Kongamano kubwa la 57 la kila mwaka la Waislamu wa Amerika Kaskazini (ISNA) mwaka huu limefanyika kufanyika kwa njia ya video na kuwashirikisha viongozi muhimu Waislamu katika masuala ya kidini, kisiasa, kielimu na kiutamaduni.
Hayo yameelezwa na mtandao wa “AboutIslam” na kuongeza kuwa, waendeshaji na wasimamiaji wa kongamano hilo ambalo ni mkusanyiko mkubwa zaidi wa Waislamu Amerika Kaskazini mwaka huu wamefanya kongamano hilo kwa njia ya video kutokana na janga la COVID-19.
Kila mwaka kongamano hilo huwakusanya pamoja maelfu ya viongozi, maulamaa, wanavyuoni pamoja na Waislamu wa kawaida na kujadiliana masuala muhimu.
Hivi sasa suala la uadilifu na usawa baina ya vizazi na mataifa yote duniani ndilo lililoshika kasi katika eneo hilo hivyo kaulimbiu ya mwaka huu ya kongamano hilo imekuwa ni “Juhudi kwa ajili ya Uadilifu wa Kijamii.”
Mtandao wa upashaji habari wa kongamano hilo umesema kuwa, udharura wa kuchunga maadili mema umetufanya tuzingatie maudhui inayohusiana na uadilifu wa kijamii na kizazi (generation) katika nchi zetu na dunia nzima kiujumla.
Kongamano la kwanza la Waislamu wa Amerika Kaskazini lilifanyika mwaka 1963 na liliitishwa na Jumuiya ya Wanachuo Waislamu wa Marekani na Canada.
Kongamano la mara hii la 57 la Waislamu hao limefanyika kwa muda wa siku mbili. Lilianza jana Jumamosi tarehe 5 Septemba na linamalizika leo Jumapili, Septemba 6, 2020 kwa njia ya video.