Unyanyasaji na udhalilishaji wa Waislamu unaendelea nchini Ufaransa na tukio la karibuni kabisa ni kuchomwa moto msikiti mmoja kaskazini mwa nchi hiyo.

Shirika la habari la Anadolu limemnukuu Fatih Sarikir, Katibu Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Jamii ya Waislamu (CIMG) akitangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, msikiti uliochomwa moto uko katika mji wa Châteaudun wa kaskazini mwa Ufaransa. Mtu mmoja asiyejulikana ameumwagia mafuta msikiti huo na kusababisha kuwaka moto.

Amesema, moto huo umezimwa kabla ya kusababisha hasara kubwa kwa mali za msikiti huo. Hakuna mtu aliyejeruhiwa katika jinai hiyo.

Kwa mujibu wa Fatih Sarikir, viongozi wa msikiti huo wameshafungua mashtaka kulaani kitendo hicho cha kiuadui na sasa hivi jeshi la polisi linafanya uchunguzi kugundua wahusika kwa njia mbalimbali kama kuangalia video zilizorekodiwa na kamera za msikitini hapo.

Katika taarifa yake nyingine, shirika la habari la Anadolu limeripoti kuwa, jana jeshi la polisi la Ufaransa liliwatia mbaroni watu wawili wa tuhuma za kuandika maneno ya chuki dhidi ya Waislamu katika ukuta wa Msikiti mmoja mjini Pantin katika viunga vya mji mkuu Paris. Msikiti huo umefungwa kwa muda wa miezi sita kwa amri ya mahakama ya Ufaransa.

Jumanne, Oktoba 27, 2020, mahakama ya mji wa Montreuil wa kaskazini mwa Ufaransa ilitoa amri ya kufungwa msikiti wa mjini Pantin wa kaskazini mashariki mwa Ufaransa kwa muda wa miezi 6 kwa madai kuwa masheikh wa Msikiti huo wana misimamo mikali.

Tarehe 19 mwezi ulioisha wa Oktoba 2020, waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa alitoa amri ya kufungwa Msikiti wa mjini Pantin kwa kusambaza mkanda wa video katika mitandao ya kijamii kulaani jinai ya jarida la Charlie Hebdo la Ufaransa ambalo limechapisha tena vibonzo vinavyomvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW. Kwa mtazamo wa viongozi wa Ufaransa akiwemo rais wa nchi hiyo, Emmanuel Macron, kumvunjia heshima Mtume Mtukufu Muhammad SAW eti ni uhuru wa kusema, lakini kulaani kitendo hicho kiovu au kurekodi sauti na video kupinga uovu huo, kwa mtazamo wa viongozi hao, ni uhalifu unaostahiki hata kufungwa Msikiti.

(Visited 39 times, 1 visits today)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

error: Content is protected !!