika matendo yote kama tutakavyoona katika mfululizo wa hikma za Luqman kwenye sehemu zitakazokuja huko mbele tukijaaliwa. Bwana huyu aliamiliana kwa huruma na Luqman na alimuheshimu kutokana na hikma zake.
Kiungo kibaya na hatari zaidi mwilini
Siku moja alitaka kumjaribu Luqman, hivyo alimtuma kuchinja kondoo. Alimwambia baada ya kumchinja mnyama huyu, nilitee sehemu iliyo mbaya na hatari zaidi ya mwili wake. Luqman alitekeleza amri na katika jambo lililomshangaza bwana wake, Luqman alimpelekea moyo na ulimi kuwa sehemu hatari na mbaya zaidi katika mwili wa kondoo. Alipopelekewa, yule bwana alitabasamu na kushangazwa na kupigwa na bumbuwazi kutokana na chaguo hilo la Luqman. Akahoji kwa udadisi akijiuliza moyoni, hivi huyu hakuona kiungo chochote kibaya zaidi kuliko ulimi na moyo? Alijua kuwa Luqman amekusudia kutoa darsa na maana ya kina, lakini kila alivyofikiri ilimuwia vigumu kuelewa nini hasa amekusudia kukibainisha Luqman. Lakini heshima yake kwa mtumwa wake huyo, iliongezeka na ikawa sasa anamfanyia upole zaidi kuliko huko nyuma.
Kiungo kizuri na salama zaidi mwilini
Baada ya siku chache, bwana wa Luqman alitaka kumfanyia mtihani mwingine mja huyo mwema wa Mwenyezi Mungu. Alimpa tena kondoo amchinje, lakini mara hii tofauti na mara iliyofuata, alimtaka amletee kiungo kilicho bora kabisa na kilicho salama zaidi katika mwili wa kondoo. Luqman alitekeleza alivyotumwa na katika jambo la kushangaza, mara hii pia alimpelekea bwana wake ulimi na moyo, kwamba ndivyo viungo salama na vyenye amani zaidi kuliko vyote. Mara hii bwana wake hakusubiri kufikiri majibu, alimuuliza tu moja kwa moja sababu za ulimi na moyo kuwa viungo hatari na salama zaidi, na kuwa viungo vibaya na vizuri zaidi kwa wakati mmoja. Luqman alimjibu, maangamizi yote yanatokana na ulimi na moyo na mafanikio yote ya mwanadamu yanatokana na ulimi na moyo. Inategemea mtu ameamua kuvitumia vipi viungo hivyo viwili. Yule bwana, kama tulivyosema sehemu ya kwanza iliyopita ya hikma za Luqman, alizidi kumuheshimu Luqman, na kimsingi yeye ndiye aliyekuwa mtumwa; na Luqman ndiye aliyekuwa bwana, kwani alikuwa akimsikiliza na kumfuata kila aliyomwambia. Luqman alikuwa anaombwa ushauri na watu wengi na hikma zake zilikuwa maarufu katika kila kona.