Baraza la Kiislamu la Uingereza (MCB) kwa mara ya kwanza limemchagua mwanamke kuwa mkurugenzi wake mkuu.
Mtandao wa habari wa al Arabi al Jadid umeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, zoezi la upigaji kura lilifanyika wiki iliyopita na Bi Zara Muhammad amechaguliwa na wajumbe wa Baraza la Kiislamu la Uingereza kuwa mkurugenzi mkuu. Kabla ya Bi Zara, Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo alkuwa Bw. Harun Khan.
Baada ya kuchaguliwa Bi Zara amesema: Nina hamu kubwa ya kuona tuna jopo la Kiislamu linalofanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa katika pande zote na ambalo litaweza kushughulikia mahitaji yote ya Waislamu wa Uingereza.
Amesema, kuchaguliwa kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu ni fakhari kubwa kwangu. Ninatumai kwamba litakuwa chachu ya kuwahamasisha wanawake na vijana kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo na kujitokeza kuchukua nafasi muhimu kwani hao ndio mustakbali wa jamii ya Kiislamu.
Kabla ya hapo Bi Zara Muhammad alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Kiislamu la Uingereza. Ana shahada ya uzamili (Master’s Degree) ya Haki za Binadamu aliyoichukua katika Chuo Kikuu cha Strathclyde ambacho ni chuo kikuu cha pili kwa ukubwa katika mji wa Glasgow huko Uskochi (Scotland). Kazi zake nyingine ni mshauri katika masuala ya elimu na ustawi.
Kabla ya Bi Zara Muhammad, Bw. Harun Khan alikuwa Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo kwa vipindi viwili mfululizo. Baraza la Kiislamu la Uingereza ndilo baraza kuu zaidi la Kiislamu la kidemokrasia nchini humo na linaendesha Misikiti, Madrasa, Shule na Taasisi mbalimbali katika kona zote za Uingereza.