Makumbusho ya Sanaa ya Kiislamu ya Cairo yameadhimisha mwaka wa 119 tangu kufunguliwa kwake. Jumba hilo la makumbusho lina moja ya mkusanyiko mkubwa wa kustaajabisha na wa kuvutia mno wa kazi za Kiislamu ulimwenguni.
Hayo yameripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari hasa vya Misri ambavyo vimesema, Makumbusho ya Sanaa ya Kiislamu ya Cairo yalifunguliwa rasmi tarehe 28 Disemba 1903, na mara baada ya kufunguliwa kwake, yalihifadhi kazi 4,500 za thamani za Kiislamu.
Jumba hilo la makumbusho lilikuwa la kwanza nchini Misri na eneo zima la Afrika Kaskazini ambalo lilikusanya kazi za kila namna za kisanii za Waislamu. Katika maadhimisho ya mwaka wa 119 wa kuasisiwa makumbusho hayo, Baraza Kuu la Mambo ya Kale la Misri limefanya maonyesho matatu ya muda katika kumbi za jengo hilo.
Mustafa Waziri, katibu mkuu wa baraza hilo la mambo ya kale ndiye aliyefungua maonesho hayo matatu zikiwemo kazi za kale za sanaa za Kiislamu.
Wakati wa ufunguzi huo alisema: Maonyesho ya kwanza yenye jina la “Miaka 119 ya Sanaa na Ubunifu” ni mkusanyiko wa picha, vitabu vya historia na kazi za kumbukumbu zinazohusiana na sanaa ya Kiislamu na ustaarabu wa Kiislamu katika historia. Maonyesho ya pili yamehusiana na mkusanyiko wa kazi 100 za kaligrafia na uandishi wa khat za wasanii maarufu wa Misri, Uchina, Japan, Thailand, Iraqi na India.
Maonyesho ya tatu yamejumuisha nakala saba za kazi bora za Kiislamu zilizotayarishwa kwa ushirikiano na Kituo cha Beit Jameel cha Mfuko wa Sanaa ya Kihistoria na Maendeleo ya Utamaduni.
Jumba hilo la makumbusho lilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 kama Makumbusho ya Misingi ya Waarabu na lilianzishwa kwa mara ya kwanza katika kasri la mtawala wa silisila ya Fatimiyyah Al-Hakim bi Amr Allah.
Jumba hilo la makumbisho la zaidi ya karne moja na miaka 19 limekusanya ndani yake kazi nyingi za kisanii za tawala na silisila zote za viongozi wa Uislamu zikiwemo za enzi wa Bani Ummayah, Bani Abbas, Ufalme wa Uthmaniyyah, Silisila ya Fatimiyya n.k. Jengo hilo linahifadhi hazina kubwa za kazi za kisanii za Mashariki mwa Dunia ikiwa ni pamoja na panga, pazia kongwe zaidi la al Kaaba, miswada ya zamani, kazi ya chuma, vyombo vya kioo, makusanyo ya vyombo vya udongo, mbao, vifaa vya makabila tofauti n.k.
Jumba la Makumbusho la Sanaa ya Kiislamu la Misri liliharibiwa katika mripuko wa bomu wa kigaidi uliolenga Idara ya Usalama ya Cairo mwaka 2014, lakini baada ya kazi kubwa za ukarabati, Jumba la Makumbusho la Sanaa za Kiislamu lilifunguliwa tena mwezi Januari 2017 yaani baada ya kusimama kwa miaka 3.
Jumba hili la makumbusho lina orofa mbili na lina mkusanyiko mkubwa zaidi wa kazi kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu wa Kiislamu. Katika jumba hilo, wageni wanaweza kuona kwa karibu kazi mbalimbali za vipindi tofauti vya historia ya Kiislamu na kuhusu ujuzi na utaalamu wa kila namna wa Waislamu wa kale kama vile unajimu, dawa, usanifu majengo, miswada na ustadi wa kutengeneza na kuhifadhi vitabu.
Miongoni mwa kazi muhimu zaidi zilizohifadhiwa katika jumba hilo la makumbusho, tunaweza kusema ufunguo wa al Kaaba wa enzi za silisila ya watawala wa Mamluk na kitambaa ambacho juu yake kimeandikwa maandishi ya kale zaidi ya hati za Kufi.