Kampeni ya Kimataifa ya kupambana na Ubaguzi wa Israel na kukalia kwake kwa mabavu ardhi za Wapalestina imesema kuwa, Tel Aviv inaendeleza ubaguzi na jinai zake dhidi ya watu wa kawaida huko Palestina.
Hayo yameripotiwa na Kituo cha Upashaji Habari cha Palestina (PIC) na kuongeza kuwa, katika ripoti yake, kampeni hiyo ya kimataifa imesema kuhusu matukio ya nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2022 kwamba Israel imeongeza kasi ya ubaguzi na ukandamizaji wake dhidi ya Wapalestina katika kipindi cha miezi sita ya awali ya mwaka huu.
Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, katika kuendeleza ukandamizaji na ubaguzi wao, viongozi wa Israel wanatumia njia mbili kuu, moja ni kueneza chuki dhidi ya Wapalestina na kupambana na suala lolote ambalo litaimarisha utambulisho wa kikaumu, kiitikadi na kiimani wa Wapalestina.
Mbinu nyingine inayotumiwa na wavamizi hao wa ardhi za Palestina ni kuyasaidia na kuyatia nguvu magenge yenye misimamo mikali hata yenye majina ya Kiislamu kwa ajili ya kujaribu kusahaulisha kadhia ya Palestina na kuzishughulisha fikra za walimwengu katika masuala mengine pamoja na kuutumbukiza Umma wa Kiislamu katika mizozo isiyoisha ya wenyewe kwa wenyewe.
Kituo hicho cha Upashaji Habari cha Palestina (PIC) kimesema pia kwenye ripoti yake kwamba katika kipindi cha miezi sita ya awali ya mwaka huu wa 2022, wanajeshi wa Israel wameshawapiga risasi na kuwaua Wapalestina wasiopungua 57.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, miongoni mwa jinai za Israel zilizoendelezwa katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2022 ni kutanua vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi wanazoporwa Wapalestina, kukanyaga haki za kimsingi kabisa za Wapalestina katika maeneo yote, kuongezeka sana wimbi la kutekwa nyara Wapalestina pamoja na mauaji na mashambulio dhidi ya wananchi wa taifa hilo linalodhulumiwa.